Na Bakari Madjeshi, Michuzi TV.
Tuzo za Ligi Kuu Soka Tanzania Bara zimetolewa leo August 7, 2020 katika Ukumbi wa Mikutano wa Mlimani City uliopo jijini Dar es Salaam wakati Nyota mbalimbali, Makocha na Timu ziking'ara katika tuzo hizo zilizovutia wengi akiwemo Kiongozi wa Serikali, Waziri wa TAMISEMI, Mhe. Suleiman Jafo ambaye alikuwa Mgeni rasmi katika sherehe hizo.
Tuzo hizo zimeonekana kung'ara zaidi kwa Kiungo wa Kimataifa wa Zambia, Cloutous Chama (Mwamba wa Lusaka) aliyeondoka na tuzo tatu peke yake katika sherehe hizo, Chama ameondoka na tuzo ya Mchezaji Bora amepata zawadi (Tsh. Milioni 10/-), Kiungo Bora wa msimu wa VPL, na kuingia kwenye jopo la Nyota wanaounda Kikosi Bora cha msimu huo sambamba na kuwa Mchezaji Bora wa Mashindano ya Kombe la Shirkisho (FA) na Mchezaji Bora wa Mashabiki (Sportpesa).
Baba Mzazi wa Haji Manara, Nyota wa zamani wa Yanga SC, na Mchezaji wa kwanza kucheza nje ya nchi, Sunday Manara (Computer) yeye alitwaa Tuzo ya Heshima iliyotajwa na Rais wa TFF, Wallaace Karia katika sherehe hizo, sambamba na kutia kibindoni kitita cha Shilingi Milioni 3 za Kitanzania.
Katika tuzo hizo, Mshambuliaji wa Kimataifa wa Rwanda, Meddie Kagere yeye ameibuka kuwa Mfungaji Bora baada ya kufumnia nyavu mara 22 msimu mzima wa Mashindano hayo ya Ligi Kuu na kujinyakulia kitita cha Shilingi Milioni 10 za Kitanzania. kama zawadi.
Mchezaji Bora Chipukizi, tuzo imeenda kwa Mshambuliaji wa Biashara United ya Mara, Novatus Dismas aliyewabwaga Beki wa Mtibwa Sugar, Dickson Job na Kelvin Kijiri wa KMC ya Dar es Salaam.
Tuzo ya Kocha Bora wa Msimu imebebwa na Kocha Mkuu wa Simba, Sven Vandenbroeck aliyenyakua kitita cha Shilingi Milioni 7 za Kitanzania baada ya kuwabwaga Kocha Mkuu wa Namungo FC, Hitimana Thienry na Kocha wa Azam FC, Aristica Cioaba.
Tuzo ya Golikipa Bora wa Mashindano imeenda kwa Kipa namba moja wa Simba SC, Aishi Salum Manula baada ya kuwa na msimu mzuri wa Mashindano kwa kuwabwaga Golikipa Nourdine Barola na David Mgore wa Biashara United.
Mwamuzi Bora Msaidizi mchuano mkali ulikuwa kwa Hamdun Said wa Mtwara, Frank Komba wa Dar es Salaam na Abdulaziz Ally wa Arusha, Mshindi wa tuzo hiyo ni Frank Komba baada ya kuwabwaga wenzake hao katika kinyang'anyiro hiko wakati huo Mwamuzi wa Kati Ramadhan Kayoko wa Dar es Salaam akiibuka kidedea kuwa Mwamuzi Bora wa msimu akiwabwaga Ahmed Ally wa Manyara na Abdallah Mwinyimkuu wa Singida.
Beki Bora wa msimu tuzo imeenda kwa Beki wa pembeni wa Azam, Nicholas Wadada aliyewashinda David Luhende wa Kagera na Bakari Nondo Mwamunyeto aliyekuwa Coastal Union ya Tanga ambaye kwa sasa amesajiliwa Yanga SC.
Katika Mashindano ya Msimu huu, Tuzo ya Goli Bora imeenda kwa Mshambuliaji wa Mbeya City, Patson Shigala aliyefunga bao safi dhidi ya JKT Tanzania katika dimba la Sokoine mjini Mbeya na kuwabwaga Luis Josse Miquisson wa Simba SC na Sadala Lipangile wa KMC.
Mabingwa wa Ligi Kuu Soka Tanzania Bara, Simba SC wamejinyakulia kitita cha Shilingi Milioni 100/-, Yanga SC wameshika nafasi ya pili wameshinda Milioni 45/-, Azam FC nafasi ya tatu Milioni 30/- na Namungo FC nafasi ya nne wameshinda Milioni 10/-. Timu yenye nidhamu, Kagera Suga imeondoka na kitita cha Shilingi Milioni 15/- baada ya kuzishinda timu za Coastal Union ya Tanga na Mwadui FC ya Shinyanga.
Kikosi Bora cha Msimu wa VPL msimu wa 2019-2020 ni Golikipa, Aishi Manula (Simba SC), Mabeki, Nicholas Wadada (Azam FC), David Luhende (Kagera Sugar), Bakari Mwamunyeto (Coastal Union/Yanga SC), Pascal Wawa (SimabSC), Viungo ni Zawadi Mauya (Kagera Sugar/Yanga SC), Lucas Kikoti (Namungo FC) na Cloutous Chama (Simba SC), Washambuliaji ni Meddie Kagere (Simba SC), John Raphael Bocco (Simba SC) na Luis Josse Miquissone (Simba SC).
Mgeni rasmi, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Suleiman Said Jafo akimkabidhi kiungo wa Simba SC, Clatous Chama tuzo ya Mchezaji Bora wa Ligi Kuu
MLINDA mlango namba moja wa Simba, Aishi Manula amechaguliwa kuwa Golikipa Bora wa Msimu wa 2019/20.Tuzo imepokelewa na Mkurugenzi wa Wanachama na Mashabiki, Hashim Mbaga.
CLATOUS Chama, kiungo wa Simba ametwaa tuzo ya Kiungo Bora ndani ya msimu wa 2019/20
Nicolas Wadada, beki wa Azam FC amekabidhiwa tuzo ya beki bora kwa msimu wa 2019/20.
KOCHA Msaidizi wa Simba Suleiman Matola, amepokea Tuzo ya Kocha Bora wa mwaka kwa niaba ya Sven Vandenbroeck ambaye ni Kocha Mkuu wa Simba.
Paston Shikala, nyota wa Mbeya City ameibuka mshindi wa tuzo ya bao bora kwa msimu wa 2019/20.
Meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu amepokea Tuzo ya Mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Vodacom kwa niaba ya Meddie Kagere raia wa Rwanda ambaye amefunga mabao 22 ndani ya ligi.
Kikosi Bora cha msimu wa 2019/20.
APP YETU MPYA: Sasa unaweza kusoma kwa urahisi kupitia APP yetu. Download hapa kwa KUBOFYA HAPA
0 Comments