KAMATI YA AMANI YALAANI VITENDO VYA UKATILI DHIDI YA WATOTO | ZamotoHabari.

Mjumbe wa Kamati ya Amani ya Mkoa Shinyanga Bw. Khalfan Ally akiwa amebeba mtoto mchanga wakati wa kamati hiyo ilipotembelea Kituo cha Afya Tinde kwa lengo la kujionea miradi ya Afya na Uwekezaji Wilaya ya Shinyanga.


Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Bi.Jasinta Mboneko akifafanua jambo kwa Kamati ya Amani ya Mkoa wa Shinyanga ilipotembelea Kituo cha Afya Tinde kwa lengo la kujionea miradi ya Afya na Uwekezaji Wilaya ya Shinyanga.



Wajumbe wa Kamati ya Amani ya Mkoa wa Shinyanga wakiangalia namna mafundi wa mradi wa SHUWASA wanavyounganisha mabomba walipotembelea miradi ya maji inayoendelea katika Manispaa ya Shinyanga.



Wajumbe wa Kamati ya Amani ya Mkoa wa Shinyanga ikiongozwa na Shekhe Balulisa pamoja na Mkuu wa Wilaya Ya Shinyanga Bi. Jasinta Mboneko wakiangalia namna mchakato wa wa matayarisho ya uchinjaji nyama unavyofanyika mapema jana katika machinjio ya kisasa yaliyo mbioni kufunguliwa nje kidogo ya Manispaa ya Shinyanga.

……………………………………………………………………….

Na Mwandishi wetu Shinyanga

Mwenyekiti wa Kamati ya Amani ya Mkoa wa Shinyanga Shekhe Balilusa Khamis amekemea tabia ya baadhi ya vijana wakike wanaotupa watoto baada ya kujifungua au kutoa mimba na kuonya kuwa kuzaa watoto ni agizo la Mwenyezi Mungu nakwamba kuna baadhi ya watu hawakujaliwa kupata mtoto.

Shekhe Khamis amesema hayo leo alipotembelea Kituo cha Afya Tinde wakati wa ziara ya Kamati ya Amani ya Mkoa wa Shinyanga iliyofanya ziara yake katika Wilaya ya Shinyanga kujionea miradi mbalimbali inayoendelea kutekelezwa katika Wilaya hiyo.

Shekhe Khamis amepongeza juhudi za Maendeleo zinazofanyika katika Wilaya hiyo na kupongeza viongozi wa Wilaya hiyo kwa kuokoa maisha ya mama na mtoto kwani imebainika kuwa tangu kukamilika kwa kituo hicho cha Afya akina mama wengi wamejitokeza kituoni hapo kwa ajili ya kujifungua na hakuna kifo hata kimoja cha mama na mtoto.

Aidha Shekhe Khamis ameongeza kuwa kama akina mama wangekataa kuzaa watoto kuna uwezekano mkubwa baadhi ya watu maarufu tunaowaona wasingekuwepo akijitolea mfano yeye mwenyewe katika familia yake ni wa tano kwa kuzaliwa kati ya watoto tisa wa familia yake akiongeza kuwa kama kwao wangezaliwa wawili bila shaka hata yeye asingekuwepo.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Bi. Jasinta Mboneko amesema kuwa vitendo vya kujifungua na kutupa watoto ni vitendo vya ukatili dhidi ya watoto na kuwataka watu wenye tabia kuliko kuwatupa watoto wawelete katika vituo vya Afya ambapo watakuwa salama.

Bi. Mboneko akiongea mbele ya Kamati ya Amani ya Mkoa wa Shinyanga amesema serikali Wilayani humo imeendelea kujenga vituo vya Afya na hospitali zenye kutoa huduma ya mama na mtoto kwa lengo kuokoa maisha ya mama na mtoto na kusikitishwa na baadhi ya watu ambao wanashindwa kuvumilia na kuamua kutupa watoto.

Kamati ya Amani ya Mkoa wa Shinyanga pamoja na mambo mengine imekagua na kujionea mradi wa maji pamoja na barabara za Manispaa ya Shinyanga zenye thamani Tsh. Bilioni 15 na kukagua maendeleo ya mradi wa machanjio ya kisasa ulioko nje kidogo ya Manispaa ya Shinyanga.

Wakati huo huo Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga Bw. Geofrey Mwangulumbi ameimbia Kamati ya Amani ya Mkoa wa Shinyanga kuwa mradi wa machinjio ya kisasa ni mradi wa kimkakati na tayari kuna baadhi ya wafanyabiashara wameonesha nia ya kufanyabiashara na mradi huo kwa lengo la kusafirisha nyama nje ya Nchi.

Kamati ya Amani ya Mkoa wa Shinyanga inayoongozwa na viongozi wa dini kutoka Mkoa wa Shinyanga inaendelea na ziara ya siku tatu katika Wilaya za Mkoa wa Shinyanga kujionea baadhi ya miradi ya Afya na Uwekezaji na inaendelea na ziara kama hiyo Makao Makuu ya Wilaya ya Shinyanga.


APP YETU MPYA: Sasa unaweza kusoma kwa urahisi kupitia APP yetu. Download hapa kwa KUBOFYA HAPA

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini