KATIBU MKUU CCM ASEMA WAMEZINDUA AWAMU YA TANO YA KAMPENI, AMPONGEZA DK. MAGFULI | ZamotoHabari.



KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi(CCM)Dk.Bashiru Ally



Na Said Mwishehe, Michuzi TV

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi(CCM)Dk.Bashiru Ally amesema leo Oktoba 9, mwaka huu wa 2020 wamezindua awamu ya tano ya kampeni za mgombea wao wa urais Dk.John Magufuli huku akitumia nafasi hiyo kumpongeza kwa kazi kubwa anayofanya ya kuomba kura tangu walipozindua rasmi kampeni zao Agosti 29 jijini Dodoma.

Dk.Bashiru ameyasema hayo leo Oktoba 9,2020 mbele ya maelfu ya wananchi wa Jiji la Dar es Salaam wakati wa mkutano wa kampeni za mgombea urais kwa tiketi ya Chama hicho Dk.Magufuli, ambapo ametumia nafasi hiyo kuelezea mwenendo wa kampeni za mgombea wao.

"Tunakupongeza kwasababu tangu ulipozindua kampeni umefanya kazi hiyo kwa uungwana, umakini na kwa kasi inayoridhisha.Nampongeza Makamu wa Rais mama Samia Suluhu Hassan pamoja na mjumbe wa Halmashauri Kuu Kassim Majaliwa kwa kazi wanayoendelea kuifanya ya kuomba kura.

"Leo unazindua awamu ya tano kampeni na kuanzia Oktoba 15 tutazindua awamu ya sita na ya lala salama za kampeni zetu, tangu ulivyotoka Zanzibar na kuingia Dar es Salaam, leo unaanza kufanya kampeni katika jiji hili, leo ni mkutano wa kwanza kwa majimbo matatu ya Temeke, Mbaala na Kigamboni, "amesema.

Amefafanua mkutano wa pili wa kampeni za mgombea urais wa CCM zitafanyika Kinyerezi kwa ajili ya majimbo ya Ilala, Segerea na Ukonga.Mkutano wa tatu utafanyika Uwanja wa Uwanja wa Barafu kwa ajili ya majimbo ya Ubungo na Kibamba wakati mkutano wa mwisho utafanyika Kawe katika Uwanja wa Tanganyika Packers.

"Umefanya hivyo kwa ukubwa wa Dar es Salaam na wakati huo huo kuwafikia wapiga kura wengi.Tunakwenda kwa mtindo wa bandika bandua, na tumekubaliana kuzingatia yale ambayo tumekubaliana katika vikao vya Chama,

"Kwanza misingi ya uhuru wetu na misingi ya Taifa letu isilegelege ,tunakupongeza kwa kufanikisha hilo , ndio maana hata wakati wa kampeni umefanya kampeni za kistaraabu, umeendelea kupokea wageni mbalimbali.

"Hata marais wa nchi jirani wameridhishwa na namna ambavyo kampeni zinaendeshwa, na hiyo ndio sifa pekee ya Watanzania na ndio silaha ya maendeleo,"amesema Dk.Bashiru.

Ameongeza katika kipindi hiki ambacho kampeni zinakwenda mwishoni ni vema amani ikaendelea kulindwa, na kwa Dar es Salaam ndiko nchi yetu imekabidhiwa uhuru wake na kwamba Ilani ya CCM imeweka mkazo wa kulifanya Jiji hilo kuwa la kibiashara.

Pia ameahidi siku zilizobakia wataendelea kunadi wagombea wao na wala hawatasababisha hofu kwa wananchi."Tutapokea ushindi kwa amani na kuanza kuchapa kazi kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu."

Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam Keti Kamba amesema wananchi wa Jiji hilo ndio wamenufaika zaidi kuliko mikoa mingine yote nchini katika kipindi hiki cha uongozi wa Rais Magufuli."Umefanya mambo makubwa na ndio maana watu wamekuja wengi kukushuru na kukutia moyo na oktoba 28 hawatakosea, kura zote kwa Dk.Magufuli.

APP YETU MPYA: Sasa unaweza kusoma kwa urahisi kupitia APP yetu. Download hapa kwa KUBOFYA HAPA

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini