Charles James, Globu ya Jamii
KUTOKANA na mvua kali ambazo zinaendelea kunyeesha katika maeneo mbalimbali nchini, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe amewaagiza mameneja wote wa TANROADS nchini kuimarisha miundombinu ya barabara na madaraja kwenye maeneo yao.
Agizo hilo pia limeenda kwa Mamlaka za hali ya news nchini kuhakikisha wanatoa taarifa za hali ya hewa hususani za mvua mara kwa mara kwa wananchi.
Waziri Kamwelwe pia ametoa wito kwa wananchi wote kuchukua tahadhari ikiwemo kuendelea kuzingatia taarifa na tahadhari za hali ya hewa zinazotolewa na mamlaka zinazohusika sambamba na kufuata ushauri unaotolewa na wataalam katika sekta husika ili kupunguza athari zinazotokana na hali mbaya ya hewa.
Akitoa taarifa ya hali ya mwenendo wa mvua zinazoendelea kunyeesha nchini mbele ya wandishi wa habari jijini Dodoma, Waziri Kamwelwe amewataka viongozi wote waliopo chini ya wizara yake kuchukua hatua zote za tahadhari katika kipindi hiki.
" Kama alivyoelekeza Mhe Rais Dk John Magufuli kuwa meneja wa TANROADS ambaye barabara zake zitakatika naye atakua ameshajifuta kazi. Nasisitiza sitakua na mzaha katika utekelezaji wa maelekezo hayo ya Mhe Rais.
Nitoe maagizo kwa viongozi wote na taasisi zilizo chini ya wizara ninayoiongoza kuhakikisha wanachukua hatua zote za tahadhari ili kuhakikisha miundombinu wanayoisisimamia ipo salama kwa matumizi ya wananchi, " Amesema Mhandisi Kamwelwe.
Amesema tayari serikali ilishatoa fedha kwa wakala za barabara kwa kila Mkoa na hata februari mwaka huu mfuko wa barabara uliwapatia kiasi cha fedha ili ziweze kusaidia kutokana na mvua zinazonyeesha hivyo atamshangaa meneja yoyote wa TANROAD ambaye atashindwa kutekeleza wajibu wake.
Mhe Waziri amesema mwaka huu Nchi imepokea mvua nyingi zisizo za kawaida ambazo zilianza tangu Oktoba mwaka jana na kuungana na msimu wa masika na zitaendelea kunyeesha hadi Mei mwaka huu.
Amesema mvua hizo ni matokeo ya athari za mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi hali ambayo pia imesababisha kuwepo na ongezeko la joto la bahari juu ya watani Kusini Magharibi mwa bahari ya Hindi.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe akizungumza na wandishi wa habari ofisini kwake jijini Dodoma.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe akitoa taarifa ya hali ya mwenendo wa mvua zinazoendelea kunyeesha nchini mbele ya wandishi wa habari ofisini kwake jijini Dodoma.
APP YETU MPYA: Sasa unaweza kusoma kwa urahisi kupitia APP yetu. Download hapa kwa KUBOFYA HAPA
0 Comments