Klabu ya Klabu ya Al Ahl ya Misri, imefanikiwa kubeba ubingwa wa michuano ya klabu bingwa barani Afrika kwa kuwafunga watani wao wa jadi klabu ya Zamalek pia ya nchini Misri kwa kuwafunga mabao 2-1, mchezo uliochezwa usiku wa kuamkia hii leo kwenye dimba la Cairo Internationa nchini Misri.
Al Ahly ndiyo waliokuwa wa kwanza kupata bao dakika ya 5 kupitia kwa winga wake Amr Eli Solia, aliyeunganisha mpira wa kona uliopigwa na Al Maaloul, na kumshinda mlinda mlango wa Zamalek Abou Gabal, na kutinga wavuni.
Dakika 26 baadaye Zamalek ambaye alifanikiwa kuutawala mchezo kwa kuwa na umiliki mkubwa wa mpira alifanikiwa kupata bao kupitia kwa mshambuliaji na nahodha Mahmoud Fadlala 'Shikabala', aliyetumia uwezo binafsi kuwapunguza walinzi wa Al Ahly na kuachia shuti kali na kutinga wavuni.
Almanusra Zamalek wapate penalti dakika ya 74 baada ya mchezaji wao Achraf Benchaki, kufanyiwa madhambi ndani ya eneo la 18 na mlinzi wa kushoto wa Al Ahly Ahmed Al Maaloul, lakini mwamuzi wa mchezo huo Mustapha Ghorbal, kutoka Algeria hakufanya maamuzi ya kuweka penalti .
Mohamed Magdy 'Afsha', ndiye aliyeibuka shujaa na nyota wa mchezo baada ya kufunga bao la ushindi kwa timu yake ya Al Ahly dakika 4 kabla mchezo kumalizika kwa shuti kali lililomshangaza mlinda mlango Gabal na kujaa wavuni.
Huu ni ubingwa wa tisa kwa Al Ahly, ambao unamfanya kuwa klabu pekee kutwaa taji hilo mara nyingi zaidi kihistoria na kuwaacha Zamalek wakiwa na mataji hayo mara tano pekee. Ubingwa huu pia ni wa kwanza kwa Al Ahly tokea mwaka 2013.
Kocha wa Al Ahly Pitso Mosimane, raia wa Afrika Kusini ameweka rekodi ya kuwa kocha watatu kutwaa taji hilo mara mbili akiwa na timu mbili tofauti baada ya kutwaa mara ya mwisho mwaka 2016 akifunga Zamalek yeye akiwa kocha wa Mamelod Sundowns ya Afrika Kusini.
Makocha wengine wawili waliowahi kufanya hivyo ni pamoja na Mohmed El Gohary, mwaka 1982 akiwa na Al Ahly, mwaka 1993 akiwa na Zamalek zote za Misri na Muargentina Oscar Fullone mwaka 1998 akiwa na Asec Mimosas ya Ivory Coast na 1999 akiwa na Raja Casablanca ya Morocco.
Ahly wameweka rekodi ya kuwafunga wapinzani wao wa jadi Zamalek mara 6 na kutoa sare 3 wakiwa hawajafungwa hata mchezo mmoja na Zamalek, kwenye michuano hii ya klabu bingwa barani Afrika. Hata ujio wa kocha Jaime Pacheco wa Zamalek kutoka Ureno umeshindwa kumsimamisha Ah Ahly.
Baada ya kubeba ubingwa huo, sasa Al Ahly anatazamiwa kupokea kiasi cha dola za kimarekani milioni moja ambazo ni sawa na zaidi ya Bilioni mbili na milioni mia tatu kumi na tisa kama zawadi ya mshindi wa kwanza na dola za kimarekani laki saba na hamsini kwa mshindi wa pili Zamalek.
Zawadi ya dola za kimarekani laki saba na hamsini kwa mshindi wa pili Zamalek ni sawa na zaidi ya bilioni moja na milioni mia saba thelathini na tisa.
Al Ahly amekata tiketi ya kucheza michuano ya kombe la dunia la vilabu mwezi februari mwaka 2021.
APP YETU MPYA: Sasa unaweza kusoma kwa urahisi kupitia APP yetu. Download hapa kwa KUBOFYA HAPA
0 Comments