By Charles Abel
Dar es Salaam. Ushindi ama pointi moja dhidi ya Tunisia leo kimojawapo kinaweza kuwa karata muhimu kwa Taifa Stars, wakati itakapokuwa mjini Tunis, Tunisia saa 4.00 usiku wa kuwania kufuzu fainali za Matiafa ya Afrika (Afcon) 2021.
Ikiwa inashika mkia katika Kundi J, Stars inahitaji angalau kupata pointi moja leo ili iweke hai matumaini yake ya kushiriki Afcon kwa mara ya pili mfululizo, vinginevyo hali itakuwa mbaya.
Ushindi wa mabao 3-2 ambao wapinzani wengine wa Stars kwenye kundi hilo, Guinea ya Ikweta waliupata dhidi ya Libya, uliiporomosha Tanzania hadi mkiani mwa Kundi J, wakiwa na pointi tatu, mabao matatu ya kufunga na matatu ya kufungwa.
Kwa maana hiyo, kama Stars itapoteza leo dhidi ya Tunisia, ambao wanaongoza kundi wakiwa na pointi sita, Guinea ya Ikweta watakuwa katika nafasi nzuri ya kutinga Afcon mwakani kwani wao wana faida ya kucheza mechi mbili nyumbani ambazo sio ngumu, dhidi ya Stars na Libya, huku wakiwa na moja ngumu ugenini dhidi ya Tunisia, ambayo itakuwa imefuzu.
Kwa wenyeji Tunisia, ushindi wa leo dhidi ya Stars utawafanya wahitaji pointi moja ili wajihakikishie kufuzu Afcon kwani watafikisha pointi 9 na wakipata sare katika mechi itakayochezwa nchini Novemba 17, watafikisha pointi 10, ambazo hazitaweza kufikiwa na Tanzania, Libya wala Guinea ya Ikweta.
Stars inaingia katika mchezo wa leo ikimkosa nahodha na mshambuliaji tegemeo, Mbwana Samatta anayechezea Fenerbahce ya Uturuki, ambaye ni majeruhi, lakini wakati huohuo itawakosa Thomas Ulimwengu na Adam Adam, ambao hawajasafiri na timu hiyo kutokana na kutotimiza taratibu za uhamiaji.
Habari Zinazohusiana
Kukosekana kwa washambuliaji hao bila shaka kunalilazimisha benchi la ufundi la Stars kufanya mabadiliko kadhaa ya kiufundi na kikosi na hapana shaka linaweza kuendelea na mfumo wa 4-2-3-1, lakini kiungo Himid Mao akachezeshwa nafasi ya winga, huku Saimon Msuva akaendelea kama mshambuliaji wa kati, winga nyingine akipangwa John Bocco kwa lengo la kuifanya timu ianze kuwakaba Tunisia kuanzia juu.
Huenda kukawa na mabadiliko katika safu ya ulinzi, ambako Juma Kaseja anaonekana anaweza kuanza badala ya David Mapigano, huku Abdallah Kheri akionekana kumpisha Erasto Nyoni katika nafasi ya beki wa kati akicheza sambamba na Bakari Mwamnyeto, mabeki wa pembeni wakiwa ni Shomary Kapombe na Mohamed Hussein.
Viungo wawili wa chini huenda wakapangwa Jonas Mkude na Feisal Salum, ambao juu yao huenda akapangwa Salum Abubakar ‘Sure Boy’
Kikosi cha Star kinaweza kuwa hivi, Juma Kaseja, Shomari Kapombe, Mohamed Hussein, Bakari Mwamnyeto, Erasto Nyoni, Jonas Mkude, Himid Mao, Feisal Salum, Saimon Msuva, Salum Abubakar ‘Sure Boy na John Bocco.
Utakuwa ni mchezo wa kwanza kuzikutanisha Stars na Tunisia kwani kabla ya hapo timu hizo hazijawahi kukutana katika mashindano yoyote na hata mechi za kirafiki.
Katika mchezo wa leo, Stars wanapaswa kuwachunga zaidi wachezaji wanne wa Tunisia ambao ndio wamekuwa chachu ya mafanikio ya timu hiyo katika siku za hivi karibuni.
Wachezaji hao ni beki wa kushoto anayechezea Al Ahly ya Misri, Ali Maaloul kutokana na kasi na uwezo wake wa kutengeneza nafasi na kufunga mabao lakini pia viungo, Seifeddine Khaoui wa Olympique Marseilles na Ferjani Sassi wa Zamalek ambao ni mafundi wa kuchezesha, kuiunganisha timu na kupika mabao.
Ukiondoa hao, wapo washambuliaji wawili ambao wana uwezo mkubwa wa kufunga mabao na kupiga pasi za mwisho ambao ni Wahbi Khazri anayechezea Saint-Etienne ya Ufaransa na nyota wao wa timu Youssef Msakni anayecheza soka la kulipwa huko Qatar katika timu ya Al-Duhail.
Akizungumzia mechi hiyo, mshambuliaji Saimon Msuva alisema wapo tayari kukabiliana na Tunisia na kuwashangaza wakiwa kwao kutokana na maandalizi mazuri waliyoyapata chini ya kocha wao, Ndayiragije.
APP YETU MPYA: Sasa unaweza kusoma kwa urahisi kupitia APP yetu. Download hapa kwa KUBOFYA HAPA
0 Comments