Na Said Mwishehe, Michuzi Globu ya jamii
TUKUBALIANE nitakachoelezea hapa hakuna uhusiano na ukweli wa moja kwa moja ila ni mtazamo wangu wa kijinga uliojaa na upumbavu ndani yake.
Nataka kuzungumzia ugonjwa hatari wa COVID-19 ( Corona) ambao umeifanya dunia kuhaha kutafuta kinga yake kwa ajili ya kuokoa maisha ya wanadamu. Corona haina adabu kabisa inakatisha maisha ya watu bila huruma. Ukweli dunia imekosa furaha kabisa kutokana na virusi vya Corona ambavyo havina tiba wala chanjo.
Nenda Italia au nenda Spain utaona huruma mamia ya watu wanapoteza maisha kila siku iendayo kwa Mungu. Ni hatari sana .Jamani jamani jamani ugonjwa huu ni hatari, hivyo ,tuchukue tahadhari kwa kuhakikisha tunajikinga na Corona. Watalaam wa afya wamekuwa wakitoa maelekezo mara kwa mara ya nini tunatakiwa kufanya. Tujiepushe na Corona kwa kunawa mikono kwa maji na sabuni mara kwa mara.
Tuepuke mikusanyiko isiyokuwa ya lazima. Ukweli kwa hapa nchini kwetu angalau watu wake wanafuata maagizo ya Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia, Wazee na Watoto. Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amekuwa mstari wa mbele kutuelimisha.Ahsante Waziri Ummy Mwalimu ,ahsante Serikali ya Awamu ya Tano kwa hatua ambazo mnazichukua kukabiliana na Corona.
Hata hivyo naomba nieleze hapa tena nikiwa na akili timamu kabisa.Meza mate kwanza .Pumzika kidogo... haya tuendelee nasema hivi kwa mujibu wa Waziri Ummy Mwalimu Tanzania tunao wagonjwa 13 wa Corona, ndio idadi ya wagonjwa waliopo na hali zao zinaendelea vizuri.Hata yule mgonjwa wa kwanza wa Corona Isabele Mwampamba amepona na ameruhusiwa. Ahsante Mungu kwa kumponya Isabela na kumrudisha kwenye afya njema.
Pia tunashukuru Mungu kwa upendo wake kwetu, hata wale wagonjwa wetu wa Corona nao wanaendelea vizuri na wameimarika sana .Nakumbuka Rais John Magufuli alisema hali za wagonjwa wa Corona ni nzuri sana na wanaweza kupiga hata pushapu.Kimsingi hapo alikuwa anamaanisha kuimarika kwa afya za wagonjwa wetu.
Ukubwa wa tatizo la ugonjwa huu kila mtu anasema analojua. Ndio! Unashangaa nini? Kwanza naomba angalia pembeni yako kuna nani maana usijisahau kisha ukakuta simu yako imeporwa. Usijisahau ukajikuta kuna mtu anasoma nilichoandika. Ndugu yangu naomba nikwambie hivi majuzi hapa nilipata nafasi ya kumsikiliza Waziri Mkuu wa Italia ,anasema kwa sasa wao wameshakufa kimwili na kiakili na wanamuachia aliyejuu.Ni hatari sana .
Hapa naomba unielewe ninachotaka kukieleza nacho ni hiki; Tunao wagonjwa wenye virusi vya Corona ambao wapo karantini wakiendelea na matibabu.Takwimu za wagonjwa hao kila nchi inayo ya kwake.Hata kwetu Tanzania takwimu zipo. Hivyo tuache kupotosha na bahati nzuri Serikali iko macho, ukipotosha tu imekula kwako.Sitaki kupotosha kuhusu Corona.
Hata hivyo kwa ujinga wangu na kufikiria bila kuwaza na kuwazua nikajikuta najifikirisha kuhusu athari za Corona.Nikapata jibu wapo wenye virusi vya Corona na hao wapo chini ya uangalizi wa watalaam wa afya.
Halafu kuna wale ambao hawana virusi vya Corona lakini kimazingira nao ni kama vile wanaugua Corona lakini bila kuwa na virusi wala kuambukizwa. Unajua kwanini? Ngoja
nikwambie leo hii kuna mamia ya watu Duniani shughuli zao za utafutaji zimesimama.Hakuna kinachofanyika.
Kwa mfano kuna nchi ambazo wananchi wake wamekatazwa kabisa kutoka nje ya nyumba zao kuepuka maambukizi ya Corona. Watu wako ndani hawana pakwenda. Hawawezi kutoka nje kwasababu zimewekwa sheria kali. Kwa Tanzania tunashukuru Rais wetu Dk.Magufuli ametoa maelekezo kujiepusha na ugonjwa huo lakini akasema watu waachwe wafanye kazi.
Ninaposema wengi wanaugua Corona ( kwa maana sio ile ya virusi vya Corona) naangalia jinsi ambavyo watu wanashindwa kutafuta riziki kupitia kazi wanazozifanya kila siku.Nenda kwenye vibanda umiza hali imekuwa ngumu, walikuwa wanaishi kwa kuonesha mipira na maisha yakawa yanakwenda.Leo Ligi mbalimbali Duniani zimesimama.
Hata Ligi Kuu Tanzania Bara nayo imesimama. Wanaotegemea kuishi kwa vibanda umiza leo wanaona athari za ugonjwa huo ni kama vile nao wako karantini ya muda nakusubiria kuona hatma ya lini Corona itakwisha waendelee na maisha yao.
Ukitaka kujua wengi wanaugua Corona maana ya athari zake ni pale ambapo usafiri wa anga katika nchi mbalimbali umesimama,waliokuwa wanaishi kwa kutegemea usafiri huo leo hawana cha kufanya.Mamia ya watu wanahofia kupoteza ajira zao.Iko hivi hofu ya ugonjwa wa Corona wakati mwingine imekuwa kubwa kuliko Corona yenyewe.
Kuna watu ambao wao walikuwa wanaishi kwa kutegemea watalii,baada ya Corona shughuli za Utalii nazo zimepungua kutokana na nchi nyingi kuzuia mipaka yake ,hivyo waliokuwa kwenye eneo hilo nao wanakumbana na athari za Corona. Ni kama vile nao wanaugua Corona kwa upande wa nyuma.
Kwa hapa nyumbani nimeona baadhi ya hoteli kubwa zimetoa matangazo ya kufunga shughuli za hoteli zao kama hatua ya kukabiliana na ugonjwa wa Corona.Pata picha waliokuwa wakifanya kazi kwenye hoteli hizo wanafikiria nini kichwani.
Nchi nyingi za Afrika watu wamesimamisha shughuli zao. Na sio Afrika hata nchi za Ulaya nako ni hivyo hivyo na pengine hali ni mbaya kuliko Afrika.Rais wa Marekani amenukuliwa akisema kuwa uchumi wa Marekani unategemea watu kufanya kazi na sasa nyingi zimesimama, hivyo tayari ametoa maagizo kuwa, kuna umuhimu wa Marekani kuendelea kuchapa kazi.
Tuombe Mungu atuepushe na balaa hili la janga la Corona.Nafahamu kuna watu ambao maisha yao yanakwenda kutokana na mikusanyiko ya watu,leo hakuna mikusanyiko ,ndio !kwa mfano kuna watu maisha yao yanategemea kuwa MC kwenye makongamano na mikutano lakini hivi sasa hakuna mikutano wala makongamano.Hivyo kwa sehemu kubwa watu hao nao wanaathiriwa na Corona moja kwa moja ingawa sio kiafya bali kiuchumi.
Eti imefika wakati hata watu wanadaiwa wakikimbushwa kulipa deni utasikia wanajibu kirahisi kabisa kuna Corona .Kwa ujinga wangu kuna mambo ambayo nimejifunza tangu kuanza kwa ugonjwa wa COVID-19 unaosababishwa na virusi vya Corona.Kuna kundi ambalo limeamua kuendelea kuwa na mzaha na kundi ambalo limeamua kuuona ugonjwa huo ni hatari na wanachukua tahadhari kubwa.Ni wakati wa kutafakari uko upande gani? Nitoe rai bila kujali unaugua COVID-19 au unasumbuliwa na ugonjwa wa Corona, chukua tahadhari kadri unavyoweza.
Kwa anayetaka kutoa maoni yake niko tayari kupokea kwa namba hiyo hapo mwishoni kabisa. Hata hivyo haya maoni mimi nayapeleka wapi? Ni bora iwe namba kwa ajili ya kuwasiliana tu na wewe mtu wangu,mshkaji wangu, rafiki yangu, ndugu yangu,mtanzania mwenzangu, Mwafrika mwenzangu na kubwa zaidi ni mwanadamu mwenzangu .Hii hapa 0713833822.
APP YETU MPYA: Sasa unaweza kusoma kwa urahisi kupitia APP yetu. Download hapa kwa KUBOFYA HAPA
0 Comments