A to Z ya Mtu Aliyeanguka Stand ya Basi Mwanza na Kuzua Taaruki Kubwa....Alikuwa Hajala Siku Mbili | ZamotoHabari.



Mwanza. Shughuli za kupandisha na kushusha abiria pamoja na biashara nyingine, jana zilisimama kwa muda katika kituo kikuu cha mabasi eneo la Nyabulogoya/Nyegezi jijini Mwanza baada ya mtu mmoja kuanguka wakati akijieleza kwa askari katika kituo kidogo cha polisi.

Kwa mujibu wa mashuhuda, tukio hilo lililotokea saa 5:00 asubuhi wakati mwanaume wa makamo alipoanguka na kuzirai wakati akijieleza kwa polisi jinsi anavyoandamwa na kikohozi na mwili wake kukosa nguvu.

Maduka na shughuli mbalimbali kituoni hapo yalifungwa, huku wananchi wakionekana kuwa na taharuki.

Ingawa mkuu wa mkoa, John Mongella amesema hajapokea taarifa hizo, magari ya polisi pamoja na ya kubeba wagonjwa yalifika kituoni hapo na kumchukua mgonjwa huyo kumkimbiza hospitali.

“Sijapokea taarifa hizo. Kama kweli shughuli zote zimesitishwa hapo stendi ni jambo la taharuki tu. Siku hizi mtu hata akiwa na kikohozi na mafua ya kawaida, watu hukimbilia kusema ni corona,” alisema Mongella.

Mkuu huyo wa mkoa alisema kama kuna mtu mwenye tatizo la kiafya ameonekana na kuchukuliwa kutoka stendi, atakuwa amekimbizwa hospitali kwa uchunguzi na huduma za kiafya kubaini tatizo lake.

“Si kila mgonjwa anayekohoa au kuwa na tatizo la kupumua anapelekwa kituo cha kuhudumia waathirika wa virusi vya corona cha Buswelu. Hatua ya kwanza ni kumpeleka hospitali, kuhudumiwa na kuchukuliwa vipimo,” alisema Mongella.

Baadaye jioni Mongella aliieleza Mwananchi kuwa mtu huyo amelazwa Hospitali ya Wilaya ya Nyamagana Butimba kwa uchunguzi na vipimo zaidi.

“Taarifa za uchunguzi wa awali zimebaini kuwa aliingia Mwanza akitokea Singida. Maelezo yake yanakanganya. Mara anasema alikuwa anawatafuta ndugu zake, mara anamtafuta mke wake,” alisema.

“Licha ya kuonekana kama mtu mwenye msongo wa mawazo, pia imebainika hajala chakula kwa muda wa siku mbili. Lakini uchunguzi wa kitabibu ikiwemo vipimo vinafanyika kubaini tatizo lake.”

Serikali imekuwa ikisisitiza kuwa taarifa zote za wagonjwa wa virusi hivyo zitatolewa na viongozi watatu-- Waziri Mkuu, Waziri wa Afya na Msemaji Mkuu wa Serikali-- katika harakati za kuzuia taharuki inayoweza kusababishwa na utoaji taarifa.

Hadi sasa, Tanzania imetangaza kugundua wagonjwa 32 tangu mgonjwa wa kwanza alipogundulika Machi 16. Kati ya waliogundulika kuwa na maambukizi ya virusi hivyo, watatu wamefariki dunia huku watano wakipona na kuruhusiwa kuondoka.

Ugonjwa huo, uliogundulika nchini China mwishoni mwa mwaka jana, umeshaua zaidi ya watu 106,000 duniani na kuambukiza zaidi ya watu milioni 1.7 hadi jana jioni.

Tayari Serikali imefunga shule na vyuo, kuzuia shughuli za mikusanyiko isiyo na umuhimu kama warsha, semina, mikutano na shughuli za michezo.

Pia imeweka sharti kwa watu wote wanaoingia kutoka nchi zenye maambukizi, kukaa karantini kwa siku 14 kwa gharama zao.




APP YETU MPYA: Sasa unaweza kusoma kwa urahisi kupitia APP yetu. Download hapa kwa KUBOFYA HAPA

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini