Kikwete aishauri Yanga "Achaneni na mvutano wa Morrison kwa kuwa mwanapoteza muda" | ZamotoHabari.


 ALIYEKUWA Rais wa awamu ya nne wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete ameishauri Yanga kuachana na mvutano wa suala la mchezaji, Bernard Morrison kwa kuwa wanapoteza muda na badala yake wawekeze nguvu kuibua vipaji vipya
Kikwete ameyasema hayo jana, Agosti 30 kwenye Kilele cha Wiki ya Mwananchi ampabo yeye alikuwa ni mgeni rasmi Uwanja wa Mkapa.

Morrison amekuwa kwenye mvutano na Yanga kuhusu suala la mkataba, Yanga inaeleza kuwa ana mkataba wa miaka miwili huku Morrison akisema dili lake la miezi sita lilikwisha.

Shauri hilo lilisikilizwa Makao Makuu ya Shirikisho la Soka Tanzania,(TFF) na Kamati ya Hadhi ya Wachezaji Tanzania kwa muda wa siku tatu mfululizo kuanzia Agosti 10-12 na mwisho Morrison alitangazwa kuwa mshindi kwa kile kilichoelezwa kuwa kulikuwa na mapungufu kwenye mkataba.

Kikwete amesema:"Naskika ninyi mwaka huu mmeibiwa mchezaji na majirani zenu,hilo ni jambo la kawaida kwani masuala haya kwa watani wa jadi hayajaanza leo ni tangu zamani yalikuwepo haya masuala.

"Kwa kuwa ninyi mmeibiwa Morrison najua nanyi mtajipanga wakati mwingine tena mtaiba mchezaji wao mzuri ni kawaida. Lakini naona masuala haya ya kupelekana FIFA ni kupoteza tu muda kwani kuna namna ya kufanya ili kutofikia hatua hiyo.

"Kinachotakiwa ni kuibua vipaji wenyewe ndani ili iwe rahisi kuwapata nyota ndani ya nchi, sasa leo tunagombania mchezaji kutoka nje na pia tumesajili wachezaji kutoka nje hii isingekuwepo kama tungekua tunaibua vipaji vyetu. Tumeona kuna makocha wa kigeni waliletwa hawa wa kuokotaokota matokeo yao yalivyokuwa ilionekana ila simtaji ni nani," amesema.

Agosti 22, Morrison, kilele cha Simba Day, Uwanja wa Mkapa alitambulishwa kuwa mchezaji wa Simba.Agosti 30, kilele cha Wiki ya Mwanachi alitambulishwa kuwa mchezaji wa Yanga kwa kuwa shauri lake limepelekwa Mahakama ya Usuluhishi wa Kimichezo,(Cas).

APP YETU MPYA: Sasa unaweza kusoma kwa urahisi kupitia APP yetu. Download hapa kwa KUBOFYA HAPA

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini