ILI uwe supastaa wa ukweli, achana na wale wa kulazimisha, kuna vitu vitatu vya muhimu unapaswa kuwa navyo; kipaji, nyota na koneksheni. Ukikosa kimojawapo, angalau ubaki na viwili, lakini usikose kuwa na nyota. Mwaka huu unaoelekea ukingoni ulishuhudia wasanii wengi wakifurukuta kutoboa kwenye gemu la Bongo Fleva.
YUPO ZUCHU MMOJA TU
Lakini OVER ZE WEEKEND inamtaja mmoja aliyeushangaza ulimwengu wa Bongo Fleva. Ni Zuhura Othman Soud almaarufu Zuchu; mtoto wa Malkia wa Taarab Afrika Mashariki na Kati, Bi Khadija Omari Kopa.
Zuchu ameweza kupenya kwenye mioyo ya Watanzania walio wengi kisha akavuka mipaka ya Tanzania, akaikamata Afrika Mashariki na sasa anajitengenezea himaya yake barani Afrika. Zuchu amejaaliwa vyote vitatu; yaani kipaji, nyota na koneksheni. Hakuna ubishi, Zuchu ndiye supastaa mpya namba moja wa kike Afrika Mashariki.
Miongoni mwa sababu za Zuchu kufanikiwa kwenye uwanda wa Bongo Fleva ni kujaaliwa nyota kali. Nyota ya Zuchu inafananishwa na ile ya kiongozi wake, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ ambaye ndiye C.E.O wa Lebo ya Wasafi Classic Baby (WCB) ndiyo maana amepachikwa jina la Diamond au Mondi wa kike kwenye mitandao ya kijamii.
Kutokana na vyote hivyo, habari za ndani ya WCB zinasema kwamba, huu ni mwanzo tu, lakini tutarajie kumuona Zuchu akifanya mambo makubwa na ya kushangaza kiasi kwamba atapachikwa majina ya kila aina kama Simba-Jike.
Tutabaki tunajiuliza kwa nini yeye, lakini tusipate majibu. Hivyo ndivyo nyota kali zinavyotokea. Sasa Zuchu ni second lady wa Wasafi baada ya Mwanahawa Abdul ‘Queen Darleen’. Zuchu amefanya mambo makubwa ndani ya miezi nane tangu alipotambulishwa kwenye gemu siku ile ya Aprili 8, mwaka huu.
Ameweka rekodi za kila aina kiasi cha runinga moja ya nchini Hispania kumpachika jina la Beyonce wa Afrika. Wengine wanamuita Zuchu Marekodi! Amedumu kwa kipindi kifupi mno kwenye gemu, lakini ameweza kufanya maajabu makubwa, ambayo yanathibitisha kwamba ni msanii wa kike ambaye hajawahi kutokea.
Tuziache kwanza rekodi za mitandao ya kusikiliza, kutazama, kuuza, kununua na kupakua muziki duniani, lakini kubwa ni ile tuzo ya kimataifa ya Mwanamuziki Bora Chipukizi wa Afrika Mashariki ya mwaka 2020 ya AFRIMMA. Huwenda Zuchu asikae kipindi kirefu, akaonekana tena kwenye Tuzo za AE, AUA, MTVMAMA na nyinginezo za kimataifa.
Tuzo ni jambo kubwa mno kwa mwanamuziki yeyote ndiyo maana kila kukicha msanii Rajabu Abdul ‘Harmonize’ analilia tuzo nyingi zianzishwe kwani pamoja na kufanya kwake muziki mzuri kwa takribani miaka mitano mfululizo, hajawahi kupata tuzo yoyote, jambo linalosemekana kumpa stresi za ajabu!
Zuchu; msanii kinda tu, lakini ameweza kutokea kwenye tuzo kubwa ambazo zinajumuisha wasanii wakubwa barani Afrika ambao wanafanya poa kinoma kwa sasa.
ZUCHU MAREKODI
Wakati hayo yakiendelea, Zuchu ameendelea kuweka rekodi mpya kila kukicha kupitia kolabo zake mbili na bosi wake, Mondi za Litawachoma na Cheche.
Ngoma hizi zimesikilizwa na zinasikilizwa (audio) na kutazamwa (video) kiasi kwamba zinaendelea kupenya na kutrendi duniani. Katika hali kama hiyo, Zuchu anazidi kupanda viwango siku hadi siku kuelekea kwenye ukubwa ambao haukutazamiwa.
KUTAZAMWA ZAIDI
Zuchu ametajwa na jarida moja nchini Kenya na mtandao wa kuuza muziki duniani wa Apple Music kama mmoja wa wasanii wa kutazamwa zaidi barani Afrika.
Ukichungulia kwenye mitandao ya kusikiliza, kutazama, kununua, kuuza na kupakua muziki ya ndani na nje ya Bongo, utaona ni jinsi gani Zuchu amekuwa wa moto kwa kila ngoma anayoachia, tofauti na wasanii wengi wapya.
KUTEKA SOKO
Ukiacha kukubalika pekee, lakini pia Zuchu ameliteka soko. Tayari amefikisha wafuasi (subscribers) zaidi ya laki 6 kwenye chaneli yake ya Mtandao wa YouTube, jambo ambalo limekuwa gumu kwa wasanii kibao waliodumu kwenye gemu kwa zaidi ya miaka 10, lakini hawajafikisha hata laki 5.
Hata ukifuatilia, mitandao yote ya muziki kama Boomplay Music, Audiomack, Apple Music, iTunes, Spotify, Deezer, Tidal, Pandora, Mdundo, Amazon Music na mingineyo, Zuchu amesikilizwa zaidi ya mara milioni 50 hadi sasa. Kule Instagram ana zaidi ya wafuasi milioni 1.6 ndani ya miezi hiyo nane tu!
Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kwamba, Zuchu amekuwa tishio kwa mastaa wenzake wa kike wa Bongo Fleva kama Faustina Charles ‘Nandy’, Esterlina Sanga ‘Linah’, Maua Sama, Zuwena Mohammed ‘Shilole’, Gift Stanford ‘Gigy Money’, Lulu Abbas ‘Lulu Diva’, Vannesa Mdee ‘V-Money’, Mariane Mdee ‘Mimi Mars’ na wengine kibao.
Hata hivyo, inasemekana kwamba, Zuchu ndiye msanii wa kwanza wa kike Afrika Mashariki kukubalika kwa muda mfupi zaidi.
Sasa, Zuchu amefikia levo ya kutrendi na mastaa wakubwa wa muziki barani Afrika kama Mondi, Wizkid, Davido, Tiwa Savege, Yemi Alade, Burna Boy na wengine kibao. Ni jambo kubwa mno kwa msanii mpya kama Zuchu kufikia levo za wasanii kama hao.
IAM ZUCHU EP (Extended Play) yake ya IAM ZUCHU ambayo aliiachia muda mfupi baada ya kusainiwa WCB hadi sasa inasumbua na kuweka rekodi kubwakubwa kwenye mitandao ya muziki.
Kwa rekodi zilizopo, IAM ZUCHU imesikilizwa, kutazamwa na kupakuliwa mara zaidi ya milioni 10 ikiwa na jumla ya ngoma saba.
KOLABO
Kwa muda mfupi, Zuchu ameweza kufanya kolabo na mastaa wengi akiwemo bosi wake, Mondi ambaye amefanya naye ngoma mbili za Litawachoma na Cheche, Joe Boy wa Nigeria, Rayvanny na Mbosso; wote kutoka Wasafi na zinakimbiza kinoma mitaani na mitandaoni.
MADILI
Hadi kampuni f’lani kufikia hatua ya kumuamini msanii huwa siyo kazi rahisi, ina ugumu wake. Lakini kwa Zuchu, imekuwa kama Mondi tu kwani kwa kipindi kifupi ameaminika na makapuni, kiasi kwamba kwa sasa ukimlinganisha na wasanii wengine, unahitaji roho ya kijasiri na iliyokosa aibu ili kumnyima ubalozi.
Vyanzo vya ndani ya Wasafi vinadai kwamba, sasa makampuni yanapishana kwenye ofisi zao wakitaka kuingia mikataba ya ubalozi wa brands (bidhaa) zao. Hadi sasa, tayari amepokea madili makubwa kama ubalozi wa nywele, siyo kitu kidogo maana kuna wasanii wana miaka zaidi ya 10 kwenye gemu, lakini hawajawahi kupata ubalozi wowote.
PONGEZI KWAKE Zuchu; kwa mahali alipofikia, yafaa kupata pongezi nyingi kwani hata kama anabebwa, basi amebebeka vizuri mno! Shukrani pia ziende kwa mashabiki kwa sababu bila wao, Zuchu asingefika hapo alipo kwenye levo za kidunia.
Makala: KHADIJA BAKARI
APP YETU MPYA: Sasa unaweza kusoma kwa urahisi kupitia APP yetu. Download hapa kwa KUBOFYA HAPA
0 Comments