Aibu! Askofu Anayetuhumiwa UZINZI Avamiwa Madhabahuni na Kuvuliwa Kofia | ZamotoHabari.



ZANZIBAR: Timbwili kuzuka baa si hoja; lakini askofu kuvamiwa madhabahuni, kusukwasukwa mpaka kuvuliwa kofia, ni jambo la aibu kufanywa kanisani.


Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Mjini Zanzibar, Michael Henry Hafidh, Jumatatu wiki hii alijikuta kwenye wakati mgumu baada ya baadhi ya waumini wake kumvamia kanisani wakimtuhumu kwa ufisadi na mambo mengine.


 


DOKEZO MUHIMU


Askofu Hafidh hivi karibuni ameburuzwa Mahakama Kuu ya Vuga mjini humo, akikabiliwa na tuhuma za uzinzi.


Kesi hiyo Namba 21/2020 ilianza kutajwa mahakamani hapo Juni 29, mwaka huu mbele ya Mheshimiwa Jaji, Dkt. Yessaya Kayange, huku mlalamikaji mkuu akitajwa kuwa ni Saburi Khamis mkazi wa Visiwani humo.


WAUMINI WANA NINI TENA?


Ikiwa shauri la uzinzi wa askofu huyo liko mahakamani kutafutiwa haki kisheria, waumini wana lipi tena la kumsumbua mtumishi huyo wa Mungu?


Majibu ni kwamba, Askofu Hafidh anadaiwa kuwaengua baadhi ya watumishi wenzake ambao hawamuungi mkono na kutaka kuwasimika mapadri wapya ambao wanamsapoti.


Kitendo hicho kimeleta mpasuko mwingine mkubwa ndani ya kanisa hilo ambapo kundi linalompinga askofu Hafidh, linasema “haiwezekani” na lile linalomuunga mkono likipigania “inawezekana.”




IKAWAJE SASA?


Sakata hilo lilianza kutimua vumbi mapema Jumatatu iliyopita siku ambayo Askofu Hafidh alikuwa ameandaa ibada ya kuwasimika mapadri wake wapya, lakini zoezi hilo lilivurugwa kwa nguvu na waumini wanaompinga.


Mapema siku ya tukio mwandishi wetu alifikia kanisani hapo na kuwakuta waumini wa kanisa hilo wakiwa wamefunga milango ya kanisa hilo pamoja na ofisi ya askofu huyo.


Akiwa kanisani hapo, mwandishi wetu aliwashuhudia waumini hao wakiwa na mabango yaliyoandikwa tuhuma mbalimbali za askofu Hafidh, huku mengine yakiwa yamebandikwa kwenye milango iliyokuwa imefunga.


Baadhi ya mabango hayo yalisomeka: “Umekiuka viapo vyako vyote, katiba huifuati, ondoka.”


“Umemaliza pesa za dayosisi, sasa umefuata za mtaa.”




WAIMARISHA ULINZI


Baada ya kufunga milango, kubandika mabango na mengine kuyashika mikononi, waumini hao ‘waasi’ wa askofu, waliweka ulinzi na kujiapiza kuwa hawatamruhusu askofu huyo na waumini wake kuingia kanisani.


Ikumbukwe kuwa, ibada hiyo ya kuwasimika mapadri hao iliyotakiwa kuanza saa tisa kamili jioni.


Punde si punde, washika doria hao waliokuwa wakiimba nyimbo za mapambio, walishuhudia umati wa watu waliowasindikiza ndugu zao waliokuwa wakitakiwa kusimikwa daraja hilo la upadri wakiingia kwenye viwanja vya kanisa hilo na hapo mzozo ukaanza.


Wakati vurugu mechi zikiwa zimeshika kasi, askofu Hafidh alifika kanisani hapo lakini alijibanza sehemu kupima hali ya hewa.


Mshikemshike kanisani hapo ulipozidi kati ya wanaosema “inawezekana” na wale wa “haiwezekani”, polisi wakatinga na kuzima vuguvugu hizo kisha kuzikutanisha pande mbili kwa lengo la kuleta mwafaka.


Hata hivyo, lakuvunda huwa halina ubani, kikao hicho cha pande hizo mbili na polisi, hakikuweza kuzaa matunda.


Mtiti wa waumini uliendelea hadi usiku, ambapo baadhi yao waliamua warudi majumbani kulala, huku wengine wakiweka doria kanisani hapo lengo likiwa ni lilelile kutimiza “haiwezekani yao.”


Mawazo ya waumini hao ambao ndiyo walioonekana kuwa na nguvu kuliko wanaomuunga mkono askofu, yalikuwa ni kama machale, kwani ni kweli kesho yake asubuhi (Jumanne) askofu Hafidh na mapadri wake walidamkia kwenye kanisa hilo na kutaka kufanya ibada hiyo.


VURUGU ZAZUKA KWA MARA NYINGINE


Kabla ya kuanza kwa ibada hiyo, waumini wanaompinga askofu huyo waliokesha doria, walianza kuwapigia simu wenzao za “ongezeni nguvu jamaa wamefika huku.”


Dakika chache baadaye, kusanyiko jingine la waasi wa askofu lilifurika kanisani na kuivamia ibada hiyo kwa ujeuri.


Nyumba ya ibada ikageuka kuwa uwanja wa fujo, Askofu Hafidhi akawa siyo muongoza ibada tena, bali mtu aliyekunjwa na kuvuliwa kofia na waumini hao akiwa madhabahuni, tayari kuongoza ibada aliyokusudia kuifanya ambapo polisi kwa mara nyingine walifika na kutuliza ghasia.


TUWASIKILIZE WAASI WA ASKOFU


Kufuatia sakata hilo, mwanahabari wetu alizungumza na mmoja wa wazee wa kanisa hilo aliyeko kundi la uasi aliyejitambulisha kwa jina la Bi. Lili Sudi, ambaye alisema:


“Huyu askofu anachofanya ni kukiuka kiapo alichokula kwa kuwa hapa kanisani sasa hivi pamekuwa na kashfa kibao ikiwemo matumizi mabaya ya madaraka ikiwemo kufuja fedha na kashfa ya ngono inayomkabili mahakamani.


“Lakini cha ajabu, malalamiko yetu yameshafika kwa Askofu Mkuu Maimbo William Mndolwa, lakini tunamshangaa naye anashindwa kuyachukulia maamuzi malalamiko ya waumini ambao tuko wengi kwa sasa.”


Mwingine aliyezungumza maneno kama hayo, ni James Daudi ambaye naye alitoa malalamiko yanayofanana na Bi. Lili.


Waumini wengine nao kwa nyakati tofauti, walitoa malalamiko yao wakimtuhumu askofu huyo kwa makosa mbalimbali.




ASKOFU HAFIDH ATAFUTWA


Baada ya kukusanya data za kutosha na kuondoka eneo la tukio, RISASI JUMAMOSI liliwasiliana kwa njia ya simu na askofu Hafidh ili kujua undani wa tukio hilo na nini mwisho wa mvutano wao, alipopokea simu alisema:


“Ahaa nakupata ndugu yangu, ila sasa nipo kwenye kikao cha amani na mashehe, hivyo naomba nitafute baadaye au nitumie ujumbe.”


Hata hivyo, licha ya kutumiwa ujumbe na kuelezwa juu ya sakata hilo, askofu huyo hakujibu chochote.


KAMANDA WA POLISI ASEMA YAKE


Baada ya kuachana na askofu huyo, mwanahabari wetu alimtafuta Kamanda wa Polisi wa Mjini Magharibi, Kamishna Msaidizi (ACP) Mohamed Haji Hassan ambaye alikiri kuufahamu mgogoro ndani ya kanisa hilo na kusema suala hilo wamemwachia mkuu wa mkoa huo (Hassan Khatib Hassan) ambaye anaendelea kuziweka sawa pande hizo zinazopingana.


Mwanahabari wetu alimtafuta mkuu huyo wa mkoa kwa njia ya simu ambapo simu yake iliita bila kupokelewa kila ilipopigwa.



APP YETU MPYA: Sasa unaweza kusoma kwa urahisi kupitia APP yetu. Download hapa kwa KUBOFYA HAPA

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini