Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel akisoma kibao cha Kijiji cha Emairete kilichopo Kata ya Monduli Juu, mara baada ya kufika katika kijiji hicho ambacho wafugaji wake wananufaika na Bwawa la Elwaniolera kwa ajili ya kunyweshea mifugo maji. Wafugaji wengine wanaonufaika na bwawa hilo ni kutoka vijiji vya Eluwai na Enguiki ambavyo pia vipo katika Kata ya Monduli Juu, Wilaya ya Monduli Mkoani Arusha.
KATIBU Mkuu Wizara ya Mifugp na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel amesema wafugaji wanaposhirikishwa katika uchangiaji wa miradi mbalimbali kwa ajili ya mifugo yao wamekuwa wakionyesha utayari na kufanya miradi hiyo kudumu kwa kuwa wanajisikia kuwa sehemu miundombinu hiyo.
Akizungumza (30.11.2020) katika bwawa la kunyweshea mifugo maji la Elwaniolera lililopo kijiji cha Eluwai, Kata ya Monduli Juu, Wilaya ya Monduli Mkoani Arusha, Prof. Gabriel amesema wakazi katika eneo hilo wameonesha utayari wa kulifanyia ukarabati bwawa hilo linalohudumia zaidi ya wafugaji 2,000 katika vijiji vya Eluwai, Emairete na Enguiki kutokana na kina cha bwawa hilo kupungua kutokana na shughuli mbalimbali za kibinadamu ikiwemo ya kilimo.
“Uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Monduli umenieleza kuwa wakazi wa Kata ya Monduli Juu wako tayari kushiriki kwa kiwango kikubwa katika kulifanyia maboresho bwawa hili, wafugaji wanaposhirikishwa nao wako tayari kushiriki na faida yake kubwa hakutakuwa na haja ya serikali kugharamia kila kitu lakini pia wanaposhirikishwa mara zote miundombinu hiyo huwa inadumu kwa kuwa nao watajisikia sehemu ya miundombinu hiyo.” Amesema Prof. Gabriel
Ameongeza kuwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi ipo tayari kulikarabati Bwawa la Elwaniolera kwa kujenga mabirika kwa ajili ya mifugo kunywea maji kwa kuwa hali ilivyo sasa ni hatari kwa mifugo, wachungaji pamoja na usalama wa bwawa lenyewe.
Aidha, Prof. Gabriel amesema wizara itaangalia namna ya kuboresha masuala ya majosho katika vijiji vya Eluwai, Emairete na Enguiki ili kuhakikisha kwamba dhana nzima ya kuboresha afya ya mifugo inafanikiwa.
Pia, amesema wakati Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli akizindua Bunge la 12 alifafanua kuwa angependa kuona Sekta ya Mifugo inachangia zaidi katika uchumi.
Amebainisha kuwa kwa sasa Sekta ya Mifugo inachangia kwa asilimia 7.64 na inakuwa kwa asilimia tano ambapo lengo la wizara ni kuhakikisha sekta hiyo ifikie kuchangia kwa zaidi ya asilimia 15.
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel amesema Kata ya Monduli Juu ina mifugo mingi hivyo masuala ya malisho na afya ya mnyama ni muhimu kwa kuwa na mifugo mingi na bora ni muhimu kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Monduli ili wafugaji waweze kunufaika kupitia Bwawa la Elwaniolera ili maji yake yaweze pia kutumika katika shughuli nyingine za kilimo cha umwagiliaji.
Kwa upande wake Afisa Mifugo wa Halmashauri ya Wilaya ya Monduli Dkt. Yandru Marmo amemueleza Prof. Gabriel kuwa Bwawa la Elwaniolera limeanza kupungua kina chake kutokana na shughuli za kibinadamu zinazoendelea katika chanzo cha maji ya bwawa hilo, hali inayosababisha udongo kusafirishwa hadi kwenye bwawa na kusababisha kina chake kuzidi kupungua na kuhofia madhara makubwa kwa wafugaji wanaolitegemea kunyweshea mifugo maji.
Dkt. Marmo ameongeza kuwa ni muhimu kwa bwawa hilo kufanyiwa ukarabati kwa kuwepo kwa mabirika ya kunyweshea mifugo maji ili mifugo isiingie ndani ya bwawa kwa kuwa inachangia pia udongo kuingia ndani ya bwawa pamoja na shughuli za kibinadamu ikiwemo ya kilimo zisifanywe karibu na chanzo cha maji ya bwawa hilo ili kuzuia pia udongo kusafirishwa hadi kwenye bwawa na kusababisha kina chake kupungua.
Bwawa la Elwaniolera lililopo Kata ya Monduli Juu, Wilaya ya Monduli Mkoani Arusha, lilijengwa mwishoni mwa miaka ya 1970 kwa jitihada za serikali wakati Hayati Edward Moringe Sokoine akiwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
APP YETU MPYA: Sasa unaweza kusoma kwa urahisi kupitia APP yetu. Download hapa kwa KUBOFYA HAPA
0 Comments