Charles James, Michuzi TV
ZOEZI la kuhakikisha Mkoa wa Dodoma unaongoza kwa kura za Mgombea Urais wa CCM, Dk John Magufuli limeendelea leo kwa Mgombea Ubunge Jimbo la Chamwino, Deo Ndejembi na Mgombea Ubunge Viti Maalum Wanawake Mkoa wa Dodoma CCM, Mariam Ditopile kuomba kura katika Kata ya Msamalo wilayani Chamwino.
Wagombea hao wa Ubunge wamefanya mikutano miwili ndani ya kata hiyo ambapo mmoja wamefanya katika kitongoji cha Mgondo na Ifunda na mwingine wamefanya katika kijiji cha Mgunda ambapo wamemuombea kura Dk Magufuli, Ndejembi mwenyewe huku wakiwashukuru wananchi kwa kumpitisha, Elias Kaweya kuwa Diwani bila kupingwa.
Akizungumza katika mikutano hiyo, Ndejembi amewaomba wananchi wa kata hiyo kumchagua yeye na Dk Magufuli kwa kura nyingi za kishindo ili waweze kuwatumikia na kuwaletea maendeleo kwa kasi kubwa.
" Ni lazima tumlipe Dk Magufuli upendo ambao ameuonesha kwa kuhamishia serikali Dodoma lakini zaidi yeye mwenyewe kuhamia Ikulu ya Chamwino, kitendo cha yeye binafsi kuhamia jimboni kwetu ni faida kubwa sana za kimaendeleo kwa sababu sasa hili haliwi tu jimbo la Chamwino bali makazi ya Rais, niombeni mjitokeze kwa wingi Oktoba 28 mkamchague awe mtumishi wetu wa kushughulika na kero zetu za Maji, Elimu, Barabara na Afya.
Mimi ni kijana wetu mnanifahamu, 2015 nilikuja hapa kura hazikutosha, mwaka huu Chama kimeniamini kikanipa ridhaa, kama ambavyo nimekua nanyi kwa miaka mitano nikiwa siyo Mbunge na nimeweza kushughulika na changamoto zenu ikiwemo kuwezesha kupatikana Milioni 60 za Ujenzi wa Sekondari ya Msamalo basi aminini nikiwa mbunge nitafanya zaidi ya hayo," Ndejembi.
Kwa upande Mgombea Ubunge Viti Maalum Wanawake, Mariam Ditopile amesema miaka mitano ya Dk Magufuli imekua ya neeema kwa wananchi wa Chamwino na watanzania kwa ujumla na hivyo kuwaomba wamchague tena yeye na Ndejembi ili kwa pamoja washirikiane kusukuma maendeleo katika jimbo hilo ili liendane na hadhi ya Ikulu.
" Kwa ngazi ya Urais kinachoendelea sasa ni mashindano ya kila Wilaya kutaka kuongoza kwa kura za Rais Magufuli, Wilaya ya Chamwino ndio anapoishi Rais wetu itakua jambo la ajabu kama hatutompigia kura za kishindo Rais ambaye ametuletea Hospitali ya Uhuru yenye hadhi ya kisasa katika Wilaya yetu ili imalize adha yetu ya kusafiri kwenda Dodoma Mjini.
Katika vijiji ambavyo vimenufika na serikali ya Magufuli kwenye umeme ni nyie watu wa Mgunga na Kata ya Msamalo, niwaombe sasa mna Mbunge kijana mwenye nguvu na akili, mwenye connection ambaye ataweza kuwaharakishia maendeleo, mnalopaswa nyie kufanya ni kumpa kura nyingi yeye na Dk Magufuli Oktoba 28," Amesema Ditopile.
Nae Diwani mteule wa kata hiyo, Elias Kaweya amewashukuru wananchi wa kata hiyo kwa imani kubwa waliyompatia ya kumpitisha bila kupinga huku akiahidi kufanya kazi kwa bidii, uadilifu na kushirikiana na mbunge wake katika kuwatumikia wananchi wa Msamalo.
Muonekano wa wananchi wa Kijiji cha Mgunga Kata ya Msamalo wilayani Chamwino ambao wamejitokeza kumsikiliza mgombea wao wa Ubunge Chama cha Mapinduzi CCM, Deo Ndejembi ambaye aliambatana na Mgombea wa Viti Maalum Wanawake, Mariam Ditopile kwenda kuomba kura za Chama hicho.
Mgombea Ubunge Viti Maalum Wanawake Mkoa wa Dodoma CCM, Mariam Ditopile akizungumza na wananchi wa Kata ya Msamalo wilayani Chamwino alipoenda kuomba kura za Chama hicho kuelekea Uchaguzi mkuu Oktoba 28 mwaka huu.
Wananchi wa Kata ya Msamalo wakimshangilia Mgombea Ubunge wa Jimbo la Chamwino CCM, Deo Ndejembi alipofanya mkutano wa kampeni wa kuomba kura kwenye kata hiyo.
Mgombea Ubunge wa Jimbo la Chamwino CCM, Deo Ndejembi (kulia) akiwa na Mgombea Ubunge Viti Maalum Wanawake Mkoa wa Dodoma CCM, Mariam Ditopile katika mkutano wa kampeni Kata ya Msamalo wilayani Chamwino.
APP YETU MPYA: Sasa unaweza kusoma kwa urahisi kupitia APP yetu. Download hapa kwa KUBOFYA HAPA
0 Comments