DITOPILE AWAVUTA WANACHAMA 11 WA UPINZANI CCM, WAUNGA MKONO JUHUDI ZA DK MAGUFULI | ZamotoHabari.

 Charles James, Michuzi TV

Wanachama 11 wa vyama mbalimbali vya upinzani wilayani Chemba Dodoma wamevihama vyama vyao katika mkutano wa kampeni wa Mgombea Ubunge Viti Maalum Wanawake Mkoa wa Dodoma CCM, Mariam Ditopile na kuomba kujiunga CCM ikiwa ni kuunga mkono juhudi za Rais Magufuli.

Akizungumza katika mkutano uliofanyika Kata ya Mondo wilayani Chemba, Ditopile amewaomba wananchi wote wa kata hiyo kumpigia kura za kishindo mgombea Urais wa CCM, Dk John Magufuli, mgombea Ubunge Mohammed Monni na Diwani wa kata hiyo, Fred Sambala.

" Tunahitaji Rais mzalendo ambaye ni Magufuli, kwa miaka mitano hajasafiri kwenda Ulaya hata familia yake ikiumwa inatibiwa hapa hapa nchini, alisema haiwezekani familia yake itibiwe nje wakati watanzania wanyonge wanatibiwa hapa, na katika kuboresha sekta ya afya kajenga vituo 480 vya Afya, Hospitali 71 za Wilaya na Chemba ikiwemo.

Hawa wapinzani 11 walioomba kujiunga CCM hawajaja kwa bahati mbaya, ni kwa sababu Dk Magufuli ameleta maendeleo makubwa ikiwemo kuleta umeme hapa licha ya kata hii kuwa upinzani, hivyo niwaombe muirudishe CCM ili kazi iwe rahisi ya kuleta kituo cha afya, Mgombea Ubunge hapa Kunti ni mbinafsi na mbaguzi ameanza kutugawa kwa ukabila tukimpa ubunge hapa maana yake Warangi na Wamasai waliopo hapa hatowahudumia, tumuepuke.

Huko kwingine wananiita Yohana Mbatizaji kila napopita nawarudisha watu wao CCM na hapa nimewarudisha 11 na kila napochukua watu wao Kunti na viongozi wenzake wa Chadema wananipigia wanalalamika nachukua watu wao, sio nawachukua ni kwamba wameridhishwa na kazi kubwa ya Dk Magufuli, " Amesema Ditopile.

Kwa upande wake mgombea udiwani Sambala amewaomba wananchi wa kata hiyo kujitokeza kwa wingi kumpigia kura za kishindo mgombea Urais, Dk John Magufuli pamoja na Mgombea Ubunge, Monni ili washirikiane kuweza kuwaletea maendeleo.

Mgombea Ubunge Viti Maalum Wanawake Mkoa wa Dodoma CCM, Mariam Ditopile (kulia) akimnadi Mgombea Udiwani kata ya Mondo wilayani Chemba, Fredy Msambala katika mkutano wa kufunga kampeni uliofanyika katika viwanja vya Hospitali kwenye kata hiyo.
Mgeni rasmi katika mkutano wa kufunga kampeni kata ya Mondo wilayani Chemba, Mariam Ditopile akitoa elimu ya jinsi ya kupiga kura kwa wananchi wa kata hiyo.
Mgombea Ubunge wa Viti Maalum Wanawake Mkoa wa Dodoma CCM, Mariam Ditopile akizungumza na wananchi wa kata ya Mondo wilayani Chemba alipoenda kufunga kampeni za chama hicho katika kata hiyo.
Wananchi wa kata ya Mondo wilayani Chemba wakimsikiliza mgombea Ubunge wa Viti Maalum Wanawake Mkoa wa Dodoma, Mariam Ditopile wakati wa kufunga kampeni za CCM kata hiyo.
 


APP YETU MPYA: Sasa unaweza kusoma kwa urahisi kupitia APP yetu. Download hapa kwa KUBOFYA HAPA

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini