WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe amesema ndege ya kwanza iliyobeba watalii ikitokea Ugiriki imetua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) wilayani Hai jana.
Aidha, Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) inakamilisha taratibu za kuanza kubeba na kupeleka mizigo Ulaya kwa ajili ya biashara.
Akizungumza jana na waandishi wa habari jana jijini hapa, Kamwelwe alisema ndege iliyobeba watu saba wakiwemo watalii wanne kutoka Ugiriki, ilitua KIA jana saa 3:30 asubuhi, ikiwa ni siku chache baada ya serikali kutangaza kufungua anga lake, lililokuwa limefungwa kutokana na maambukizi ya virusi vya corona.
Hii ni hatua ya mwanzo ya kurejea kwa usafiri wa anga kwa ndege za kimataifa nchini, ikiwa ni zaidi ya mwezi mmoja tangu anga la Tanzania lifungwe.
“Ndege iliyotua ilikuwa na watalii wanne na crew ya watu watatu na wametua tayari wamepokelewa na wameenda kuangalia wanyama,” alieleza Kamwelwe.
Aliongeza kuwa tayari kuna ratiba ya ndege, zitakazofanya safari zake kuja Tanzania na nafasi zimejaa. Alisisitiza kuwa ifikapo Mei, 28 mwaka huu ndege nyingi zaidi zitatua.
“Yapo mashirika ya ndege yalishajiandaa kama Emirates, Ethiopian na KLM. Kwa upande wa ndege za mizigo tulianza na Rwanda Airline kuanza kubeba minofu ya samaki, leo (jana) tumeongeza ndege nyingine Ethiopian Airlines ambayo itabeba tani 19 za minofu ya samaki,” alieleza.
Alisema pia Jumapili hii Ethiopian Airlines, itarudi tena jijini Mwanza kubeba tani 40 ya minofu ya samaki.
“Uwanja wa Mwanza umefunguka na kwa kuwa ni uwanja wa kimataifa, ndege zitaruka kimataifa kwa ajili ya kubeba mizigo na tunaendelea kuongea na Waziri wa Mifugo na Uvuvi ili nyama ianze kusafirishwa,” alisema waziri huyo mwenye dhamana ya Uchukuzi.
APP YETU MPYA: Sasa unaweza kusoma kwa urahisi kupitia APP yetu. Download hapa kwa KUBOFYA HAPA
0 Comments