MAGUFULI AWAOMBA WATANZANIA WAMPE MIAKA MITANO MINGINE | ZamotoHabari.

*Asema mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Tano yapimwe baada ya miaka 10
*Maelfu ya wananchi mkoani Shinyanga wamhakikishia ushindi wa kishindo

Na Said Mwishehe, Michuzi TV-Shinyanga

NIPENI baada ya miaka mitano!Ndivyo ambavyo Mgombea Urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dk.John Magufuli amewaambia Watanzania wakati akizungumza kwenye mkutano wa kampeni za uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba 28 mwaka huu.

Pia amesema kwa maendeleo ambayo Serikali ya Awamu ya Tano imefanya katika miaka mitano haoni sababu ya wananchi kutomchagua ili aendelee kuwatumikia wananchi kwa kuwaletea maendeleo , hivyo ni vema akapewa miaka mingine mitano.

Akizungumza mbele ya maelfu ya wananchi wa Mkoa wa Shinyanga leo Septemba 3,2020, Dk.Magufuli ametumia muda mwingi kuelezea kurasa kwa kurasa kuhusu miradi ya maendeleo itakayofanywa katika mkoa huo na kufafanua kuna maendeleo makubwa yamefanyika nchini.

"Tumefanya mambo makubwa katika nchi yetu na mkoa wa Shinyanga ukiwemo, hata hivyo huwezi kumaliza changamoto kwa siku moja, Baba wa Taifa Mwalim Nyerer amefanya kazi kubwa ya kuliunganisha Taifa letu na kuliletea maendeleo lakini hakumaliza changamoto, Mzee Ali Hassan Mwinyi ametatua aliyoweza mengine hakumaliza, Mzee Mkapa amefanya yake ametatua aliyoweza mengine hakumaliza, Mzee Kikwete naye amekuja ametatua aliyoweza.
 
"Nami nimekuja,msinipime kwa miaka mitano, mnipe kwa miaka 10.Tunafahamu nchi yetu ilikotoka iliko na inakokwenda , sote ni mashahidi tumefanya mambo mengi, tumetatua changamoto nyingine na tutaendelea kuzitatua.Nawaahidi mkinipa tena miaka mitano nitaleta maendeleo zaidi ya haya ambayo tumeyafanya sasa,"amesema Dk.Magufuli.

Akizungumzia maendeleo ambayo yamefanyika katika kipindi cha miaka mitano iliyopita Dk.Magufuli amefafanua hatua kwa hatua maendeleo yaliyopatiakana kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo na kwamba katika elimu serikali imeendelea kutoa elimu bure, imeimarisha sekta ya afya, kilimo, ufugaji, imeboresha sekta ya usafiri wa anga ambapo mbali na kuboresha viwanja vya ndege imenunua ndege 11 kwa fedha za Serikali na mkakati uliopo ni kununua ndege nyingine mpya tano.

"Tumefanya mambo mengi mengi sana katika kipindi cha miaka mitano, ndio maana tunaomba mtupe tena miaka mitano tukafanye kazi. Mwanza kule wanafahamu changamoto ya meli lakini sasa tumetengeza meli mpya.Watu zaidi ya 1000 walizama Ziwa Victoria na hatukuweza kununua hata boti.Tumetumia fedha zetu kuboresha usafiri wa meli.

"Nimekuwa Waziri wa Ujenzi kwa Mkapa na Kikwete(Marais wastaafu),nafahamu na nilijifunza matatizo ya watanzania wengi.Katika usafiri wa reli tumeendelea kuimarisha miundombinu ya reli na hivi sasa ujenzi wa reli kwa ajili ya treni inayotumia umeme unaendelea kutoka Dar es Salaam kwenda Morogoro , kisha Makotopola Mjini Dodoma.Pia treni hiyo ya umeme itakwenda Isaka mpaka Mwanza, hivyo Shinyanga itanufaika na reli hiyo ambayo inasafiri kilometa 160 kwa saa.

"Nchi yetu ndio yenye kilometa nyingi zaidi za treni ya umeme ukilinganisha na nchi jirani.Kufanya haya yote na maendeleo mengine mengi ambayo nimeyaeleza ni kujitoa sadaka, hakuna anayefurahi.Eneo hili la Tanzania  lina utajiri mkubwa, tumeibiwa sana.Katika sekta ya madini baada ya kujenga ukuta kule Mirerani na kudhibiti rasilimali za madini hata mapato yatokanayo na madini yetu yameongeza,"amesema Dk.Magufuli na kuongeza

"Nimesimama hapa nikujua ni kwa kiasi gani tumeibiwa, sitaki kudanganya wenzangu halafu nikaenda kuhukumiwa, nina waeleza ukweli, nchi yetu tunaweza, tumetoka kutambulika kuwa nchi ya uchumi wa kati kutoka nchi masikini.Nipeni miaka mitano nifanye haya ninayofanya, nataka nikitangulia mbele za haki nikaulizwa nikasema niliyofanya kwa ajili ya Watanzania. huenda nikawa hata nafanya kazi kwenye nyuma za Malaika,"amesema Dk.Magufuli.

Hata hivyo amehoji nani hajui Machinga walikuwa wanasumbuliwa, wakiweka mchicha tu wanafukuzwa, wapo wanawake wengi ambao walikuwa wakisumbulia wanapoamua kufanyabiashara lakini baada ya kuingia madarakani aliamua kuagiza Machinga wasisumbuliwe na ukawekwa utaratibu wa kulipa Sh.20,000 kwa ajili ya kufanya shughuli zao kwa mwaka mzima wakati awali walikuwa kwa mwezi wanalipishwa kati ya Sh.30000 hadi Sh.60,000.

Dk.Magufuli amesema baada ya kuanzisha utaratibu huo , wapo wanaosema kwamba kodi ya kichwa imerudishwa.Hata Marekani wanalipa kodi, hata Makanisani wanalipa fungu la 10...Yesu aliwahi  kusema ya Mungu mpe Mungu na ya Kaisari mpe Kaisari.Tuliamua kutoa elimu bure ambapo  tumetumia Sh.trilioni 1.09 kwa ajili ya elimu bure, hawa watoto masikini wangesoma lini.unakuta Mama alizaa mtoto na mwanaume akamkimbia na hampi matumizi.

"Unabaki na watoto huna  hela ya kusomesha, tukaamua watoto hawa wasome bure na uamuzi huo umesaidia hata idadi ya watoto kwa shule za msingi kuongeza kutoka watoto milioni moja hadi wanafunzi milioni 1.6. Hivi kusomesha watoto bure nimefanya makosa, mnataka mnitoe ili mumpe mtu mwingine.

"Kwa ndugu zetu Arusha na Moshi zaidi ya miaka 30 hajawahi kuona treni,.Ni treni iliyojengwa na Baba wa taifa imeachwa, usafirishaji ukanda ule wanatumia malori na magari, nikaa chini ya uongozi wenu nikasema lazima tuwaonee huruma watu.Moshi na Arusha sikupata kura nyingi lakini lazima utende haki, usilipe kisasi, tumepeleka treni mpaka Arusha na treni sasa itaanza kufanya kazi, kwa kutumia fedha zetu, kweli nimefanya vibaya?
 
"Tumeanza kupanua bandari zetu kuanzi ile ya Tanga ,Dar es Salaam na Mtwara.Zimetumika Sh.trilioni 1.2 kwa ajili ya kuboresha bandari zetu.Katika kipindi cha miaka mitano tumetawanya mitandao ya simu kila mahali, hii ni mipango mikubwa ambayo sisi Serikali tumepanga kuiteleza.Katika wote wanaozunguka sijamuona wa kunifikia hata kwa robo,amesema Dk.Magufuli.


APP YETU MPYA: Sasa unaweza kusoma kwa urahisi kupitia APP yetu. Download hapa kwa KUBOFYA HAPA

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini