Jeshi la Polisi laipongeza SGA kwa kuwajali wafanyakazi | ZamotoHabari.

 

SGA Security, ambayo ni kampuni inayoongoza na kongwe ya binafsi ya ulinzi Tanzania imepogezwa na Jesi la Polisi kwa namna inavyowahudumia wafanyakazi wake.

Pongezi hizo zilitolewa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, ACP Ramadhan Kingai wakati akiwatunuku wafanyakazi waliohudumu kwa muda mrefu katika kampuni hiyo.  

Kamanda huyo alisema jitihada za SGA katika kujali masilahi ya wafanyakazi ilisababisha kampuni hiyo kupata tuzo ya kampuni bora ya ulinzi iliyo na vifaa vya kutosha na inaamnika zaidi yaani Most Equipped and Reliable Security Company of the Year, 2020award wakati wa Tuzo za Chaguo la Mteja (Tanzania Consumer Choice Awards) Jijini Dar es Salaam hivi karibuni na inadhihirisha imani ya wateja kwa SGA.  

Kamanda Kingai alitoa wito kwa makampuni mengine ya ulinzi yaige mfano wa SGA Security na namna inavyoendesha shughuli zake.

Alisema alipata nafasi ya kushuhudia namna SGA inaendesha shughuli zake na alifurashishwa na namna kampuni hiyo imewekeza katika teknolojia ya kisasa ikiwemo magari yanayotumiwa kusafirisha vitu vyenye thamani, jambo ambalo limefanya kampuni hiyo iendelee kuongoza katika sekta hiyo.

Alisema wanachokifanya SGA kinaendana na maono ya Rais John Pombe Magufuli ya wawekezaji kuwapa wafanyakazi wao kipaumbele.  

Aliwapongeza wafanyakazi wote waliotimiza miaka 20 na zaidi kazini ambao wanajiunga na Kilabu maalumu kinachojulikana kama Club 20, jambo ambalo alisema ni nadra kwa makampuni binafsi ya ulinzi huku akiwakumbusha kuwa siri ya mafanikio ni kujituma, nidhamu na weledi katika utendaji wa kazi.

Kamanda huyo alipata fursa ya kumtunuku Bw. Clifton Desouza aliyeitumikia kampuni hiyo kwa miaka 42.

Alitumia fursa hiyo pia kutoa wito kwa makampuni yote ya ulinzi kufuata sheria na miongozo inayotolewa na Jeshi la polisi na kuwataka pia watumie jeshi hilo katika zoezi la kuwapata walinzi wazuri ambao wana sifa njema na wasio na rekodi ya uhalifu.

“Mameneja rasilimaliwatu wana jukumu la kutunza kumpukumbu za wafanyakazi vizuri na zinajitosheleza ikiwemo kitambulisho cha taifa na taarifa za wadhamini wao,” alisema na kuongeza kuwa kumekuwepo kesi za walinzi kukabidhi nyaraka feki na kumbukumbu feki za wadhamini na baadaye kufanya uhalifu na kukimbia.

Shughuli hii ya kuwatunuku wafanyakazi ilifanyika katika matawi yote ya SGA  Security nchi nzima huku Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Eric Sambu akielezea kuwa shughuli hiyo ya kuwatambua wafanyakazi waliohudumu kwa zaidi ya miaka 20 hufanyika kila mwaka na wao hujiunga katika Club 20.

Alisema hadi sasa Club 20 ina zaidi ya wanachama 240 na wanazidi kuongezeka na kudhihirisha kuwa wafanyakazi hao wana malengo ya kufanya kazi na kampuni hiyo hadi wakati wa kustaafu kisheria.

Alisema SGA ina wafanyakazi zaidi ya 6000 nchi nzima huku meneja Rasilimali watu, Ebenezer Kaale akisema siri ya mafanikio ni jinsi wamekuwa wakiwajali wafanyakazi wao.“Tunaamini kuwa tukiwajali basi nao watawajali wateja zaidi. Huwa tunawachunguza vizuri kabla ya kuwaajiri, tunawapa mafunzo ya mara kwa mara na pia kuwapa motisha mara kwa mara,” alisema.

SGA Security inatoa huduma mbalimbali ikiwemo za ulinzi, alarm, huduma za fedha, ulinziwa kielektroniki, huduma ya kusafirisha mizigo na huduma nyinginezo.

SGA pia inajivunia kuwa kampuni pekee yenye cheti cha ISO18788 (Security Operations Management System). Pia ina ISO 9001: 2015 na ISO 45000:2018 (Occupation Health and Safety).

Kamanda wa Polisi katika Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, ACP Ramadhan Kingai (kushoto) akitoa tuzo kwa Clifton Desouza ambaye ni mfanyakazi aliyehudumu katika kampuni ya SGA Security kwa miaka mingi tangu ilipoanzishwa 1984 na kwa sasa anastaafu akiwa amitumikia kampuni hiyo kwa miaka 42. Tuzo hiyo ilitolewa wakati  wa hafla ya mwisho wa mwaka kuwatunuku wafanyakazi waliohudumu kwa muda mrefu.
Kamanda wa Polisi katika Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, ACP Ramadhan Kingai (aliyekaa katikati) pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa SGA Security, Eric Sambu (mwenye kofia nyeupe) na mameneja wengine wa kampuni hiyo wakiwa katika picha ya pamoja na wanachama wapya wa Club 20 ya wafanyakazi waliohudumu zaidi ya miaka 20 katika kampuni hiyo wakati  wa hafla ya mwisho wa mwaka kuwatunuku wafanyakazi  waliohudumu kwa muda mrefu 
Kamanda wa Polisi katika Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, ACP Ramadhan Kingai (kushoto) akitoa zawadi kwa mmoja wa wafanyakazi waliohudumu katika  kampuni ya SGA Security kwa miaka mingi. Tuzo hiyo ilitolewa wakati  wa hafla ya mwisho wa mwaka kuwatunuku wafanyakazi waliohudumu kwa muda mrefu.


APP YETU MPYA: Sasa unaweza kusoma kwa urahisi kupitia APP yetu. Download hapa kwa KUBOFYA HAPA

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini