Awamu ya Tano Yafanikisha Ndoto ya Wananchi Uyui | ZamotoHabari.

Na Frank Mvungi- MAELEZO.

Serikali ya Awamu ya Tano imetimiza ndoto ya wananchi wa Wilaya ya Uyui, mkoani Tabora kufikiwa na huduma bora za afya katika maeneo yao.

Akizungumza katika mahojiano maalum wilayani humo, Mkuu wa Wilaya, Gift Msuya amesema kuwa kwa sasa wananchi wa wilaya hiyo wanafikiwa na huduma za afya kupitia vituo vya afya vilivyojengwa na vile vilivyoboreshwa katika kipindi cha miaka mine iliyopita.

“ Tumekamilisha ujenzi wa Hospitali ya Wilaya iliyogharimu Shilingi bilioni 1.5 na iko tayari kuanza kutoa huduma baada ya kuwasili kwa vifaa, hili linaenda sambamba na utoaji wa huduma katika vituo vyetu vya afya ambavyo vinatoa huduma zinazoendana na mahitaji ya wananchi,” alisisitiza Msuya

Aidha, Msuya amesema kuwa Serikali ilitoa milioni 500 zilizowezesha kuboreshwa kwa Kituo cha Afya Upuge na pia shilingi milioni 400 zimetumika katika ujenzi wa Kituo cha Afya Igalula.

Kuwepo kwa huduma bora na vifaa vya kisasa kumewezesha Wilaya ya Uyui kutokuwa na vifo vya akinamama wanaopatwa na uchungu pingamizi kwa kuwa sasa huduma ya upasuaji inapatikana karibu na walipo wananchi tofauti na ilivyokuwa awali.

Naye Kaimu Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Upuge, Sr. Dkt. Yustina Raphael amesema kuwa tangu kuanza kwa huduma ya upasuaji kwa akinamama zaidi ya akinamama 100 wamefanyiwa upasuaji kwa ufanisi.

“Jukumu letu ni kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi kupitia kituo hiki cha Upuge kwa kuwa kimeboreshwa na kina vifaa vya kisasa vya kutolea huduma ikiwemo vya maabara na vya kufanyia upasuaji,” alisisitiza Sr. Dkt. Yustina

Awali, kabla ya maboresho ya kituo hiki kilichoanza mwaka 1977 kilikuwa na huduma chache na kwa sasa kimeongeza huduma kama za maabara, upasuaji, mama na mtoto na pia watumishi wameongezwa ili kuendana na mahitaji.

Akizungumzia kuhusu rufaa katika Kituo hicho, Sr. Dkt. Yustina amesema kuwa baada ya maboresho rufaa za wagonjwa zimepungua kwa kiwango kikubwa na hivyo kuwapunguzia wananchi adha ya kutembea umbali mrefu au kusafiri kufuata huduma za afya.

Kwa upande wake mmoja wa wagonjwa waliofika kupata huduma katika kituo hicho, Bi. Salma Ramadhani aliwapongeza watoa huduma wa kituo cha afya Upuge kwa utendaji bora na wenye tija kwa wananchi wote wanaofika kupata huduma kituoni hapo.

“Tunamshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kuboresha sekta ya afya hasa vituo vyetu vya afya kama hiki cha Upuge kwa sasa tunapata huduma za upasuaji hapa na wahudumu wa hapa wakiwemo madaktari wanatuhudumia vizuri na mazingira yameboreshwa kupitia majengo mapya na vifaa vya kisasa kabisa”, alisisitiza Salma.

Akifafanua amesema kuwa amefanikiwa kujifungua salama kutokana na huduma bora zilizopo katika kituo hicho hali inayowafanya akinamama kuondokana na adha ya kusafiri umbali mrefu kufuata huduma hizo.

Serikali ya Awamu ya Tano imefanikiwa katika kuimarisha huduma za afya ikiwemo ujenzi wa vituo vya afya, hospitali za wilaya, zahanati, ujenzi wa hosptali za rufaa za Mikoa na Kanda na pia upatikanaji wa dawa na vifaa tiba imekuwa chachu ya kuboreshwa kwa huduma katika wilaya na mikoa yote hapa nchini. 

Muonekano wa Jengo la utawala katika Hospitali ya  Wilaya ya Uyui  Mkoani Tabora baada ya ujenzi wa Hospitali hiyo kukamilka tayari kwa kuanza kutoa huduma, ujenzi wa Hospitali hiyo umegharimu shilingi Bilioni 1.5 hadi kukamilika

Sehemu ya majengo ya Hospitali ya Wilaya ya Uyui  Mkoani Tabora baada ya ujenzi wa Hospitali hiyo kukamilka tayari kwa kuanza kutoa huduma, ujenzi wa Hospitali hiyo umegharimu shilingi Bilioni 1.5 hadi kukamilika.


 Muonekano wa Chumba cha Upasuaji katika kituo cha Afya Upuge Wilayani Uyui baada ya kuboreshwa kwa gharama ya shilingi milioni 500 zilizotumika kujenga majengo mapya yaliyowezesha huduma kuboreshwa ikiwemo kuanza kwa huduma za upasuaji.
 Sehemu ya majengo mapya ya Kituo cha Afya Upuge Wilayani Uyui Mkoani Tabora kama yanavyoonekana  baada  kuboreshwa kwa gharama ya shilingi milioni 500 zilizotumika kujenga majengo mapya yaliyowezesha huduma kuboreshwa ikiwemo kuanza kwa huduma za upasuaji.               (Picha zote na Aboubakari Kafumba)



APP YETU MPYA: Sasa unaweza kusoma kwa urahisi kupitia APP yetu. Download hapa kwa KUBOFYA HAPA

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini