SERIKALI KUBORESHA MAENEO YA KUTUPA TAKA:DKT. SUBI | ZamotoHabari.

 

Mkurugenzi wa huduma za kinga kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Leonard Subi akitoa maelekezo kwa Maafisa Afya mazingira (hawapo kwenye picha) katika kilele cha wiki ya usafi wa mazingira kitaifa na mkutano wa maafisa afya wa mikoa na halmashauri iliyofanyika jijini Dodoma.

Mkurugenzi msaidizi wa Afya mazingira Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Khalid Massa akimkaribisha Mkurugenzi wa huduma za kinga Wizara ya Afya Dkt. Leonard Subi (hayupo kwenye picha) wakati wa kilele cha wiki ya usafi wa mazingira kitaifa na mkutano wa maafisa afya wa mikoa na halmashauri iliyofanyika jijini Dodoma.

Maafisa Afya mazingira kutoka ngazi ya Mikoa na Halmashauri wakifuatilia neno kutoka kwa Mgeni rasmi ambae ni Mkurugenzi wa Huduma za Kinga Wizara ya Afya Dkt Leonard Subi wakati wa kilele cha wiki ya usafi wa mazingira kitaifa iliyofanyika jijini Dodoma.

Na.Catherine Sungura,WAMJW-Dodoma

Serikali ya awamu ya tano ina nia ya dhati ya kuboresha maeneo ya kutupia taka hususani madampo yaliyopo kwenye miji ili yawe ya kisasa.

Hayo yamesemwa leo na Dkt. Leonard Subi Mkurugenzi wa huduma za kinga kutoka Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto kwenye kilele cha wiki ya usafi wa mazingira kitaifa na mkutano wa maafisa afya wa mikoa na halmashauri iliyofanyika jijini Dodoma.

Dkt.Subi amesema kuwa,uchafuzi wa mazingira utokanao na taka ngumu umeendelea kuwa changamoto katika maeneo ya mijini.

“Ili kukabiliana na tatizo hili,Serikali imepanga kuongeza nguvu kwenye mamlaka za serikali za mitaa ili kuboresga miundombinu katika mitaa iliyopo nchini hasa katika suala la usimamizi wa taka ngumu na majitaka”.

Aidha,Dkt. Subi amesema serikali imeandaa mwongozo wa uwekezaji katika taka ngumu ili kuhamasisha uwekezaji na kuongeza jitihada za kuboresha usimamizi wa taka hapa nchini.

Hata hivyo alizitaka halmashauri zipitie sheria ndogo za halmashauri ili kutekeleza vema,Sheria ya Afya ya Jamii ya mwaka 2009 hususani katika maeneo ya utiririshaji maji taka hasa katika maeneo ya mijini na kudhibiti tabia ya kujisaidia porini wakati wa kusafiri maarufu kama ‘ kuchimba dawa’ ambayo bado imeendelea kuwepo.

Dkt.Subi aliwapongeza maafisa afya hao katika maeneo ya ujenzi wa vyoo bora,unawaji wa mikono ,huduma za afya mipakani,udhibiti wa kipindupindu,Corona,mlipuko wa Dengue pamoja na udhibiti wa taka zitokanazo na huduma za afya na mengine mengi.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Maafisa Afya Tanzania (CHAMATA) Twaha Mubarak ameishukuru Wizara ya afya kwa kufanya afya mazingira ni kipaumbele katika kuondoa magonjwa,hivyo wataalam wanajivunia na kuweza kupunguza ugonjwa wa Malaria ili kuweza kufanikiwa kutimiza lengo la kutokomeza Malaria ifikapo mwaka 2030



APP YETU MPYA: Sasa unaweza kusoma kwa urahisi kupitia APP yetu. Download hapa kwa KUBOFYA HAPA

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini