Ukistaajabu ya Kukonda ya Wema Sepetu, Basi Bado Hujaona ya Mwanamuziki Celine Dion..Dunia Yote Yamshangaa | ZamotoHabari.


Ukistaajabu ya Kukonda ya Wema Sepetu, Basi Bado Hujaona ya Mwanamuziki Celine Dion..Dunia Yote Yamshangaa

UKIKUTANA na staa wa sinema za Kibongo, Wema Isaac Sepetu, bado utakuwa unajiuliza ni nini kilimpata. Kutoka kwenye lile umbo lake matata la kuvunja chaga lililowavunja shingo wanaume hadi kuwa kimbaumbau!



Wakati ukistaajabu ya Wema kukondeana na kupungua uzito kutoka kilo 96 hadi 70 na sasa chini ya hapo, utaona ya staa wa dunia wa muziki wa Blues, Celine Dion.

Kwa wahenga wenzangu, bado nyimbo za Celine zimewakaa kichwani. Kuanzia Because You Love Me, My Heart Will Go On, That’s The Way It Is, I am Your Angel, A New Day Has Come, I am Alive, The Power Of Love hadi It’s All Coming Back To Me na nyinginezo nyingi.



Basi, taarifa ikufikie kuwa, simulizi ya kukondeana kwa Celine kiasi cha kuonekana kama mdoli wa kuning’iniza nguo madukani, inaendelea huku kila shabiki akijiuliza; “Celine anaumwa?”

Celine mwenye maskani yake pale Las Vegas, Marekani, alianza kukongoroka mdogomdogo mara tu baada ya kufiwa na mumewe kipenzi, Rene Angelil, mwaka 2016.



Mwanamama huyo mwenye umri wa miaka 52, ameendelea kustaajabisha ulimwengu katika kipindi cha miaka minne. Celine ameendelea kupungua siku hadi siku kiasi cha kuzua hofu juu ya afya yake.

Kama ilivyo kwa Wema, naye ameendelea kusisitiza; “Nipo vizuri, najisikia vizuri sasa kuliko wakati mwingine wowote!”



Mwenyewe anasema amekuwa akishuhudia mjadala mkali juu ya afya yake kwa takriban miaka minne sasa.

Hata hivyo, pamoja na kutengeneza vichwa vingi vya habari za burudani ndani na nje ya Marekani, hakuna aliyewahi kutaja kiasi kamili cha uzito aliopoteza kwa maana ya kilo.



Je, Celine alifanyaje hadi akapungua uzito na kukongoroka kiasi hicho? Hili ndilo swali lililomfanya mwandishi wa Gazeti la The Sun, Dan Wootton ambaye alimvaa na kumtaka kusema ni nini hasa kilitokea mara tu baada ya kifo cha mumewe?

Katika majibu yake kwa mwandishi huyo, Celine anasema;

“Nimefanya hivi kwa ajili yangu. Nataka kujisikia imara, nisipoteze uzuri wangu, niendelee kuwa na mvuto.”



Kuhusu mwili wake kuonekana skeletoni na kustaajabisha mashabiki wake ambao sasa wanaogopa hadi kumuona na kupiga naye picha, Celine anajibu;

“Kama mimi napenda kuwa hivi, siumizi kichwa sana na sipendi kulizungumzia.



“Wasijali sana, wasipige picha na mimi. Kama mtu ananipenda jinsi nilivyo, nipo kwa ajili yake. Kama mtu hapendi aniache na mwili wangu.”

Celine anaendelea kusema kuwa, amekuwa akifanya mazoezi ya kucheza muziki na kupata mafunzo ya kuhimili steji akiwa na rafiki na mbunifu wake, Pepe Munoz.



Katika picha yake ya mwisho kule Paris, Ufaransa mwezi Januari mwaka huu, Celine aliwaambia waandishi wa habari;

“Nina furaha sasa na uimara wa mwili wangu kuliko wakati mwingine wowote.”

Celine anakataa katakata kuwa hana tatizo lolote la kiafya na si kweli kwamba ana msongo au kushindwa kula kutokana na kumpoteza mumewe.



Anasema; “Sina utapiamlo, watu wanastaajabu kwa nini nimekonda na sifanyi juhudi za kunenepa.

“Nashangaa kwa nini mjadala huu sasa, nimekuwa mwembamba maisha yangu yote. Katika familia yetu hakuna mtu mnene.”

Celine anasema amejitolea maisha yake yote kuwa mtumbuizaji, ili kutimiza hilo, hawezi kuwa mnene.

Anaongeza; “Kutumbuiza ni jambo lililopo ndani ya vinasaba vyangu (DNA) katika maisha yangu yote. Natimiza ndoto yangu hapa duniani!



“Nafanya mazoezi mara nne kwa wiki. Watu wanasema nimekuwa mwembamba sana, lakini hawajui ni kwa kiasi gani ninajituma kuwa hivi nilivyo!”

Pamoja na utetezi wake huo, maelfu ya mashabiki wake duniani kote, wameendelea kumlaumu kila anapoweka picha kwenye ukurasa wake wa Instagram juu ya kukondeana huko.

Sehemu ya maoni hayo yanasomeka;

“Celine sasa unatisha, umekauka sana.”

“Celine umekondeana sana, ngozi imekakamaa.”

“Celine tangu nimeanza kukuona na kuwa shabiki wako, sijawahi kukuona hivi, unatisha!”

Makala: Sifael Paul

APP YETU MPYA: Sasa unaweza kusoma kwa urahisi kupitia APP yetu. Download hapa kwa KUBOFYA HAPA

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini