CHILDBIRTH SURVIVAL INTERNATIONAL(CSI) WAJA NA PROGRAMU KUWAWEZESHA VIJANA KUTIMIZA NDOTO ZAO | ZamotoHabari.

Na Said Mwishehe, Michuzi TV
SHIRIKA la Childbirth Survival International(CSI)limeamua kuanzisha programu maalum ya kuwasaidia vijana kutumiza ndoto zao za kimaisha ambazo zimekwama kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ya kiuchumi, ambapo kupitia programu hiyo vijana watapata elimu itakayowawezesha kujimudu kimaisha.
Kwa mujibu wa CSI, wameamua kuungana na vijana na kuwasaidia kwasababu vijana ndio wazazi wa kesho , na kijana anapowezeshwa tangu anapokuwa mdogo akaweza kusoma na kupata elimu inamaana akiwa mtu mzima anaweza kujikidhi mahitaji na kujisimamia katika masuala ya ujasiriamali na kazi.
Akizungumza leo Desemba 18, 2020 jijini Dar es Salaam wakati wa mchakato wa kuwapata vijana hao kupitia usaili uliofanywa chini ya CSI na Chuo cha Urembo Maznat, Meneja Programu za Vijana kutoka Shirika hilo Ester Mpanda amesema wameamua kuja na programu hiyo kwa ajili ya kusaidia vijana kujikwamua kiuchumi.
"CSI tunaamini tunapomuandaa kijana wa leo katika kumuwezesha kutimiza ndoto yake kimaisha, maaa yake tunakwenda kumsaidia kiuchumi , kupitia programu hii ya kuwasaidia vijana tutalipa ada na nauli kwa vijana ambao wanakwenda kusoma Chuo cha Urembo Maznat, wakimaliza masomo watajiari au kuajiriwa.Hivyo kijana anapokuwa na ujuzi wake ataweza kujimudu katika kukidhi mahitaji yake, kijana huyu ambaye tunamuandaa leo kimaisha ndio anayekuwa kuwa baba au mama wa kesho,"amesema Ester Mpanda.
Amesisitiza wanaamini vijana ndio wazazi wa kesho na anapowezeshwa kuanzia mdogo akasoma na kupata elimu inamaana akiwa mtu mzima anaweza kukidhi mahitaji yake kwa kujisimamia katika masuala ya kibiashara na kazi ili aweze kuisaidia familia yake kupata chakula na lishe bora au anapokuwa katika familia yake aweze kwenda klikini kwa wakati.
"Hivyo katika siku ya leo tumekuwa na vijana 20 ambao wamekuja kwenye programu hii kujaribu bahati yao na wale ambao watashinda baada ya kujieleza na kujibu maswali ya majaji watapata nafasi ya kwenda kusoma katika chuo hicho ambacho ambacho kinafundisha masuala ya urembo , ushonaji na kazi nyingine za mikono.
"Kwetu CSI tunaamini hii ni fursa kwa vijana na programu ambayo itakuwa endelevu, tunataka kuanza wazazi wa kesho ambao wataweza kumudu kuhudumia familia zao ikiwa ni mkakati ule ule wa kupambana na kukomesha vifo vya mama na mtoto wakati wa kujifungua ,"amesema Ester.
Aidha mbali ya CSI kuzungumzia umuhimu wa programu hiyo ya kuwawezesha vijana, imetumia nafasi hiyo kuipongeza na kuisifu Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dk.John Magufuli kwasababu imesogeza huduma za afya karibu na wananchi kwa kujenga zahanati na vituo vya afya. "Awali huduma za afya zilikuwa mbali na hivyo kusababisha changamoto ya kupata huduma za afya hasa kwa mama na mtoto.
"Sasa hivi chini ya Rais Magufuli kila mahali iwe kwenye kitongoji, kijijini au mijini kuna vituo vya afya, hivyo hata sisi CSI kazi yetu imekuwa rahisi , ni kwenda tu na kuelimisha watu kuwaambia umuhimu wa kwenda kliniki mapema, kutambua viashiria hatarishi kwa mama mjamzito ili kupunguza vifo kwa mama na mtoto,"amesema.
Kuhusu CSI, Ester amesema ni shirika la kimataifa ambalo limeanzishwa na wamama wa wawili Tausi Hamis Kagasheki ambaye yupo nchini Marekani ambako ndiko yalipo makao makuu ya CSI pamoja na mama Stella Mpanda ambaye yupo nchini Tanzania, waliamua kuanzisha shirika hilo ikiwa ni mkakati wa kukabiliana au kupunguza vifo kwa mama mjazito na mtoto wakati wa kujifungua.

Kupitia CSI wamekuwa wakitoa elimu kwa jamii kuhusu kutambua afya ya uzazi salama kupitia programu mbalimbali ambazo wamekuwa wakizitoa kwa zaidi ya miaka 10 sasa sambamba na kusaidia vifaa vya kujifungulia katika hospitali mbalimbali nchini.
"CSI tumekuwepo kwa muda mrefu sasa, na tupo Somalia,Rwanda na tunarajia kuwa na tawi nchini Rwanda, haya ambayo tunafanya Tanzania yanafanyika pia na kwenye nchi hizo , hivyo tutaendelea kutoa elimu ya afya ya uzazi salama kwa akina mama na vijana kupitia programu zetu mbalimbali,"amesema.
Awali Mwalimu wa Chuo cha Maznat Josephine Augustino amewaambia vijana waliokuwa kwenye usaili huo zaidi ya 20 kwamba, umefika wakati kwa vijana kujitambua na kujimiani, na kwamba kupitia urembo na ushonaji wataweza kujiajiri na kujiingizia kipato."Hiki ambacho CSI wanakifanya kwa kushirikiana na Chuo chetu cha Maznat kinakwenda kufungua ukurasa mpya kwa vijana.
"Tunafahamu wapo ambao wanaona kazi ya urembo ni kwa ajili ya wanawake tu, lakini tunasema hapana, kazi hii inafanywa na wanaume pia.Tumekuwa tukifundisha kuhusu urembo ambao upo wa aina mbalimbali, tunafundisha ushonaji, kupamba kumbi a harusi pamoja na kumbi za starehe, wengi ambao wamepita chuoni kwetu wamejipatia ajira aidha za kujiajiri au kuajiriwa.
"Wanaendesha maisha yao bila tatizo lolote, hivyo niwaombe vijana jitokezeni na wakati ni sasa, kwa kutumia mikono tuliyonayo tunaweza kubadilisha maisha yetu kutoka hapa yalipo na kuwa bora zaidi, mimi kupitia mikono yangu nasuka, napamba maharusi na kufanya shughuli nyingine ambazo zote zinaniingizia kipato,"amesema.
Wakati huo huo vijana Suzana Kanyara na David Francis wameibuka washindi baada ya majaji kutoka CSI na Chuo cha Maznat kuwachagua baada ya kujibu maswali na kujieleza vizuri, hivyo watapata nafasi ya kusoma katika chuo hicho kwa kulipiwa ada na nauli kwa muda wote wa masomo na CSI ndio watakaogharamia.

Meneja wa Programu za Vijana katika shirika la Childbirth Survival International(CSI) Ester Mpanda akizungumza na washiriki wakati wa mchakato wa kuwapata vijana hao kupitia usaili uliofanywa chini ya CSI na Chuo cha Urembo Maznat ili kuwapata vijana wawili watakaofadhiliwa na shitika hilo kwenye masomo ya urembo.
Mwalimu wa Chuo cha Urembo Maznat, Josephine Augustino akizungumza na washiriki kuhusu chuo cha Maznat kinavyofanya kazi pamoja na kuwasisistiza vijana kujitambua na kujimiani ili kufikia malengo waliojiwekea wakati wa mchakato wa kuwapata vijana hao kupitia usaili uliofanywa chini ya CSI na Chuo cha Urembo Maznat
Baadhi ya washiriki wakifuatia mada zilizokuwa zinatolewa wakati wa mchakato wa kuwapata vijana hao kupitia usaili uliofanywa chini ya CSI na Chuo cha Urembo Maznat
Mwalimu wa Chuo cha Urembo Maznat, Juma Kimwaga akizungumza na washiriki kuhusu kujitambua na kusisitiza kazi za mikono ni kazikama kazi nyingine wakati wa mchakato wa kuwapata vijana hao kupitia usaili uliofanywa chini ya CSI na Chuo cha Urembo Maznat.
Baadhi ya washiriki wakiwa kwenye usaili kwenye mchakato wa kuwapata vijana wawili uliofanywa chini ya CSI na Chuo cha Urembo Maznat watakaosomeshwa masuala ya urembo na Shirika la Childbirth Survival International(CSI).
David Francis ambaye aliibuka mshindi kwenye usaili wa kuwapata vijana wawili uliofanywa chini ya CSI na Chuo cha Urembo Maznat akizungumza na waandishi wa habari kuhusu namna alivyojiamini mpaka kuwa mshindi kwenye shundano hilo.
Uogozi wa Shirika la Childbirth Survival International(CSI) wakiwa kwenye picha ya pamoja na walimu wa Chuo cha Urembo Maznat pamoja na washiriki waliofika kwenye usaili wa kuwapata vijana wawili uliofanywa chini ya CSI na Chuo cha Urembo cha Maznat .
Uogozi wa Shirika la Childbirth Survival International(CSI) pamoja na walimu wa Chuo cha Urembo chaMaznat wakiwa kwenye picha ya pamoja na washindi ambao ni ni Suzana Kanyara(wa pili kushoto) na David Francis (wa tatu kushoto) waliopatikana kwenye usaili wa kuwapata vijana wawili watakaosomeshwa na shirika ilo masuala ya urembo katika chuo cha Urembo cha Maznat


APP YETU MPYA: Sasa unaweza kusoma kwa urahisi kupitia APP yetu. Download hapa kwa KUBOFYA HAPA

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini