· Suluhisho pia kutolewa kwa Wateja Wakubwa
Benki ya NMB Plc leo imetangaza unafuu wa ulipaji mikopo kwa Wateja wa Biashara ndogo na za kati (SME/MSME) na wakubwa ili kuwasaidia kukabiliana na madhara yaliyotokana na janga la COVID - 19 kwenye biashara zao. Hii ni jitihada ya benki katika kutoa ahueni kwa wateja wake hususani sekta zilizoathiriwa zaidi na janga la COVID-19.
Takribani wateja 412 biashara ndogo na za kati wameshapata ahueni hii kwa kupitia likizo ya marejesho ya mikopo yao na wengine wakiongezewa muda wa kulipa mikopo hiyo ili kuwasaidia kukabiliana na madhara yaliyoletwa na COVID – 19 katika biashara zao.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa NMB , Ruth Zaipuna alisema athari ambazo zimetokana na janga la COVID-19 kwa watu wa kawaida na wafanya biashara zimekuwa si kubwa sana ukilinganisha na nchi ambazo zilifunga shughuli zote na watu kujifungia ndani, hata hivyo, uamuzi wa nchi nyingine kujifungia umeleta mtikisiko katika biashara duniani na hivyo kuathiri baadhi ya wateja wetu wa hapa nchini.
"Kama Benki, tunatambua kuwa huu ni wakati mgumu kwa wateja wetu ambao biashara zao zimeathirika kutokana na mtikisiko huu kutoka nje, tumedhamiria kutoa ahueni kutokana na mahitaji ya wateja na ukubwa wa athari, hii ni kwa sababu si biashara zote na wateja wote wameathirika kwa kiwango sawa, mkazo ni katika biashara zilizoathirika zaidi na COVID-19," aliongeza.
"Tunapenda kuwahakikishia wateja wetu kuwa hawako peke yao kwenye safari hii. Milango yetu ipo wazi na tupo tayari kuwasaidia katika nyakati hizi zisizo na uhakika za janga la COVID-19. Mara zote lengo letu ni kuhakikisha ukuaji wa uchumi wa nchi yetu. Njia pekee tunayoweza kufanya hilo ni kuhakikisha kuwa ukuaji wa wateja wetu ni endelevu, hivyo umuhimu wa kuwapunguzia mzigo huu katika kipindi hiki”
“ Pamoja na ahueni hii ya kifedha, pia tutatoa mafunzo ya kibiashara na nasaha mbalimbali za uwekezaji na usimamizi wa fedha kwa njia za kiilektroniki kwa kutumia wataalamu wa ndani." Alisema Bi. Zaipuna
Benki ya NMB pia imeimarisha njia mbadala za kidijitali ili kuhakikisha kuwa mteja anafanya miamala kwa usalama mahali alipo, njia hizi ni kama NMB Mkononi na miamala ya mtandao wa kompyuta inayotoa fursa ya kufanya miamala bila kufika tawini.
Hatua hizo ni ushuhuda wa kujitoa kwetu kupata suluhisho halisi, linalowalenga wateja, katika kipindi hiki kisicho na uhakika, "alisema Zaipuna.
“Tunawasihi wateja wetu ambao wana uwezo wa kuendelea kufanya malipo yao, wafanye hivyo. Hii itatuwezesha kupanua wigo kwa wengine wengi ambao hawako katika nafasi sawa," alisema.
APP YETU MPYA: Sasa unaweza kusoma kwa urahisi kupitia APP yetu. Download hapa kwa KUBOFYA HAPA
0 Comments