Dawa Ilivyomnasa Mwizi Zanzibar Akapitiwa Usingizini Fofofo! | ZamotoHabari.



KIPORO cha habari ya mwizi kusinzia wakati akiiba nyumbani kwa mwandishi Farouk Karim huko Visiwani Zanzibar hivi karibuni hakijachacha, Amani lina ishu nzima.

Chanzo kilimwambia mwandishi wetu kuwa, tangu tukio hilo litokee Juni 2, mwaka huu, watu mbalimbali wengine vigogo, wamekuwa wakifika nyumbani kwa mwandishi huyo wakitaka dawa ya kunasa wezi.


“Yaani watu ni wengi mno, wanafika kwa huyo mwandishi, magari yanapishana na wengine wanasafiri kutoka mikoani.“Hilo tukio la mwizi kunasa wakati akiiba limetikisa sana, mimi sisemi mengi lakini mtafute Farouk atakuambia mengi,” chanzo ambacho kilidai kiko karibu na makazi ya mwandishi huyo kilisema.

MAZUNGUMZO YA AMANI NA FAROUK, HAYA HAPA

Amani: Salama kaka?

Farouk: Salama, habari za siku?

Amani: Njema, unajificha wakati mimi wezi wa matikiti wananisumbua shambani.

Farouk: Hahahaa; nashangaa, ninyi kwenye hicho chombo chenu hamkuja, wengine wamekuja.

Amani: Hebu niambie baada ya stori ya mwizi kulala nyumbani kwako baada ya kuiba, kuna usumbufu umepata kwa watu kutaka dawa ya wezi?

Farouk: Nimepata, tena usumbufu mkubwa mno na hivi ninavyokuambia, mpaka sasa nasumbuliwa.

Amani: Kwa hiyo watu wanafika hapo kwako kutaka dawa hiyo ya kunasa wezi?


Farouk: Yaani nakwambia dah… watu wengi wanakuja, wengine si watu wadogo, ni wazito kabisa nikikutajia majina wala huwezi kuamini, lakini wanakuja kutaka dawa ya wezi.

Amani: Kwa hiyo mambo yanakunyookea Farouk?

Farouk: Yaninyookee wapi bwana, watu wazito wanakuja wananiambia nina kitu nao niwape, sasa inakuwa balaa tupu.

Amani: Hahahaa…lakini si ulijitangaza kwamba una kitu na watu wakitaka wakuone?

Farouk: Aaa, aaah… sijajitangaza hivyo, mimi nilisema ni kuomba dua tu, sasa wengine wanataka niwape kitu fulani, hicho mimi sina.

Amani: Kwa hiyo umekuwa ukifanyaje?

Farouk: Yaani ni shida kweli, ukiwaambia watu kwamba hiyo ni dua ambayo kila mtu anaweza kuomba kivyake hawaamini, wanasema No kuna kitu ninacho siyo bure.

Amani: Pole sana.

Farouk: Hivi ninavyokuambia hadi hii leo kuna mtu kanipigia simu kutoka mkoani anataka hiyo dawa. Jana kuna mama kafika nyumbani kwangu usiku anasema nimpatie hiyo dawa.

Amani: Nasikia kuna watu wengine wanatoka mikoani wanakufuata Zanzibar.

Farouk: Napata simu kutoka kila kona ya nchi hii, yaani kama ni umaarufu umezidi mara dufu, ingawa mimi kwa hapa Zanzibar ni maarufu tangia hapo mwanzo.

Amani: Wengi wanataka dawa ya wezi tu au na nyingine za mambo yao maana huu ni mwaka wa uchaguzi pia.

Farouk: Hahaha; mambo ni mazito, naanza kuhisi kuna watu wamedaka hili suala na wanalikuza ili wapate fedha, maana limekuwa jambo kubwa sana.

Amani: Huyu jamaa ambaye alinasa wakati akiiba, kwako umemalizana naye vipi?

Farouk: Mimi niliachana naye, lakini bado ana kesi polisi kwa sababu kuna watu wengine walijitokeza kudai kuwa aliwahi kuwaibia.

Amani: Ok!

Farouk: Asante ndugu lakini kiukweli imeni-distabu sana hii, maana kila nikipita watu wanaoneshana na wengine wananifuata wanasema tupe dawa, basi tabu kweli.


TUJIKUMBUSHE

Juni 2, mwaka huu kijana mmoja aliingia nyumbani kwa mwandishi Farouk usiku wa manane kwa madai ya wizi wa vitu mbalimbali na kwamba alipofungua mlango wa gari kutaka kuiba power window, alijikuta akipitiwa na usingizi hadi asubuhi ambapo alinaswa kirahisi.


Hata hivyo, baada ya mwandishi huyo kuhojiwa sababu za mtuhumiwa huyo kulala wakati akiiba alisema; yote hayo yametokana na dua alizoomba jambo ambalo wengi hawakuliamini na kudai huwenda Farouk ana dawa za kichawi za kunasa wezi jambo ambalo limemletea usumbufu

APP YETU MPYA: Sasa unaweza kusoma kwa urahisi kupitia APP yetu. Download hapa kwa KUBOFYA HAPA

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini