Mgombea ubunge Jimbo la Hanang’ Mkoani Manyara, kwa tiketi ya CCM, mhandisi Samwel Hhayuma akizungumza na wananchi wa Kata ya Masakta wakati akiomba kura zake, za mgombea urais wa CCM Dkt John Magufuli na mgombea udiwani Marko Kia.
Mgombea ubunge Jimbo la Hanang’ Mkoani Manyara, kwa tiketi ya CCM, mhandisi Samwel Hhayuma akizungumza na wananchi wa Kata ya Ganana wakati akiomba kura zake, za mgombea urais wa CCM Dkt John Magufuli na mgombea udiwani Isaya Mbise.
Mbunge mstaafu wa Jimbo la Hanang’ Mkoani Manyara, Dk Mary Nagu katikati akiwa na mgombea ubunge Jimbo la Hanang’, mhandisi Samwel Hhayuma alipofika kuzungumza na wananchi wa Kata ya Masakta wakati akiomba kura za mgombea urais wa CCM Dkt John Magufuli, ubunge mhandisi Hhayuma na mgombea udiwani Marko Kia, kulia.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Hanang’ Mkoani Manyara, Mathew Darema (kushoto) akimnadi mgombea ubunge wa Jimbo la Hanang’ mhandisi Samwel Hhayuma.
Wakereketwa wa CCM wa Kata ya Endasak Wilayani Hanang’ Mkoani Manyara, wakimpokea mgombea ubunge wa Jimbo hilo mhandisi Samwel Hhayuma alipofika kwa ajili ya kufanya mkutano wa kampeni.
……………………………………………………………………………………..
Na Mwandishi wetu, Manyara
Mhandisi Samwel Hhayuma “Kwa kutumia rasilimali zilizopo hapa Hanang’ tutahakikisha zinatumika ipasavyo katika kunyanyua uchumi wa mtu mmoja mmoja na jamii kwa ujumla,” hivi ndivyo mgombea ubunge wa Jimbo la Hanang’ Mkoani Manyara, mhandisi Samwel Hhayuma anavyoanza kuelezea mikakati yake pindi akichaguliwa kuwa mbunge.
Mhandisi Hhayuma ambaye amewahi kufanya kazi sehemu mbalimbali nchini hadi nje ya nchi ikiwemo Afrika kusini, amerejea nyumbani kwao Hanang’ kwa lengo la kuwatumikia wananchi baada ya kuombwa kufanya hivyo.
Historia yake kwa ufupi
Mgombea ubunge wa Jimbo la Hanang’ kwa tiketi ya CCM, mhandisi Samwel Hhayuma alizaliwa Novemba 26 mwaka 1975 kwenye kijiji cha Bassotughang wilayani Hanang Mkoani Manyara.
Mhandisi Hhayuma alisoma shule ya msingi Bassotughang kuanzia darasa la kwanza mwaka 1985 hadi la saba mwaka 1991.
Alisoma shule ya sekondari Tanga Technical kuanzia kidato cha kwanza mwaka 1992 hadi kidato cha nne mwaka 1995.
Vyuo vikuu alisoma Dar es salaam Institute of Technology, University of Cape Town AfriKa Kusini, Korea na Burkina Faso.
Vipaumbele vyake
Hhayuma anasema akichaguliwa kushika nafasi hiyo pamoja na mambo mengine kipaumbele chake cha kwanza atahakikisha anafanikisha uchumi kwa jamii kupitia viwanda kutokana na rasilimali zilizopo eneo hilo.
Anasema kupitia mazao ya ngano, mahindi na alizeti, viwanda vya nafaka vitaanzishwa ili kuongeza thamani mazao hayo tofauti na kuyauza yakiwa ghafi kwani yanauzwa kwa bei ndogo hivyo mkulima kupunjwa.
“Ardhi ya Hanang’ ina rutuba nzuri hivyo tunataka kupitia mazao hayo watu wanunue unga siyo mahindi, wanunue unga wa ngano, kuliko ilivyo hivi sasa ili kuongeza thamani mazao yetu na jamii kunyanyuka kiuchumi,” anasema Hhayuma.
Anasema kwenye kata ya Gendabi kuna madini ya chumvi napo kunapaswa kuwekwa kiwanda cha chumvi ili watu wakinunua chumvi iwe imefungwa kitaalamu na siyo kuwekwa kienyeji.
Anasema kwenye kata ya Mogitu kuna mawe yanayotengenezea saruji hivyo watahakikisha kiwanda kinajengwa ili wananchi wanunue saruji iliyozalishwa Hanang’ na siyo sehemu nyingine.
“Pia tunapaswa kuweka kiwanda cha kuchakata mazao ya mifugo ikiwemo nyama na ngozi ili kwa namna moja au nyingine tunyanyue uchumi wa wafugaji kupitia benki ya jamii na kuboresha machinjio, majosho na chanjo za mifugo,” anasema Hhayuma.
Anasema endapo uwekezaji wa viwanda ukifanyika ajira za vijana zitakuwepo na uchumi utabaki mifukoni mwa wananchi wa Hanang kupitia sekta mbalimbali.
“Kupitia marafiki watafanikisha mikopo isiyoumiza kwa wananchi wa Hanang’ kuchangamkia fursa hiyo tofauti na hivi sasa baadhi ya taasisi za fedha zinawatapeli watu,” anasema mhandisi Hhayuma.
