NGOMA inazidi kupigwa kwa sasa ndani ya Ligi Kuu Bara ambapo vita ya kuwania ubingwa imeanza kukolea kwa timu tatu za juu ambazo zinaonekana kuwa na jambo lao wanalosaka. Simba ambao ni mabingwa watetezi kwenye mechi 10 hawajaambulia kunusa harufu ya kwanza baada ya ligi kuanza Septemba 6, jambo linaloongeza ushindani ndani ya ligi.
Timu zote tatu zina mitambo yao ya kazi inayowabeba huku makocha wakiwa na kazi katika kuwatumia nyota wao, hapa Championi Ijumaa inakuletea namna vita ilivyo ndani ya tatu bora msimu wa 2020/21;
AZAM FC
Imecheza jumla ya mechi 10, imefunga mabao 18 imefungwa mabao manne na pointi zake ni 25.
Imeweka bayana kupitia kwa Mtendaji Mkuu wa timu hiyo, Abdulkarim Amin kuwa inahitaji kuwa tofauti kwa msimu wa 2020/21. “Tuna malengo makubwa kwa msimu wa 2020/21, hali hiyo imepelekea tumefanya usajili makini, imani yetu tutaleta ushindani ndani ya ligi,” alisema.
PRINCE DUBE
Mtambo wa mabao ni Prince Dube ambaye kwenye mechi 10 ameweza kuanza kikosi cha kwanza mechi zote na amehusika kwenye mabao 10 kati ya 18. Amefunga mabao sita na ametoa jumla ya pasi nne za mabao ndani ya kikosi hicho kinachonolewa na Kocha Mkuu, Aristica Cioaba.
Mkononi ana tuzo ya mchezaji bora wa mwezi Septemba ndani ya ligi sawa na bosi wake Cioaba. NYUMA YA NYAVU Kipa wao namba moja ni David Kissu ambaye yupo kwenye timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars.
Mchezo wa kirafi ki dhidi ya Burundi Uwanja wa Mkapa aliwakalisha benchi Aishi Manula wa Simba na Metacha Mnata wa Yanga na alifungwa bao moja nje ya 18. Kwenye mechi 10 ikiwa ni dakika 900 amekaa langoni ametunguliwa kwenye mechi dhidi ya Kagera Sugar 2-4 Azam FC, Azam FC 1-1 JKT Tanzania na Mtibwa Sugar 1-0 Azam FC.
Kibindoni ana clean sheet saba akiwa amefungwa jumla ya mabao manne na ana wastani wa kuokota bao moja langoni kila baada ya dakika 225. YANGA Ipo nafasi ya pili imefunga mabao 12.
Msimu wa 2019/20 waliboronga kwenye mashindano yote makubwa ambapo kwenye ligi waliishia nafasi ya pili na ile ya Kombe la Shirikisho walitunguliwa na watani zao wa jadi Simba kwa mabao 4-1 Uwanja wa Mkapa hatua ya nusu fainali.
MICHAEL SARPONG
Mtupiaji namba moja ndani ya Yanga ametupia jumla ya mabao matatu na moja kati ya hilo aliwafunga watani wa jadi Simba kwenye dabi yake ya kwanza Novemba 7. Chini ya Cedric Kaze ambaye ameliambia Championi Ijumaa kuwa kazi bado inaendelea, imejikusanyia jumla ya pointi 24 ikiwa nafasi ya pili na imecheza mechi 10 bila kupoteza mchezo mpaka sasa.
UKUTA MATATA
Safu ya ulinzi inayoongozwa na mzawa Bakari Mwamnyeto ingizo jipya kutoka Klabu ya Coastal Union, imefungwa mabao matatu ikiwa ni idadi ndogo kuliko timu zote Bongo.
NYUMA YA NYAVU
Kipa namba moja ni Metacha Mnata, ameanza kikosi cha kwanza kwenye mechi 9, amefungwa mbele ya KMC 1-2 Yanga, Yanga 1-1 Simba. Amekusanya clean sheet 7.
SIMBA
Simba imefungwa mabao matano na imefunga mabao 22 ina pointi 20 nafasi ya tatu. Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara wana kazi nzito ya kufanya kutetea taji lao msimu wa 2020/21 kutokana na kuwa na tatizo kwenye safu ya ulinzi ambayo inaongoza kwa kuruhusu mabao mengi kwa zile zilizopo tatu bora ambayo ni matano.
Sven Vandenbroeck, Kocha Mkuu wa Simba alishuhudia timu yake ikiyeyusha pointi 10 ilizokuwa inasaka ndani ya ligi kwa kuanza kuambulia sare ya kufungana bao 1-1 dhidi ya Mtibwa Sugar, kichapo cha bao 1-0 dhidi ya Tanzania Prisons, bao 1-0 dhidi ya Ruvu Shooting na sare ya kufungana bao 1-1 dhidi ya Yanga.
ULINZI
Safu yake ya ulinzi inayoongozwa na Joash Onyango ilianza kupoteana kwenye mchezo wa kwanza wa ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Ihefu jambo ambalo linaipasua kichwa Simba ambayo inaiwakilisha nchi kimataifa.
Nyuma ya nyavu kipa namba moja Aishi Manula amekaa kwenye mechi saba, amekusanya clean sheet tatu na kutunguliwa mabao manne, ilikuwa mbele ya Tanzania Prisons 1-0, Ihefu 1-2 Simba, Simba 1-1 Yanga, Mtibwa Sugar 1-1 na bao la tano alitunguliwa Beno Kakolanya kwenye kichapo cha bao 1-0 dhidi ya Ruvu Shooting na ana clean sheet mbili. LUIS MIQUISSONE Mtambo wa mabao ni Luis Miquissone ambaye ni kinara wa pasi za mwisho ndani ya ligi akiwa nazo sita na amefunga bao moja kati ya mabao 22.
APP YETU MPYA: Sasa unaweza kusoma kwa urahisi kupitia APP yetu. Download hapa kwa KUBOFYA HAPA
0 Comments