Na Mwandishi Wetu
WANAFUNZI wa Shule ya Msingi Hazina wametia fora kwa kuongoza kwenye usaili wa kujiunga na kidato cha kwanza kwenye shule maarufu nchini.
Mkuu wa shule hiyo, Omari Juma amesema, wanafunzi wengi wa shule hiyo waliokwenda kufanya usaili katika shule mbali mbali zenye majina makubwa wamefanikiwa kuongoza na kupata nafasi za kujiunga kidato cha kwanza.
"Mfano mwanafunzi aliyeongoza kwenye usaili kwenye shule maarufu ya Feza Boys, Harris Edward ametoka hapa shuleni kwetu Hazina na wanafunzi wa shule hiii wamekuwa wakiongoza kila mwaka kwenye usaili katika shule mbali mbali. Amesema Mwalimu Mkuu Juma.
Amesema katika usaili wa mwaka huu wanafunzi sita wa Hazina wamefanikiwa kufanya vizuri zaidi kwenye usaili na kujiunga na shule za Marian zilizoko Bagamoyo Mkoa wa Pwani huku wanafunzi wengine wakiwa wamefanikiwa kufanya vizuri zaidi na kujiunga na shule za Feza wakati wanafunzi wengine tisa wamefanya vizuri na kujiunga na shule ya wavulana ya Shamsiye.
“Mwaka 2019 tulipeleka wanafunzi wengi sana kwenye shule hizo na waliongoza na wazazi wengi wanapenda sana watoto wakimaliza shule ya msingi wakasome shule nzuri ndiyo sababu wanapenda kuwaleta hapa Hazina,” alisema
Mzazi ambaye mtoto wake ameongoza kwenye usaili shule ya Feza, Neema Mwaisunga ameelezea kufurahishwa kwake na matokeo hayo na kufanikiwa kupata udahili kwani wanafunzi walikuwa wengi kupita kawaida.
“Wanafunzi wanaofanya udahili wanafikia 6,000 nafasi zilizopo ni 100 hivyo kupata nafasi pale ni ushahidi kwamba hapa Hazina wanafunzi wanaandaliwa vizuri sana,” alisema
Pia amefurahi kuona mtoto wake amepata shule ambayo ilikuwa ndoto yake na amewashukuru walimu na wafanyakazi wa shule ya Hazina kwa namna walivyowaandaa wanafunzi wa shule hiyo.
“Kwa kweli shule ya Hazina imekuwa ikifanya vizuri kwenye mitihani ya kitaifa na wamewaandaa vyema wanafunzi na kushinda kwenye usaili kwenye shule hizi zenye majina makubwa ni ushahidi wa namna Hazina ilivyo shule bora nawashukuru na kuwapongeza sana,” alisema.
Mwalimu Mkuu wa shule ya Msingi Hazina ya jijini Dar es Salaam, Omari Juma akimpa zawadi mwanafunzi aliyemaliza darasa la saba katika shule hiyo Harris Edward aliyeshika namba moja kwenye usaili wa kujiunga na shule ya Feza Boys ya jijini Dar es Salaam.APP YETU MPYA: Sasa unaweza kusoma kwa urahisi kupitia APP yetu. Download hapa kwa KUBOFYA HAPA
0 Comments