YANGA jana imepata ushindi wa jioni wa bao 1-0 dhidi ya Mbeya City kwenye mechi ya Ligi Kuu Bara iliyopigwa Uwanja wa Mkapa, Dar lakini mashabiki wa timu hiyo, wamekunwa na kiwango kilichoonyeshwa na Muangola, Carlinhos katika mchezo huo.Nyota huyo aliingia dakika ya 61 na kushangiliwa san ana mashabiki.
Aliweza kuuchangamsha mpira licha ya kuwa bado hana ‘match fitness’, akionyesha ufundi mkubwa wa kupiga mashuti na pasi muhimu kwa wenzake.
Carlinhos ndiye aliyepiga kona dakika ya 86 akimtengea mpira safi beki kisiki, Lamine Moro aliyefunga bao hilo pekee la Yanga katika mchezo huo uliojaa ushindani mkubwa tangu mwanzo wa mchezo.
Mbeya City walionekana wanataka pointi kutoka kwa Yanga baada ya kuonyesha kiwango safi na kukaza hadi walipoachia dakika ya 86, zikiwa zimebaki dakika nne kabla ya mpira kumalizika.
Carlinhos alipiga shuti kali dakika ya 73 ambalo lilitoka nje kidogo ya lango.
Mashabiki wa Yanga waliokuwa jukwaani walionyesha kukubali kiwango cha mastaa wao mbalimbali akiwemo Carlinhos na walisema timu yao itakuwa moto sana wakiendelea kuzoeana.
Carlinhos alichezewa faulo mbaya na Abdul Selemani dakika ya 90 na alitolewa kwa machela na mchezaji huyo wa City akapewa kadi ya njano. Carlinhos baadaye alirudi uwanjani.
Kwa ujumla, Carlinhos aliyeingia kuchukua nafasi ya Feisal Salum, alipiga kona mbili ambazo hazikuzaa matunda na ile ya tatu aliyopiga dakika ya 86, ndiyo iliyozaa bao.
Ushindi huo unaifanya Yanga kufikisha jumla ya pointi nne ndani ya ligi ikiwa sawa na watani zao wa jadi Simba wakiwa tofauti kwa mabao ya kufunga na kufungwa ambapo Simba imefunga mabao matano na Yanga imefunga mabao mawili.
Mbeya City inabidi wajilaumu wenyewe kwa kuwa walipambana dakika 85 kwa kulinda lango lao na kushindwa kufunga ambapo mshambuliaji wao alikuwa ni Siraj Juma akiwa kinara wa kufanya majaribio ikiwa ni pamoja na ile ya dakika 66 iliyokwenda nje kidogo ya lango,dakika ya 71 na dakika ya 78 alipaisha.
Kwa upande wa Yanga licha ya kushinda bao 1-0 bado walikosa kufunga mabao kutokana na mikono ya mlinda mlango wa Mbeya City, Haruna Mandanda kutimiza majukumu yake.
Aliokoa hatari ya Mustapha Yassin dakika ya 21 ambaye alikuwa akimwaga maji kutoka pembeni kuelekea lango la Mbeya City.
Michael Sarpong ambaye alikuwa na uchu wa kutaka kufunga alikwama kumtungua Mandanda huku Feisal Salum naye kiungo wa Yanga alifanya majaribio mawili makali ambayo yalikwenda nje ya lango ikiwa ni dakika ya 19 na 55. Yacouba Songne alifunga bao dakika ya 84 lakini alikuwa ameotea, hivyo likakataliwa.
Michael Sarpong alipiga mashuti mawili angoni kipindi cha kwanza, moja lililenga goli na jingine lilikwenda nje. Kipindi cha pili alipiga mashuti manne, matatu yakalenga lango na moja halikulenga.Hii ni mechi ya pili kwa Yanga, zote ikicheza kwenye Uwanja wa Mkapa.
Mechi ya awali, ilitoka sare ya 1-1 dhidi ya Tanzania Prisons ambayo nayo ni ya Mbeya.Mechi inayofuata ya Yanga ni dhidi ya Kagera Sugar Jumamosi ijayo kwenye Uwanja wa Kaitaba ambapo itatoka kwa mara ya kwanza kwenye ardhi ya Dar es Salaam.
Kwa upande wa Mbeya City, mechi ya kwanza ilifungwa 4-0 dhidi ya KMC jijini Dar es Salaam, hivyo imepokea vipigo viwili mfululizo licha ya kuonekana ni timu nzuri.
YANGA: Metacha Mnata, Shomari Kibwana, Yassin Mustapha, Lamine Moro, Bakari Mwamnyeto, Mukoko Tonombe, Deus Kaseke, Feisal Salum ‘Fei Toto’, Michael Sarpong, Haruna Niyonzima na Tuisila Kisinda.
CITY: Haroun Mandanda, Kenneth Kunambi, Mpoki Mwakinyuke, Juma Ramadhani, Babilas Chitembe, Abdulrazack Mohammed, Selemani Ibrahim, Abdul Selemani, Rashid Michelenga, Kibu Denis na Siraji Juma.MATokeomengine: Ihefu 1-0 Ruvu Shooting, Uwanja wa Sokoine, bao lilifungwa na Enock Jiah dakika ya 7.Biashara United 1-0 Mwadui FC, Uwanja wa Karume. Bao lilifungwa na Deogratius Judika dakika ya 72.
APP YETU MPYA: Sasa unaweza kusoma kwa urahisi kupitia APP yetu. Download hapa kwa KUBOFYA HAPA
0 Comments