Chillah ni mmoja wa wasanii wenye vipaji vikubwa hasa katika suala la sauti na utunzi, alikuwa anakuwa vizuri kisanii lakini hapo kati anajua mwenyewe alichokifanya kikamfanya apotee kwenye ‘game’, kwa sasa anapambana kurejea lakini bado inaonekana ana mtihani mkubwa mbele yake.
Mtihani huo unatokana na sababu kadhaa ikiwemo yeye mwenyewe kusababisha mvuto wake kisanii kupotea na changamoto ya vijana wapya kwenye muziki, licha ya kuwa bado ana kipaji cha hali ya juu lakini huyo pekee haiwezi kumfanya kurejesha heshima kama aliyokuwa nayo miaka ya nyuma.
Pamoja na lawama nyingine kadhaa lakini ukweli ni kuwa kwa asilimia kubwa Chillah ni mfano mzuri wa wasanii wengi wenye vipaji vya ukweli vya kuimba ambao wamechangia kujipoteza wao wenyewe au wamejiwekea vizingiti vya kushindwa kupiga hatua kubwa kimafanikio.
Najua siyo lazima wasanii wote wawe kama Diamond Platnumz kimafanikio lakini kuna levo fulani ambayo mtu unamuona fulani anastahili kuwa sehemu fulani kisha anakuwa hayupo hapo unapoona anastahili.
Watu wengi wa aina hiyo wakishaanza kupotea aku wakipata wakati mgumu wanaanza kutoa lawama, fulani na fulani ndiyo waliosababisha wakafeli kimuziki wakati wanasahau kuwa muziki ni kama vita.
Kiuhalisia muziki ni vita kama ambavyo maisha ya kawaida yalivyo ni vita, bila kupambana utaishia kuwa mtu wa lawama kila siku.
Kwenye maisha usipoamka na kupigana ni rahisi kupoteza mwelekeo na mwisho wake ni kuanza kulaumu fulani ananibania au kanikwamisha. Pambana ili kizazi chako kije kikusifie kuwa ulipigana kwa ajili yao.
Bila kuzunguka sana Richi Mavoko ni bonge moja la msanii ambaye kama utafatilia miaka kadhaa ya nyuma alikuwa akifananishwa na levo za kina Diamond na Ali Kiba, hata kama alikuwa hajafikia ubora wa juu kimafanikio lakini kipaji chake kilikuwa wazi na kilionekana.
Mavoko alikuwa akitoa video kali, nyimbo kali na hata kwenye jukwaa alijua kazi yake vizuri.7
Ninaposema Richard Martin au Mavoko anajua kuimba ninamaanisha, ndiyo maana hajawahi kuharibu ‘chorus’ hata moja ambayo ameshirikishwa.
Aliposainiwa na WBC wengi wakaona kama anajimaliza kwa kuwa bosi wake anakuwa ni yule ambaye alikuwa akifananishwa naye, bahati mbaya mambo hayakwenda kama alivyotarajia.
Kipindi anasainiwa WCB niliamini halikuwa jambo sahihi, bali mtazamo wangu niliamini alitakiwa kutafuta timu sahihi nyuma yake imuongoze katika tifina na mipango yote ya muziki, levo aliyokuwa nayo haikuwa ya kusainiwa na WCB ambapo wengi wao kimuziki ni kama alikuwa amewazidi au wapo levo naye moja.
Lakini kusaini kwake WCB haikuwa kosa sana kwa kuwa kwenye maisha kuna njia nyingi za kutokea. Sasa baada ya kuondoka hapo, inaonekana kuna sababu za kimkataba zimembana ikiwemo kutumia akaunti ya YouTube aliyokuwa akiitumia na vitu vingine kadhaa.
Akafungua akaunti mpya ya YouTube alitoa nyimbo kadhaa ambazo nazo hazijafika mbali, ghafla amepotea kusikojulikana kwenye uso wa Bongo Fleva.
Sijui kilichopo nyuma ya pazia kwake kwa sasa lakini kiuhalisia anaon yesha unyonge sana wa kushindwa vita mapema, kwa picha ya nje inaonyesha ni kama Rich Mavoko amekata tamaa baada ya gia zake kutofanikiwa.
Mavoko ni mzoefu, amepitia milima mingi kabla ya kuwa staa mkubwa, kabla ya kusainiwa na WCB alikuwa ameshakuwa msanii mkubwa, najua lengo la kusainia lilikuwa ni kutoka daraja moja kwenda lingine, kama imeshindikana arudi nyuma na kutafakari alipokosea ili ajipange.
Ukitazama nyimbo alizokuwa akizitoa kabla ya kusainiwa na hawa wakati yumo ndani ya lebo unaona ni mtu ambaye anatoa nyimbo zinazoeleweka na zinazohitajika sokoni.
Lakini ukipitia akaunti yake mpya ya YouTube ya Billionea Kid ukasikiliza na kutazama nyimbo zake zilizomo humo na kisha kwenda kufananisha na zile alizokuwa akiimba huko nyuma utakubaliana nami kuwa ‘stresi’ za muziki zinampelekea pabaya.
Ushauri wangu ni kuwa hawezi kufanikiwa akiwa peke yake, atafute watu sahihi nyuma yake ili wamuonyeshe njia sahihi ili yeye aongeze nguvu kwenye kutengeneza muziki, ajitafute tena arejee kwenye ubora wake.
Tofauti na hapo namuona anaelekea kuwa kwenye kundi la wale wasanii ambao kila siku huwa tunasema ni wakali lakini hawana ‘impact’ kwenye Bongo Fleva, yaani wapowapo tu kawaida!
APP YETU MPYA: Sasa unaweza kusoma kwa urahisi kupitia APP yetu. Download hapa kwa KUBOFYA HAPA
0 Comments