Na Jumbe Ismailly MKALAMA
WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi,Mh.Luhaga Joelson Mpina amewaagiza wakurugenzi wa Halmashauri 82 za Tanzania Bara ambazo hazijatoa kabisa huduma za chanjo ya mifugo au walitoa kwa kiwango kidogo chanjo hiyo,kuanza mara moja kuchanja mifugo hiyo kwenye maeneo yao.
Waziri Mpina alitoa agizo hilo katika Kijiji cha Kinyangiri,wilayani Mkalama,Mkoani Singida wakati wa uziznduzi wa Kampeni ya Kitaifa ya chanjo ya kuzuia ugonjwa wa homa ya mapafu.
Aidha Waziri huyo alifafanua kwamba Halmashauri 103 kati ya 185 sawa na asilimia 56 ndizo ambazo zimekuwa zikitoa huduma za baadhi ya chanjo kwa mifugo,ambapo kwa mwaka 2019/2020 jumla ya dozi 53,851,850 zilichanjwa.
“Hii ni idadi ndogo ukilinganisha na idadi ya mifugo na chanjo za kipaumbele zinazotakiwa kutolewa na hivyo nitumie muda huu kuwaelekeza Wakurugenzi wa Halmashauri 82 Tanzania Bara ambao aidha hawatoi kabisa huduma za chanjo au wanatoa kwa kiwango kidogo kuanza mara moja kuchanja mifugo.”alisisitiza Waziri huyo wa Mifugo na Uvuvi.
Kwa mujibu wa Waziri huyo kutokana na kutotoa kabisa huduma hiyo ya chanjo au kutoa kwa kiwango kidogo kiasi ambacho hakuna hata takwimu zake,hivyo aliwaagiza wakurugenzi hao kuanza mara moja kuchanja mifugo kwenye maeneo yao.
Waziri huyo wa Mifugo na Uvuvi hata hivyo alisisitiza kwamba sheria ya magonjwa ya wanyama imesema wazi juu ya udhaifu huo wa kutotoa chanjo lakini sheria ya usatwi wa wanyama pia na yenyewe inazungumza wajibu wa kila Halmashauri na wajibu wa kila mtaalamu kuwajibika kuchanja mifugo.
Akizungumzia kuhusu Halmashauri zinazochukua chanjo na kutorejesha fedha kwa Wakala wa Maabara Tanzania (TVLA),Mpina aliweka bayana kwamba ili kuongeza ufanisi katika kuzalisha chanjo,aliziagiza Halmashauri zote zinazodaiwa na TVLA kwamba ifikapo Aug,30,mwaka huu ziwe zimelipa madeni yake yote.
Katika kuimarisha huduma ya chanjo na upatikanaji wa chanjo wa uhakika nchini,wakala wa Maabara Tanzania (TVLA) imetakiwa kutoa chanjo kwa Halmashauri mbali mbali nchini kwa makubaliano kwamba mara baada ya kuchanja,fedha itarejeshwa kwa wakala ili kuendeleza uzalishaji wa chanjo.
Hata hivyo wazziri huyo mwenye dhamana ya kusimamia sekta ya mifugo na uvuvi aliweka bayana kuwa Halmashauri nyingi zimekuwa zikizingatia utaratibu wa marejesho,lakini chache zimekuwa na madeni sugu nay a muda mrefu na hivyo kukwamisha shughuli za uzalishaji wa chanjo.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Maabara ya Veterinary Tanzania (TVLA),Dkt.Furaha Mramba alibainisha lengo la kuanzishwa kwa Maabara hiyo mwaka 2012 kuwa ni pamoja na kufanya kazi za uchunguzi,utambuzi wa magonjwa ili waweze kujua kwamba mifugo yao inapougua ni kitu gani wanachotakiwa kufanya na ni dawa gani wanayotakiwa kutumia.
