WAZIRI WA AFYA AJITOSA KUGOMBEA UBUNGE JIMBO LA TANGA,AWASHUKURU AKINA MAMA | ZamotoHabari.


Na Mashaka Mhando, Tanga

WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu, amechukua fomu ya kugombea ubunge Jimbo la Tanga, huku akiwashukuru akina mama kwa kumpa kitenge alichoshona na kukivaa wakati akichukua fomu hiyo.

Ummy alifika katika ofisi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) eneo la masiwani na kukabidhiwa fomu yake na Katibu wa CCM Tanga Mjini Salim Kidima.

"Nawashukuru akina mama mmenipa kitenge na pesa za mashono, leo nimekivaa na nimechukua fomu, nawashukuru sana, " alisema Ummy mara baada ya kukabidhiwa fomu hiyo.

Alisema anawashukuru watu wote wanaomuunga mkono katika hatua hiyo ya kugombea Jimbo la Tanga, na wakati rasmi ukifika ataeleza kwanini amewakubalia kugombea.

"Ndugu zangu wakati ukifika nitasema kilichonisukuma kugombea lakini kwa sasa itoshe kusema nawashukuru wote kwa kuniunga mkono," alisema Waziri Ummy.

Waziri Ummy amejizolea umaarufu mkubwa kutokana na kutimiza majukumu yake tangu alipoteuliwa na Rais John Magufuli kushika wadhifa wa wizara hiyo.

Na hata wiki iliyopita akiwa katika uzinduzi wa vituo vya afya vilivyopo Jijini Tanga, akina mama wa Kata ya Mabawa walimpa sh 30,000 na kitenge kwa ajili ya kukishona ili akivae akichukua fomu.

Katika hatua nyingine aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Tanga Kassim Mbughuni alitinga akiwa na baiskeli kuchukua fomu ya kugombea Jimbo hilo la Tanga.

Mbughuni ambaye alikuwa mwenyekiti mwaka 2012 hadi 2017, amechukua fomu ili awawakilishe wananchi wa Jiji hilo.

Hadi kufikia jana mchana Wana-CCM 17 wamechukua fomu ya kuomba kuchaguliwa kuwa wabunge wa Jimbo la Tanga ambalo mwaka 2015 lilichukuliwa na Mussa Mbaruok wa Chama Cha Wananchi (CUF).

Katibu wa CCM wilaya ya Tanga Salim Kidima akimkabidhi fomu ya ubunge Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu akiwa ameshika fomu yake mara ya kukabidhiwa na katibu wa CCM Salim Kidima (kushoto)

Akizungumza na wananchi waliojitokeza kumsindikiza mara baada ya kuchukua fomu


APP YETU MPYA: Sasa unaweza kusoma kwa urahisi kupitia APP yetu. Download hapa kwa KUBOFYA HAPA

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini