Ndoa ya MONDI, ZUCHU Utamu Unakuja, unakata | ZamotoHabari.


NDOA anayotarajia kufunga mwanamuziki mkubwa barani Afrika, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ imeibua mambo mazito, huku akihusishwa na msanii wake, Zuhura Othman ‘Zuchu’.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, Diamond au Mondi alitangaza kufunga ndoa Oktoba 2, mwaka huu ambayo ni siku ya kumbukumbu ya kuzaliwa kwake (birthday).

UTAMU UNAKUJA, UNAKATA

Chanzo kutoka ndani ya familia ya Mondi kimedai kwamba, kuna shinikizo kubwa kwa jamaa huyo kutoka kwa baadhi ya ndugu ambao wanamtaka amuoe Zuchu, jambo ambalo linaleta utamu na furaha ndani yao.

Lakini wapo ambao wanachukizwa mno na taarifa au shinikizo hilo la Mondi kutakiwa amuoe Zuchu, hivyo hao ndiyo wanakata kabisa utamu wa tukio hilo.

VUGUVUGU LA MONDI KUMUOA ZUCHU

Vuguvugu la Mondi kutakiwa kumuoa Zuchu, lilianza muda mfupi tu baada ya Aprili 8, mwaka huu, pale mrembo huyo aliposainiwa kwenye Lebo ya Wasafi Classic Baby (WCB) chini ya Mondi.

Baada ya hapo, wawili hao wakawa wanapostiana kwenye mitandao ya kijamii na familia ya Mondi kumsifi a mno Zuchu kwa kufungua ukurasa mpya wa maisha ndani ya familia yao.

Mtoa habari wetu huyo ndani ya familia hiyo alisema;

“Asikwambie mtu, familia ya Nasibu (Mondi) hasa mama yake mzazi (Sanura Kassim ‘Mama Dangote’) anatamani sana Zuchu ndiye aolewe na mwanaye.

“Yaani Mama Dangote anasema kabisa kwamba, anafurahi sana kumuona Nasibu (Mondi) na Zuchu kwani wanapendezeana mno.
“Kwa kuwa Nasibu (Mondi) hapindui kwa mama yake, amemwambia hawezi kupingana na mtazamo wake,” kilidai chanzo chetu.

Yote haya yanakuja siku chache baada ya Mondi kutamka kuwa kwa sasa hahitaji tena maisha ya kurukaruka na wanawake na kwamba, jamii ikimsikia, basi atakuwa ameoa.


SHINIKIZO MITANDAONI

Katika hali inayoonesha kuwa mashabiki wa Mondi wanaipenda ‘kapo’ yake na Zuchu, mara kadhaa wamekuwa wakishabikia na kuwasifia wanapowaona wawili kwenye picha ya pamoja.

Wawili hao wamekuwa wakiibua shangwe kama lote mitandaoni kwa upande wa mashabiki wao na inapotokea mmoja akasema hawaendani, basi anakuwa amesababisha uvunjifu wa amani, kwani anakuwa amewakata stimu na kuishia kuoga matusi ya nguoni.


“Mungu ni mwema jamani, yaani natamani tu kuiona kapo ya Mondi na Zuchu, kiukweli wanapendezeana sana.
“Ona wakivaa nguo zinazofanana, wanaendana…
“Mondi vuta chuma hicho kimejileta chenyewe usafi ni…”
“Wachawi sijui wataweka wapi sura zao…
“Anayesema hawaendani anatukata kabisa stimu na kutuondolea utamu.”



Hizo ni baadhi ya komenti ambazo zilipostiwa kwenye Mtandao wa Instagram kwenye kurasa za watu tofautitofauti walioripoti wawili hao kuhisiwa kuwa ni wapenzi.



FAMILIA YAGAWANYIKA

Aidha, gazeti hili lilipofanya mahojiano na mmoja kati ya ndugu wa Mondi ambaye aliomba hifadhi ya jina kwa kuwa siyo msemaji wa familia hiyo na kumuuliza kuhusu kinachoendelea kwa wawili hao, alisema;



“Nakuambia utamu unakuja ‘then’ unakata. Unakuja kwa maana ya baadhi ya ndugu tunaunga mkono na tumefurahi na hata hiyo ndoa yao ikitokea, itakuwa pambe, lakini wapo ambao hawataki na hawa ndiyo wanasababisha utamu unakata.”



WAKANUSHA SIYO WAPENZI

Hata hivyo, mara kadhaa Mondi na Zuchu wamekuwa wakikanusha kwa nguvu kubwa kuwa, hawana uhusiano kama huo, kwani wanaheshimiana kama mtu na bosi wake au mtu na kaka yake.

“Ninamheshimu sana Diamond kama bosi wangu, sijawahi kutoa hata busu ili anisaidie,” alisema Zuchu.

KWA NINI ZUCHU KWA MONDI?

Tangu kusainiwa kwa Zuchu ndani ya Wasafi , kumekuwa na sintofahamu kwa baadhi ya mashabiki wao kiasi cha kufi kia hatua ya kutaka kugombana pale unapoibuka ubishi wa ama ni wapenzi au la?


Kuna ambao wamekuwa wakigeuka mbogo kwa kusema kuwa, kudai Mondi anatoka kimapenzi na Zuchu, ni kama kumtusi staa huyo, kwani anaheshimiana vilivyo na mama mzazi wa binti huyo, Malkia wa Taarab, Khadija Omari Kopa ‘Bi Khadija’.

Miongoni mwa mambo yanayochochea tetesi za Mondi kuwa mbioni kumuoa Zuchu, ni matukio ya wawili hao yenye viulizo vingi.

Tukio la Mondi kuonekana anaingia na Zuchu kwenye harusi ya dada yake, Esma Khan kule Madale na Ukumbi wa Lugalo Golf jijini Dar, limekuwa ni tukio ambalo linazungumzwa mno kuwa huwenda kuna kitu kinaendelea baina yao.

Baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo, walisema si mara ya kwanza kwa wawili hao kuingia pamoja kwenye shughuli mbalimbali, hata kwenye hafl a ya Zuchu pale Mlimani City, Julai 18, mwaka huu ilikuwa hivyohivyo. Siku hiyo, Mondi aliingia akiwa amemshika mkono Zuchu na kupiga picha za pamoja kwenye zulia jekundu kama ilivyofanyika Madale.

Matukio mengine mbali na shughuli ya Esma yanayotajwa kuibua hisia hizo ni pamoja na lile la Mondi kumfanyia Zuchu shopping ya mamilioni.

Tukio lingine lililoibua maswali ni lile la Mondi kumzawadia Zuchu ndinga kali aina ya Toyota Vanguard, jambo ambalo hajawahi kulifanya kwa msanii wake mwingine, hivyo mengine muda utasema, tusubiri!


ZUCHU NI NANI?

Zuchu ni msanii wa pili wa kike kusainiwa Wasafi baada ya dada yake Mondi, Mwanahawa Abdul ‘Queen Darleen’.

Tangu Zuchu asajiliwe hivi karibuni, amekuwa akipewa kipaumbele kimuziki na Mondi, jambo ambalo limezua maswali na wengine kumsihi Zuchu kuwa makini, asije akaingia kwenye himaya ya mapenzi ya msanii huyo, kwani mwisho wake hautakuwa mzuri.

STORI: SIFAEL PAUL, DAR

APP YETU MPYA: Sasa unaweza kusoma kwa urahisi kupitia APP yetu. Download hapa kwa KUBOFYA HAPA

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini