Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli amewataka viongozi anaowateua kuwa na uvumilivu na kuridhika, akimtolea mfano Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Dkt. Selemani Serera aliyevumilia mshahara mdogo akikitumikia Chama Cha Mapinduzi.
Akizungumza leo Julai 16, 2020 Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma, katika hafla ya kuwaapisha wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya na makatibu tawala, Rais Magufuli amesema kuwa kijana huyo ambaye amezaliwa miaka ya 1980, ingawa alikuwa msomi mwenye shahada ya uzamivu (PhD) alikuwa akilipwa mshahara wa Shilingi 500,000 tu, lakini alivumilia na kuendelea kuchapa kazi.
“Kwenye hizi kazi kuridhika ni kitu kikubwa sana, yule kijana pale anaitwa Selemani ni PhD holder lakini mshahara wake ulikuwa Sh. 500,000, alikuwa pale Makao Makuu ya CCM, lakini aliridhika na mshahara wake. Ilipojitokeza fursa ndio tukamteua kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kongwa,” amesema Rais Magufuli.
“Alisoma degree, akasoma Masters yake na akasoma PhD kwa miaka minne nchini China,” alisema Rais Magufuli na kuongeza kuwa kuna vijana wasioridhika hasa waliozamiliwa miaka ya 1982, lakini anaamini Dkt. Serera ataenda kuifanya kazi hiyo vizuri.
Amewataka wateule hao walioapishwa leo kuzingatia viapo vyao na kufanya kazi kwa bidii kuwatumikia wananchi kama walivyopaswa kuifanya katika maeneo yao.
Katika hatua nyingine, Rais Magufuli amesema kuwa kwa wale ambao wameamua kwenda kuchukua fomu ya kugombea nafasi ya ubunge, hakuna hata mmoja ambaye yeye amemtuma, na kwamba hata Makamu wa Rais na Waziri Mkuu nao hawajawatuma watu wakagombee.
APP YETU MPYA: Sasa unaweza kusoma kwa urahisi kupitia APP yetu. Download hapa kwa KUBOFYA HAPA
0 Comments