Anasema ataboresha suala la afya kwa kuibana serikali itekeleze sera ya afya ya kuwepo zahanati kila kijiji na kituo cha afya kila kata.
Anasema kwenye sekta ya michezo atahakikisha ajira zinapatikana kwa vijana kupitia riadha, soka, burudani na sanaa, kwani vijana wanapaswa kuchangamkia nafasi hiyo na siyo kuangalia hayo kwenye vibanda umiza.
“Tunapaswa tuibue vipaji vipya vya riadha Hanang irudi kwenye enzi zake kama kina mheshimiwa Gidamis Shahanga wengine, mimi niliwahi kushiriki mita 400 nikawa wanne, tutajitahidi kuboresha michezo,” anasema mhandisi Hhayuma.
Anasema atahakikisha anaanzisha baraza la ardhi na nyumba Wilaya Wilaya ya Hanang’ ili wananchi wenye migogoro waweze kuitatua tofauti karibu tofauti na sasa hadi waende mjini Babati.
Anasema kuna changamoto ya ubovu wa miundombinu barabara hasa nyakati za mvua hivyo bei ya usafiri kupanda, hivyo atahakikisha zinatengenezwa.
Mama Samia amuombea kura mhandisi Hhayuma
Hivi karibuni mgombea mwenza wa urais kupitia CCM mama Samia Suluhu Hassan alifika wilayani Hanang’ kufanya kampeni ya kuomba kura kwa mgombea urais John Magufuli, mgombea ubunge mhandisi Hhayuna na madiwani wa CCM, fursa iliyomwezesha mhandisi Hhayuma kuwasilisha changamoto zinazoikabili jimbo hilo.
Mhandisi Hhayuma akataja baadhi ya changamoto zinazowakabili wananchi wa jimbo hilo ni ubovu wa miundombu ya barabara, maji na nishati ya umeme vijijini.
Anasema wanaomba kujengewa kilomita 10 ya barabara ya lami kwenye mji mdogo wa Katesh na lami kutoka kata ya Mogitu hadi hospitali ya kilutheri ya Haydom wilayani Mbulu.
Anasema changamoto za maji zinawakabili wananchi wa vijiji mbalimbali ikiwemo mradi wa maji wa thamani ya sh. bilioni 2 wa kutoka kata ya Mogitu hadi mji mdogo wa Katesh.
“Pia kuna changamoto ya nishati ya umeme kwani ni asilimia 75 pekee ya vijiji vya jimbo la Hanang’ ndiyo kuna umeme bado asilimia 25 ya vijiji ambavyo havina umeme,” anasema mhandisi Hhayuma.
Hata hivyo, mgombea mwenza huyo Samia anasema kupitia ilani ya uchaguzi wa CCM changamoto nyingi zilizotajwa na mhandisi Hhayuma zitapatiwa ufumbuzi kwa kutekelezwa kwa mwaka 2020/2025.
Anasema miradi ya maji itakamilishwa, umeme utafika vijiji vyote na barabara ya lami ya Mogitu hadi Haydom itajengwa kwani ipo kwenye ilani ya uchaguzi kwa mwaka 2020/2025.
“Ili kukamilisha hayo tunaomba muichague CCM kwa kumpa kura nyingi Rais John Magufuli, mhandisi Hhayuma achaguliwe kwenye ubunge na madiwani wanaotokana na CCM,” anasema mama Samia.
Waziri mkuu mstaafu wa awamu ya tatu, Fredrick Sumaye anasema mhandisi Hhayuma ni kijana msomi ambaye anaweza hata kuchaguliwa kuwa Waziri pindi akichaguliwa kuwa mbunge na Rais Magufuli atakaposhinda tena.
Sumaye anasema wananchi wa Hanang’ wasipotoshwe na wapinzani na kupoteza kura zao kwani muda wa siasa umeshapita kimachotakiwa hivi sasa ni maendeleo pekee.
Mbunge wa jimbo hilo wa kipindi kilichopita, Dk Mary Nagu anasema mradi wa maji wa Mogitu hadi Katesh wa gharama ya sh. bilioni 2 umechukua muda mrefu bila kukamilika.
“Maji ni uhai na inabidi mradi huu uelekezewe nguvu zaidi ili uweze kukamilika na wananchi wa eneo hili la Katesh wapate maji ya uhakika,” anasema Dk Nagu.
Mshindi wa kura za maoni ya chama hicho aliyechaguliwa na wajumbe, George Bajuta anasema wanaoeleza kuwa amenuna baada ya jina lake kukatwa na kushindwa kugombea ubunge ni waongo kwani anaunga mkono uamuzi wa kamati kuu ya CCM kwa asilimia 100.
“Baba yako akiamua mtoto mwingine akachunge ng’ombe hupaswi kulalamika kazi zipo nyingi huenda nikatumwa kuuza duka au nikapewa kazi nyingine,” anasema Bajuta.
Wilaya ya Hanang’ yenye tarafa tano na kata 33 ina miaka 35 tangu ianzishwe baada ya kumegwa kutoka wilaya ya Babati.
Kwa mujibu wa sensa ya watu ya mwaka 2012 Wilaya hiyo ina watu 275,990 na makisio ya sasa ni watu 385,068.
Vyama vinavyogombea nafasi ya ubunge kwenye jimbo la Hanang’ ni CCM, ACT-Wazalendo na Chadema.
APP YETU MPYA: Sasa unaweza kusoma kwa urahisi kupitia APP yetu. Download hapa kwa
KUBOFYA HAPA
0 Comments