WANANCHI RUNGWE WAIPONGEZA SERIKALI KUWAONDOLEA KERO YA MAJI | ZamotoHabari.

Na Mohamed Saif

Wananchi wa Kijiji cha Bulongwe Wilaya ya Rungwe Mkoani Mbeya waimeipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kupitia Wizara ya Maji kwa jitihada zake za kuwaondolea kero ya maji iliyowasumbua kwa kipindi kirefu.

Pongezi hizo zimetolewa kwa nyakati tofauti Julai hapo juzi wakati wa ziara ya Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga ya kukagua utekelezaji wa miradi ya Maji Mkoani humo na kuzungumza na wanufaika wa miradi hiyo.

Akiwa kwenye mradi wa Masoko Skimu ya Bulongwe Wilayani Rungwe, Mhandisi Sanga alisema kuwa wakati wa kampeni za Urais Mwaka 2015, Rais Dkt. John Pombe Magufuli aliahidi kuwa wananchi hao watafikiwa na huduma ya majisafi na salama na kwamba ziara yake wilayani humo imelenga kukagua utekelezaji wa ahadi hiyo sambamba na kubaini changamoto zilizopo kwa lengo la kuzipatia ufumbuzi wa haraka.

"Rais Magufuli aliahidi na alituelekeza kuhakikisha wananchi wake wa Rungwe wanapata huduma ya maji, nipo hapa kukagua utekelezaji wa maelekezo hayo pamoja na kuona namna ya kuboresha zaidi huduma ya maji kwa wananchi wasiokuwa na huduma" alisema Mhandisi Sanga.

Aidha, akizungumza kwa niaba ya wananchi wa Kijiji cha Bulongwe Mwenyekiti wa Kijiji, Gibons Mwapangala alisema kero ya maji ilikuwa ni ya muda mrefu lakini kupitia Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli kero hiyo imekuwa historia.

“Kiukweli kwa niaba ya wananchi wa Bulongwe ninampongeza na kumshukuru sana Rais wetu, kero ya maji ilitusumbua sana, lakini yeye alipita hapa na alituahidi kwamba tutapata maji na kweli tumeyapata,” alisema Mwapangala.

Hata hivyo alibainisha kwamba kuna maeneo machache ambayo bado hayajafikiwa na huduma na alimuomba Katibu Mkuu Sanga kufikisha huduma kwenye maeneo hayo.

Kwa upande wake Mhandisi Sanga aliielekeza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mbeya (Mbeya UWSA) kukutana haraka na wananchi ambao bado hawajafikishiwa huduma na alitoa Siku 14 maeneo yote ambayo hayajafikishiwa yawe yamefikishiwa huduma.

"Nawaelekeza Mamlaka ya Maji Mbeya pamoja na Wakala wa Maji Vijijini (RUWASA) Wilaya ya Rungwe kukutana na wananchi wa Bulongwe siku ya Jumatatu Agosti 10, 2020 na mhakikishe ndani ya Siku 14 kutoka sasa muwe mmewafikishia maji," alielekeza Mhandisi Sanga. 

Aidha, akiwasilisha taarifa ya mradi, Mhandisi wa Maji, Mamlaka ya Maji Mbeya (Mbeya UWSA), Raphael Kolong'onyo alisema mradi huo unatekelezwa na wataalam wa ndani kwa mfumo wa force account na kwamba utekelezaji wake ulianza Septemba, 2019 na hadi hivi sasa ujenzi wake umefikia asilimia 97. 

"Tayari baadhi ya wananchi wanapata huduma lakini wachache tunaendelea kuwasogezea kwani tunatarajia kuukamilisha hapo Septemba, 2020 na utakuwa umegharimu jumla ya shilingi milioni 547," alisema Mhandisi Kolong'onyo. 

Kukamilika kwa mradi huo wa Bulongwe kutanufaisha zaidi ya wananchi 10,000 kutoka vijiji sita ambavyo ni Bulongwe, Ngaseke, Igembe, Ntandabala, Bujera na Nsongola.
 Mkuu wa Wilaya ya Rungwe, Chalya Nyangindu akitoa taarifa ya Sekta ya Maji ya Wilaya ya Rungwe kwa Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga.

 Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga (kushoto) akisalimiana na wananchi wa Kijiji cha Bulongwe, Wilaya ya Rungwe Mkoani Mbeya wakati wa ziara ya kukagua ujenzi wa miradi wilayani humo.
 Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga (kushoto) akiwasikiliza wananchi wa Bulongwe (hawapo pichani) wakati wa ziara ya kutembelea mradi wa maji Bulongwe. Kulia ni Mhandisi wa mradi kutoka Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mbeya (Mbeya UWSA), Raphael Kilong’onyo.
 Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga (kushoto) akiwasikiliza wananchi wakati wa ziara ya kutembelea mradi wa maji Bulongwe. 



APP YETU MPYA: Sasa unaweza kusoma kwa urahisi kupitia APP yetu. Download hapa kwa KUBOFYA HAPA

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini