CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimewataka wabunge wenye ushahidi juu ya tuhuma za matumizi mabaya ya fedha, kuuweka hadharani.
Kauli hiyo ya Chadema imetolewa jana Jumamosi tarehe 23 Mei 2020, na Benson Kigaila, Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Bara, kufuatia wimbi la wabunge waliotangaza kukihama chama hicho, kudai kwamba Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema anatumia vibaya fedha za chama hicho.
“Waambie walete huo ushahidi kwa sababu anayetoa tuhuma anatakiwa alete ushahidi, kama zimekopwa walete ushahidi. Kuna yeyote ameshatoa ushahidi kama zimekopwa?” amehoji Kigaila.
Juzi Ijumaa tarehe 22 Mei 2020, Susan Maselle na Joyce Sokombi , Wabunge Viti Maalumu wa Chadema, walipotangaza adhima ya kukihama chama hicho na kujiunga na NCCR- Mageuzi mara baada ya Bunge la 11 kuvunjwa walitoa shutuma kadhaa ikiwamo unyanyasaji wa kingono.
Pia, walidai hakuna mtu anayeruhusiwa kuhoji juu ya matumizi ya fedha za Chadema.
Tuhuma hizo pia ziliwahi kutolewa bungeni na Spika Job Ndugai, hivi karibuni, ambaye alimtuhumu Mbowe kuwa anawalazimisha wabunge kuchangia fedha hizo.
Ndugai alidai kwamba, kuna wabunge kadhaa wa Chadema walifikisha malalamiko yao katika ofisi yake, ya kwamba wanalazimishwa kutoa sehemu za posho yao, kwa ajili ya kuchangia shughuli za chama hicho.
Kuhusu matumizi ya fedha za Chadema kutowekwa hadharani, Kigaila amesema tuhuma hizo sio za kweli, kwa kuwa bajeti ya matumizi ya chama hicho inapangwa na vikao husika, kisha kupitishwa na baraza lake kuu.
Kigaila amesema baada ya fedha za Chadema kutumika, Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), hukagua taarifa za matumizi hayo.
“Pesa wanazochanga wabunge, madiwani na wanachama wakishachanga zinakuwa za chama haziwi za wabunge, chama kinapanga matumizi ya fedha zozote iwe ruzuku, michango ya wanachama, watu binafsi na wadau wengine, ” ameeleza Kigaila
“Chama kinapanga matumizi kwa kutumia vikao vya chama, bajeti ya chama inapitishwa na baraza kuu kisha matumizi yanaidhinishwa kwa wakati. Na taarifa zinatolewa na kamati kuu, si wabunge wanakaa na kupanga matumizi.”
Wakati huo huo, Kigaila amesema katiba ya Chadema inaelekeza wabunge kuchangia fedha, kwa ajili ya kuendesha shughuli zake.
“Hakuna makubaliano kati ya chama na wabunge isipokuwa kwa kanuni ya chama, wao walichangia kwa mujibu wa kanuni ya chama kama wengine walivyochangia toka mwaka 2006. Hatukai na wabunge tukakubaliana hizi hela zinatumikaje, ni chama kinapanga zinatumikaje, zikishatumika CAG anakuja kukagua, ” amesema Kigaila.
Kigaila ameongeza kuwa “Katiba ya chama hicho imeeleza namna wabunge wanavyotakiwa kuchangia chama, kwamba wabunge wa majimbo watachangia asilimia 10 ya posho, na viti malaumu watachangia asilimia 30 ya posho zao.”
Amesema wanaolalamika kuchangishwa fedha kinyume na sheria, ni uzembe wao wa kutosoma katiba ya chama kilichowadhamini kupata ubunge.
“Mbunge yeyote wa Chadema anakuwa na katiba kabla hajagombea, anateuliwa hadi anashinda, anajua akiwa mbunge atachangia hivyo, hakuna makubaliano chama kinakaa na wabunge wanasema watachangia,” amesema Kigaila
“Hao wanalalamika huenda katiba inaandikwa wakati hawakuwa Chadema, lakini ukiingia Chadema inatakiwa usome kanuni, kama hujasoma hilo ni tatizo lako binafsi.”
OPEN IN BROWSER
APP YETU MPYA: Sasa unaweza kusoma kwa urahisi kupitia APP yetu. Download hapa kwa KUBOFYA HAPA
0 Comments