UCHAGUZI MKUU MWAKA HUU WAANDISHI WA HABARI WAJITOSA KUWANIA UDIWANI,UBUNGE | ZamotoHabari.

Na Said Mwishehe,Michuzi TV.

BAADA ya vyama vya siasa nchini kutangaza ratiba ya uchukuaji na urejeshaji fomu za kuwania nafasi za udiwani na ubunge katika Uchaguzi Mkuu mwaka huu, baadhi ya waandishi wa vyombo vya habari nchini wameamua kujitosa kuwania nafasi hizo.

Kuna waandishi walioamua kuonesha nia kwenye nafasi ya udiwani, na wengine kwenye nafasi ya ubunge.Waandishi hao wapo ambao wametangaza hadharani na wengine wametumia mitandao yao ya kijamii kueleza dhamira waliyonayo kwenye kuomba ridhaa ya wananchi katika uchaguzi mkuu mwaka huu.

Hata hivyo kwa sehemu kubwa ya waandishi hao ambao wameonesha nia hiyo ya kuomba ridhaa ya kugombea ubunge wameamua kutumia Chama Cha Mapinduzi(CCM).

Michuzi TV na Michuzi Blog kwa nyakati tofauti imepata nafasi ya kuzungumza na baadhi ya waandishi hao ambapo wengi wao wamesema kutokana na kazi kubwa ambayo inafanywa na CCM pamoja na Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dk.John Magufuli wanaona ni wakati muafaka kwao kuomba ridhaa na watakapopata nafasi washiriki vema kwenye ujenzi wa maendeleo ya Tanzania.

Wengine wamesema Serikali ya Awamu ya Tano imeonesha kwa vitendo namna ambavyo inatambua mchango wa vyombo vya habari katika kushriki kuleta maendeleo, hivyo ni wakati sahihi kwao kuingia kwenye vyombo vya maamuzi.

Katika waandishi hao ambao wameamua kugombea mwaka huu wapo ambao wameamua kukaa kimya hadi sasa wakiendelea kusoma upepo unavyokwenda lakini wengine wao tayari wametangaza na baadhi ya waliojitangaza kwa kutumia njia mbalimbali zikiwemo ya mitandao ya kijamii ni Dk.Kanael Kaale jimbo la Vunjo na Suleima Msuya anayekwenda kugombea jimbo Mwanga.

Pia yumo mwandishi Edith Karlo aliyeko mkoani Kigoma, Sharifa Marira jimbo la Same Magharibi, Albert Kawogo jimbo la Bagamoyo,Rashid Mtagaruka jimbo la Mchinga pamoja na Dk.Frank Mbunda.

Hata hivyo kadri muda wa uchukuaji fomu unavyokwenda ndivyo idadi ya waandishi watia nia itakavyoendelea kuongeza kwani wapo wengine ambao pamoja na kuwa na nia hiyo wameomba majina yao kwa sasa yahifadhiwe kwanza na kisha wakati ukifika watatoa taarifa kwa umma.



APP YETU MPYA: Sasa unaweza kusoma kwa urahisi kupitia APP yetu. Download hapa kwa KUBOFYA HAPA

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini