OFISI ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, imetoa ruhusa ya siku tatu kwa watumishi wa umma ambao vituo vyao vya kazi vipo sehemu tofauti na maeneo walikojiandikisha kupiga kura kwenda kupiga ili kutimiza haki yao ya kikatiba.
Taarifa ilitolewa mwishoni mwa wiki na Katibu Mkuu Utumishi, Dk Laurean Ndumbaro kwenda kwa viongozi wa taasisi, wizara, halmashauri, Idara zinazojitegemea mashirika, wakurugenzi na watendaji wengine imeagiza watumishi wapewe ruhusa.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo ruhusa inaanza leo hadi Oktoba 29 mwaka huu.
“Napenda kuwataarifu kuwa serikali imebaini uwepo wa watumishi waliojiandikisha kupiga kura kwenye maeneo tofauti na vituo vyao vya kazi kwa sasa, ili kuwawezesha kutumia haki yao ya kikatiba ya kupiga kura Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 28 mwaka huu, ninaelekeza kuwaruhusu kusafiri kwenda kupiga kura katika vituo walivyojiandikisha. Ruhusa itolewe kuanzia Oktoba 27 hadi 29 mwaka huu” ilieleza taarifa hiyo ya Dk Ndumbaro.
Hivi karibuni Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), ilitangaza kuwa katika Uchaguzi Mkuu unaofanyika kesho kutakuwa na jumla ya vituo 80,155 vya kupigia kura na kwamba katika kila kituo kitakuwa na wapiga kura wasiozidi 500.
Katika hatua nyingine, NEC imeruhusu pia wapiga kura waliojiandikisha na majina yao yapo kwenye daftari la kudumu la wapiga kura, na wamepoteza vitambulisho vya kupigia kura wapige kura kwa kutumia leseni ya udereva, kitambulisho cha taifa au hati ya kusafiria.
APP YETU MPYA: Sasa unaweza kusoma kwa urahisi kupitia APP yetu. Download hapa kwa KUBOFYA HAPA
0 Comments