“Mheshimiwa waziri Taasisi ya chanjo Kibaha imeanzishwa ili nchi iweze kuzalisha chanjo zote muhimu zitakazokidhi mahitaji ya idadi kubwa ya mifugo kwa ajili ya kuweza kufanya upungufu au kuondoa kabisa magonjwa yale yanayowezekana kuondolewa.”alifafanua daktari huyo wa Maabara ya Mifugo.
Naye Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo,Wizara ya Mifugo na Uvuvi,Profesa Hezron Nonga alibainisha kuwa ili kukabiliana na magonjwa mbali mbali ya mifugo,Wizara ilinunua lita 12,54.50 za dawa za kuogesha mifugo ambazo ziliwezesha michovyo 211,037,290 kufanyika.
Kwa mujibu wa Profesa Nonga jumla ya michovyo iliyofanyika kwa ng’ombe ni 149,954,080,mbuzi 45,477,778 na kondoo ni michovyo 15,605,431.
Mkuu wa wilaya ya Mkalama,Mhandisi Jackson Masaka alifafanua kuwa lengo la wilaya hiyo lilikuwa kutoa chanjo kwa mifugo zaidi ya laki moja,lakini mpaka zoezi hilo la chanjo lilipokuwa likiziduliwa,jumla ya ng’ombe 45,000,mbuzi na kondoo wapatao 37,000.
“Kwa hiyo lengo ni zuri tunapoanza kuzindua leo chanjo unazindua ukiwa na kianzio cha mifugo iliyochanjwa karibu 70,000 Mkalama na tunaendelea kuchanja.”alibainisha Mkuu wa wilaya huyo.
Hata hivyo Mhandisi Masaka alitumia pia fursa ya uzinduzi wa kampeni hiyo ya kitaifa ya chanjo kuiomba wizara ya mifugo na uvuvi kuangalia uwezekano wa kuwajengea viwanda vinavyotoa biadhaa za mifugo,kama vile viwanda vya kuchinja au vinavyochakata nyama za kuku na ngozi.
Kwa upande wao baadhi ya wafugaji waliopatiwa huduma hizo za chanjo ya kuzuia ugonjwa wa homa ya mapafu,pamoja na kuipongeza wizara hiyo na kuelezea sababu zilizokuwa zikikwamisha zoezi hilo katika siku za awali kuwa ni bei kubwa ya madawa ya chanjo hizo.
Waziri wa Mifugo,Luhaga Mpina akiongea na wananchi pamoja na wafugaji wa Kijiji cha Kinyangiri wilayani Mkalama mkoani Singida kabla ya kuzindua kampeni ya chanjo ya ugonjwa wa homa ya mapafu.
aziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina akitekeleza masharti ya wataalamu wa afya juu ya kujikinga na ugonjwa wa korona kwa kunawa maji tiririka mara abaada ya kuwasili kwenye viwanja vya mnada wa mifugo wa Kijiji cha Kinyangiri kulikofanyika zoezi la uzinduzi wa kampeni ya chanjo ya ugonjwa wa Homa ya mapafu.
Wataalamu wa mifugo wakimkabidhi Waziri wa Mifugo na Uvuvi sindano ya kutolea chanjo ya mifugo ya kuzuia ugonjwa wa Homa ya mapafu ili aweze kuzindua chanjo hiyo iliyofanyika kitaifa katika Kijiji cha Kinyangiri, wilayani Mkalama.
Baadhi ya Mifugo ya wafugaji wa Kijiji cha Kinyangiri, wilaya ya Mkalama iliyoletwa kwa ajili ya kupatiwa chanjo ya kujikinga na ugonjwa wa Homa ya mapafu.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi,Luhaga Mpiana akisaidiana na wafugaji kuswaga ng;'ombe ili waweze kuingia kwenye kibanio cha kuchanjia mifugo ili waweze kupatiwa chanjo ya kinga ya ugonjwa wa Homa ya mapafu.(Picha zote Na Jumbe Ismailly)
APP YETU MPYA: Sasa unaweza kusoma kwa urahisi kupitia APP yetu. Download hapa kwa KUBOFYA HAPA
0 Comments