CHAMA kikuu cha Ushirika cha Sonamcu mkoani Ruvuma, kimesambaza zaidi ya mifuko 4,444 ya mbolea aina ya SA kwa wakulima wa zao la tumbaku ambao ni wanachama wa chama hicho kama mkakati wake wa kuboresha kilimo cha zao hilo katika msimu wa kilimo 2020/2021.
Meneja shughuli wa Sonamcu Zamakanaly Komba alisema, mbolea hiyo imeshakwenda kwa wakulima wa vyama 28 vinavyojishughulisha na kilimo cha Tumbaku ambapo kati ya vyama hivyo kimoja kipo wilaya ya Mbinga, kimoja Songea na vilivyobaki vipo katika wilaya ya Namtumbo.
Alisema,msimu wa mwaka huu wanatarajia kulima jumla ya ekari 1,111 ambazo zitaleta mavuno zaidi ya tani 5000 kutoka kwa wakulima hao ambapo kazi ya (kuatika)kuotesha mbegu kwenye vitalu imeshashafanyika na wakulima wanasubiri mvua ili waanze kupeleka shambani.
Alisema, matumizi ya mbolea aina ya SA imetokana na mahitaji ya mnunuzi kampuni ya Primer Active Tanzania Ltd ambayo kutokana na soko ametoa sharti kwa wakulima kutumia mbolea aina ya SA sio nyingine kama ilivyozoeleka na wakulima wengi wa tumbaku.
Komba alisema, Sonamcu imeingia mkataba wa miaka saba kuanzia mwaka 2017 na kampuni hiyo kuzalisha tumbaku ya moshi, ambapo katika msimu wa kilimo 2020/2021 chama hicho kupitia vyama vya msingi vya ushirika vimepewa lengo la kuzalisha 5000 tu na mnunuzi.
Alisema, hilo ni pigo kubwa kwa wakulima na hata kwa Sonamcu kwani katika msimu msimu 2018/2019 walipewa kuzalisha tani 1000 lakini wakulima walifanikiwa kuvuna tani 1247 na hivyo kuvuka lengo.
Kwa mujibu wa Komba katika msimu 2019/2020 walipewa kuzalisha tani 800, lakini walishuka kufikia kiwango walichopewa badala yake walizalisha tani 745.
Alisema sababu za kushusha kwa kiwango cha kuzalisha tumbaku ni kutokana na soko la tumbaku ya moshi ambalo liko katika nchi wanachama wa COMESA na Tanzania sio mwanachama, tofauti na tumbaku aina nyingine zinazozalimwa katika mikoa mingine.
Aidha alisema, licha ya mnunuzi kuwataka kupunguza uzalishaji ni jambo la kujivunia ni kwamba ndiyo zao pekee mkoani Ruvuma ambapo mkulima kabla hajaingia shambani ana uhakika wa bei ikilinganisha na mazao mengine yanayolimwa katika mkoa wa Ruvuma.
Amesema, Sonamcu inajuvunia sana kuona sasa hali ya maisha ya wakulima wa Tumbaku ni nzuri kutokana na kupata soka la uhakika ambapo wakulima wengi wamejenga nyumba bora tofauti na siku za nyuma.
Hata hivyo alisema, changamoto kubwa kwa wakulima ni uzalishaji mdogo licha ya uwezo wa wakulima katika uzalishaji kuwa mkubwa na sasa baada ya kuona kuna soko la uhakika wakulima wanataka kulima zao hilo, Sonamcu inalazimika kugawa katika vyama vyake 15 vinavyolima zao hilo kiasi cha kuzalisha.
Komba, amewataka wakulima kuwa wavumilifu wakati huu Sonamcu inaendelea na mazungumzo na mnuuzi ili kama kuna uwezekano wa kununua tumbaku nyingi katika msimu ujao.
Alisema, wao kama chama kikuu wataendelea kutoa pembejeo kwa wakulima mwaka hadi mwaka ili kuwasaidia wanachama wao ambapo amewataka wakulima wachache waliobahatika kuwemo kwenye mpango, kuhakikisha wanazalisha tumbaku bora kama hatua ya kumshawishi mnunuzi kuongeza kiwango cha mahitaji yake .
Kwa upande wao, baadhi ya wakulima wa tumbaku wameishukuru serikali ya awamu ya tano kwa jitihada za kufufua zao hilo ambalo lilishaanza kupotea kutokana na kukosa soko la uhakika na hivyo kuwakatisha wakulima tamaa.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake Ali Ngonyani alisema, jitihada zilizofanywa na Serikali kwa kushirikiana chama kikuu kimeleta faraja kubwa kwa wakulima na wananchi hususani wa wilaya ya Namtumbo ambao kwa muda mrefu wanategemea zao hilo kama njia kuu ya uchumi wao.
Hata hivyo,wameiomba Sonamcu uamuzi wa kutoa pembejeo usiishie katika zao la tumbaku tu bali kuangalia na mazao mengine kama ufuta,mbaazi na soya ambayo kwa sasa yana soko kubwa na yameanza kuleta tija kubwa kwa wakulima.
APP YETU MPYA: Sasa unaweza kusoma kwa urahisi kupitia APP yetu. Download hapa kwa KUBOFYA HAPA
0 Comments