MVULANA wa miaka 17 katika Kaunti ya Tana River, nchini Kenya ametorosha mahari iliyokusudiwa kutumiwa na baba’ke kuoa mke wa nne, ambaye alikuwa ni mchumba wake.
Mvulana huyo ambaye alirejea nyumbani wiki iliyopita baada ya ushawishi kutoka kwa vijana waliotumwa kumtafuta kichakani, alitorosha ng’ombe waliokuwa watumiwe kulipia mahari hiyo bya baba yake.
Akisimulia mkasa huo kijana huyo alisema alichukua hatua hiyo baada ya juhudi zake za kushawishi wazee kusimamisha baba’ke asioe mchumba wake kugonga mwamba.
Kwa mujibu wa Mzee Hussein Barisa, ambaye aliongoza mchakato wa upatanishi, kijana huyo aliwaeleza kuwa bi harusi tayari ana mimba yake ya miezi mitatu.
“Msichana alikuwa aozwe kwa mzee huyo ili kuiepusha familia yake aibu baada ya wazazi kugundua alikuwa mjamzito nje ya ndoa na hakutaka kumtaja aliyehusika,” alisema Barisa.
“Baada ya kijana kufichua kuhusu uhusiano wake na bi harusi, tulizungumza na babake na tukamwelezea kwamba kweli mwanamke huyo alikuwa na ujauzito wa mtoto wake na alishtuka sana,” alisema.
Kijana naye alisema waliamua kupata ujauzito na mchumba’ke kama njia ya kumshawishi babake akubali waoane, akidai babake alikuwa na tabia ya kukataa wachumba wake wote. Sasa mzee huyo wa miaka 74 amekubali kupatana na mwanawe.
Aidha, Mzee huyo alisema mtoto wake hakumuarifu kuhusu uhusiano wao na hata kuhusu ujauzito.
Alijitetea kuwa hamu yake ya kumuoa msichana huyo ilikuwa katika juhudi za kuiondolea familia yake aibu, jambo alilosema linakubalika kitamaduni.
Baada ya kupatana, mzee huyo amemzawadia mwanawe mahari ya ng’ombe 17 aliotoroka nao awali, na ameahidi kumsaidia yeye na mchumba wake kuoana.
Wawili hao watashiriki katika sherehe ya uchumba kitamaduni mwezi ujao, sherehe itakayoongozwa na wazazi wa pande mbili, kabla ya harusi mwaka ujao.
APP YETU MPYA: Sasa unaweza kusoma kwa urahisi kupitia APP yetu. Download hapa kwa KUBOFYA HAPA
0 Comments