DK.MAGUFULI ASEMA NDANI YA MIAKA MITANO VIJIJI 9570 VIMEUNGANISHWA NA UMEME, KUMALIZIA VILIVYOBAKIA | ZamotoHabari.

Na Said Mwishehe,Michuzi TV-Manyoni

MGOMBEA urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi(CCM) Rais Dk.John Magufuli amesema wakati anaingia mwaka 2015 vijiji ambavyo vilikuwa vimeunganishiwa umeme katika nchi zima vilikuwa 2,018  na sasa baada ya miaka mitano idadi ya vijiji vyenye umeme ni 9,570.

Dk.Magufuli amesema hayo leo Septemba 1 mwaka huu wa 2020 wakati anazungumza na wananchi wa Wilaya ya Manyoni mkoani Singida alipokuwa akizungumza katika mkutano wa kampeni za Uchaguzi Mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba 28 mwaka huu.

Amesema kutokana na jitihada za Serikali katika kuunganisha umeme nchini kwa sasa vimebakia vijiji 2,600 na hivyo wakipata ridhaa ya kuongoza tena kwa miaka mitano mingine watahakikisha wanamalizia vijiji vilivyobakia na hilo halitawashinda.

“Nimekuja hapa kuwaomba kura ,nimekuja hapa kumuombea kura mgombea ubunge wa CCM na nawaombea kura madiwani wote wa CCM, tuchagueni tukamalizie kazi ambayo tumeianza, maendeleo ambayo yamepatikana yanatokana na ninyi , hivyo tupeni nafasi tuendelee kutekeleza miradi ya maendeleo,”amesema Dk.Magufuli.

Akiwa Wilaya ya Ikungi Dk.Magufuli amepata fursa ya kuzungumza na wananchi waliojitokeza kwa wingi kwa ajili ya kusikiliza sera na Ilani ya Uchaguzi Mkuu mwaka 2020 ya CCM ambayo anazunguka kuinadi kwa Watanzania katika kipindi hiki cha kampeni za uchaguzi huo ambapo amesisitiza kuwa wamejipanga vema kuendelea kuwatumikia Watanzania.

Wakati huo huo akiwa katika mikutano yake ya kampeni ya kuomba kura, Dk.Magufuli ameelezea kwa kina jinsi ambavyo wameendelea kuwatumikia watanzania kwa uaminifu mkubwa na kuhakikisha wanamtanguliza Mungu kwa kila jambo.

Amesema Serikali ya Awamu ya Tano katika kipindi cha miaka mitano maendeleo makubwa yamefanyika nchini na kwamba katika usafiri wa anga Serikali ilimua kuimarisha miundombinu ya viwanja vya ndega ikiwa pamoja na kununua ndege mpya na iwapo atachaguliwa ataendelea kununua ndege nyingine mpya.

Kuhusu elimu Dk.Magufuli amesisitiza Serikali ya CCM kuendelea kutoa elimu bure kwa wanafunzi kuanzia elimu ya msingi hadi sekondari huku akizungumzia walivyojipanga kuendelea kuimarisha sekta ya afya, maji, miundombinu ya barabara na sekta nyingine kwa ajili ya maendeleo ya Watanzania wote.


APP YETU MPYA: Sasa unaweza kusoma kwa urahisi kupitia APP yetu. Download hapa kwa KUBOFYA HAPA

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini