Charles James, Michuzi TV
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Dodoma imekiri kumhoji Mbunge wa Jimbo la Mtera mkoani Dodoma, Livingston Lusinde 'Kibajaji' baada ya kupata taarifa za Mbunge huyo kuwakusanya wajumbe wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Chamwino na kuwahonga.
Akizungumza na Michuzi Blog, Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Dodoma, Sosthnes Kibwengo amekiri kumhoji kwa masaa mawili Mbunge huyo jana na kumuachia na kwamba uchunguzi zaidi juu ya tuhuma hizo bado unaendelea.
Kibwengo anasema Ofisi yao ilipata taarifa za Mbunge huyo kuwakusanya wajumbe wa mkutano mkuu wa Chama wa wilaya na wale wa Umoja wa Wanawake Tanzania UWT wilaya ya Chamwino kwa lengo la kuwapatia fedha kwa ajili ya ushawishi ili wamsaidie kwenye kampeni zake za Ubunge.
" Hakuwekwa ndani ila tulimhoji katika Ofisi zetu za Takukuru Wilaya Chamwino kwa masaa mawili au matatu hivi, na taarifa tulizopata ni kwamba anakusanya watu na kuwahonga hatukupata ushahidi wa yeye kuhonga lakini uchunguzi wa hilo jambo bado unaendelea," Amesema Kibwengo.
Usiku wa kuamkia leo kulizuka taarifa za kushikiliwa kwa Mbunge huyo sambamba na baadhi ya wajumbe na wanachama wa CCM.
APP YETU MPYA: Sasa unaweza kusoma kwa urahisi kupitia APP yetu. Download hapa kwa KUBOFYA HAPA
0 Comments