Simba Kutuma Mashushushu Nigeria Wiki Ijayo | ZamotoHabari.



UONGOZI wa Klabu ya Simba upo katika mchakato wa kuwatuma watangulizi kwa ajili ya kuwachunguza wapinzani wao nchini Nigeria, Plateau FC wanaotarajia kukutana nao katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.


Simba inatarajia kuwakilisha nchi katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kuanza michuano hiyo dhidi ya Plateau FC ya Nigeria ambapo mechi ya kwanza itakuwa kati ya Novemba 27 na 29 ugenini, kisha mchezo wa marudiano utachezwa kati ya Desemba 4-6, mwaka huu.

Akizungumza na Championi Ijumaa, Katibu wa Simba, Dk Arnold Kashembe, amefunguka kuwa, kuna mchakato ambao unaandaliwa kwa ajili ya kuwatuma watu ambao watatangulia kwa ajili ya kuangalia mazingira kabla ya kikosi kwenda nchini humo.

“Ratiba ya klabu bingwa imepangwa na kila mtu ameiona, hivyo kama uongozi kuna mipango ambayo tunaiandaa kuelekea katika michuano hiyo, wiki ijayo kuna watu watatumwa kwenda nchini Nigeria kuandaa mazingira jinsi timu itakapofikia na masuala mengine ya uwanjani mwenye jukumu ni kocha.

“Mipango yote kuelekea mchezo huo ipo vizuri lakini siwezi kuwataja ni akina nani watakwenda na ni lini, ila kila kitu kipo vizuri, lengo ni kuona tunapata matokeo mazuri katika mchezo huo,” alisema Kashembe.

Msimu uliopita Simba ambayo ilipata nafasi ya kuiwakilisha nchi katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, iliishia hatua ya awali ya michuano hiyo baada ya kutolewa na UD Songo ya Msumbiji.



APP YETU MPYA: Sasa unaweza kusoma kwa urahisi kupitia APP yetu. Download hapa kwa KUBOFYA HAPA

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini