Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bi, Mary Maganga, akiwataka Wasimamizi wa Mali za Serikali kutoka mikoa 21 ya Tanzania Bara kuhakikisha wanafanya kazi kwa weledi ili kumshauri vema Mlipaji Mkuu wa Serikali katika eneo hilo la Mali za Serikali, jijini Dodoma.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bi, Mary Maganga (katikati) akipeana mkono na Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Usimamizi wa Mali za Umma Bw. Benedict Mgonya, baada ya kufungua kikao kazi cha Wasimamizi wa Mali za Serikali kutoka mikoa 21 ya Tanzania Bara, katika ukumbi wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) jijini Dodoma.
Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi wa Mali za Serikali Bw. Chotto Sendo, akiwataka Watumishi wa Idara hiyo kutoka mikoa mbalimbali nchini kuhakikisha wanachambua vema mali chakavu kabla ya kutoa Taarifa Wizara ya Fedha na Mipango ili kuziondoa, katika kikao kazi kilichofanyika ukumbi wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) jijini Dodoma
Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi wa Mali za Serikali Bw. Chotto Sendo (kushoto), na Msaidizi wake Bw. Benedict Mgonya pamoja na washiriki wa kikao kazi cha Wasimamizi wa mali za Umma, wakifuatilia kwa makini mada zilizokuwa zikiwasilishwa jijini Dodoma.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bi, Mary Maganga na Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi wa Mali za Serikali Bw. Chotto Sendo, wakizungumza jambo wakati wa kikao kazi cha Wasimamizi wa Mali za Umma kilichofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), jijini Dodoma
Baadhi ya Washiriki wa Kikao kazi cha Wasimamizi wa Mali za Umma kutoka Mikoa 21 ya Tanzania Bara wakiwa katika kikao cha kufanya tathimini ya utendaji wao na kuangalia maeneo ambayo yanaweza kuboreshwa ili utendaji wao uwe na tija kwa Taifa.
Meza kuu ikiongozwa na Naibu Katibu Mkuu wizara ya Fedha na Mipango, Bi. Mary Maganga (wa tatu kushoto, walioketi) wakiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa kikao kazi cha Wasimamizi wa Mali za Umma, kilichofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), jijini Dodoma
(Picha na Saidina Msangi, WFM, Dodoma)
************************************
Na. Saidina Msangi na Peter Haule, WFM, Dodoma
Serikali imeahidi kutatua changamoto ya uhaba wa Wasimamizi wa Mali za Serikali kutokana na umuhimu wao katika kuisaidia Serikali kusimamia mali zake ambazo ni nyingi.
Hayo yamebainishwa jijini Dodoma na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bi. Mary Maganga, wakati akifungua Kikao kazi cha Wasimamizi wa Mali za Serikali kutoka Mikoa 21 ya Tanzania Bara, kilicholenga kutathimini kazi za Idara hiyo na maeneo yanayotakiwa kuboreshwa.
Bi. Maganga alisema suala la upungufu wa watumishi wa Idara hiyo limechukuliwa kwa uzito na Serikali hivyo katika maeneo ambayo yanaupungufu mkubwa wa nguvu kazi wataanza kuona watumishi wakiongezeka kwa kuwa hatua za dhati zimeanza kuchukuliwa.
Amesema kuwa Miongozo iliyotolewa na Idara ya Usimamizi wa Mali za Serikali ikiwa ni pamoja na Mfumo wa Kutunza Kumbukumbu za Mali za Serikali (GAMIS) itasaidia kurahisisha utendaji kazi na kuongeza ufanisi wenye tija katika kujua na kudhibiti mali za Serikali katika maeneo yote nchini.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi wa Mali za Serikali Bw. Chotto Sendo alisema kuwa Wasimamizi wa Mali za Serikali katika Mikoa yote wanatakiwa kusimamia na kutoa tathmini nzuri kwa Mali za Serikali zinazofutwa kwa kujiridhisha juu ya uchakavu wake kabla ya kuiarifu Wizara kwa ajili ya maamuzi.
Alisema kuwa Idara yake inajukumu la kubuni Sera, kanuni, taratibu na miongozo ya kusimamia mali za Serikali, kutoa Leseni za Udalali, Kusimamia vifaa vya kutunzia mali (Kasiki) pamoja na ufuatiliaji wa mali chakavu ambazo huondolewa kulingana na Sheria na kanuni zilizopo.
Bw. Sendo alisema kuwa Idara yake ina umuhimu mkubwa kwa Wakuu wa Mikoa kuwa na uhakika wa mali wanazozimiliki, hivyo kuwasaidia katika maamuzi mbalimbali ya kiuongozi katika eneo lao la utawala.
Aliwapongeza watumishi walioshiriki kikao kazi hicho kwa kuwa kina lengo la kupashana habari lakini pia kufahamiana, kupeana miongozo mbalimbali ya majukumu na kujua wajibu wao katika utekelezaji wa majukumu yao.
Kikao kazi hicho cha siku mbili kimewashirikisha watumishi 88 kutoka mikoa 21 ya Tanzania bara wakiwemo Wahakiki Mali na Mafundi Kamonga.
APP YETU MPYA: Sasa unaweza kusoma kwa urahisi kupitia APP yetu. Download hapa kwa
KUBOFYA HAPA
0 Comments