Waziri wa Viwanda na Biashara, Geoffrey Mwambe akizungumza kwenye mahafali ya 55 ya Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) yaliyofanyika Dar es Salaam mwishoni mwa wiki. Anayefuata ni Naibu Mkuu wa chuo Profesa Tandi Lwoga na Mkuu wa chuo hicho, Profesa Emmanuel Mjema na Naibu Waziri Wizara ya Viwanda na Biashara, Exhaud Kigahe.
Wahitimu wa fani mbalimbali wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) Dar es Salaam wakiwa kwenye mahafali ya 55 ya chuo hicho yaliyofanyika mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam ambapo mgeni rasmi alikuwa Waziri wa Viwanda na Biashara, Geoffrey Mwambe.
Waziri wa Viwanda na Biashara, Godfery Mwambe akimkabidhi zawadi mwanafunzi wa Chuo cha Elimu ya Biashara, Ali Hemedi Ali ambaye aliibuka mshindi wa jumla kwa ngazi ya Shahada ya Uzamili kwenye mahafali ya 55 ya Chuo Cha Elimu ya Biashara (CBE) yaliyofanyika mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam.Waziri aipongeza CBE kwa kupanda ubora wa vyuo vikuu
Na Mwandishi Wetu
WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Geoffrey Mwambe amekipongeza Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) kwa kufanikiwa kupanda kwa hadhi ya ubora wa vyuo vikuu ndani ya kipindi kifupi cha miaka mitano.
Ametoa pongezi hizo mwishoni mwa wiki kwenye mahafali ya 55 ya chuo hicho ambapo wahitimu 2,248 walitunukiwa astashahada, shahada ma shahada za uzamili katika fani mbalimbali.
Alisema hatua ya chuo hicho kupanda ndani ya muda mfupi kutoka nafasi ya 54 mpaka 14 ni jambo la kuigwa na la kujivunia na aliahidi kuwa serikali itaendelea kuwa bega kwa bega na chuo hicho kuhakikisha miundombinu yake inaboreshwa.
“Mmefanya kazi kubwa sana kuvuka kutoka nafasi ya 54 hadi nafasi ya 14 ndani ya miaka mitano si kazi ndogo, changamoto zote zilizosemwa hapa nimezichukua na ninawaahidi ushirikiano kuzitatua sitawaangusha kwasababu tunataka kuona CBE ikiendelea kutoa wahitimu bora,” alisema
Poa amewahimiza wahitimu wa Chuo hicho kutumia elimu waliyoipata kujiajiri na kuajiri watanzania wenzao badala ya kutembea na vyeti kutafuta ajira wanapohitimu.
Amesema kuna fursa nyingi sana ambazo wahitimu wanaweza kuzitumia na kuwa na maisha mazuri wakiwa wabunifu kwani sekta binafsi ndiyo mwajiri mkuu na siyo serikali.
“Mimi ningetamani kusikia kila mmoja hapa anaanzisha kampuni yake, wewe uliyesomea uhasibu anzisha kampuni ya kutengeneza hesabu za makampuni mbalimbali, uliyesomea ukaguzi anzisha kampuni ya kukagua hesabu na hata waliosomea masoko hivyo hivyo,” alisema Mwambe.
Waziri Mwambe amesema kazi ya serikali itakuwa kuweka mazingira mazuri kwa ukuaji wa sekta binafsi ili kuiwezesha kuongeza uzalishaji, kuongeza tija ili hatimaye Tanzania iwe na uchumi mkubwa Afrika Mashariki, Kusini mwa Afrika na duniani ikiwezekana.
Pia ameupongeza uongozi wa chuo hicho kwa namna walivyomudu kukiongezea hadhi chuo hicho na kupanda kuwa miongoni mwa vyuo bora nchini kutoka nafasi ya 53 ndani ya miaka mitano hadi kuwa nafasi ya 14.
Amesema inawezekana kabisa Tanzania kuondokana na umaskini iwapo kila mmoja atawajibika na kuwa mbinifu kwenye eneo lake la kazi .
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya chuo hicho, Profesa Esther Ishengoma amesema chuo hicho kimepata hati safi kutoka Ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG) na hati safi kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma Public Procurement Regulatory Authority (PPRA)
Amesema siri ya kupata hati safi ni chuo kuhakikisha fedha zote zinazopatikana zinakwenda kwenye matumizi yaliyopangwa ya kuendeleza na kuboresha miundombinu ya chuo hicho.
“Bodi ya uongozi wa chuo imeendelea kusimamia mapato na matumizi ya fedha za chuo na katika kipindi chote hicho chuo kimekuwa kikipata hati safi kutoka kwa CAG na PPRA,” alisema
Vile vile, Profesa Ishengoma ameongeza kuwa taifa linazalisha nafasi chache za ajira kuna uhitaji mkubwa sana wa kutengeneza nafasi hizo hivyo CBE itajitajidi kuzalisha wajasiriamali watakaojiajiri mara baada ya kuhitimu.
Amesema kwa kuzingatia hilo CBE kwa kushirikiana na Shule ya Biashara ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDBS), waliandika andiko la namna wanavyoweza kufanya kutatua tatizo la ajira nchini na kwamba wana imani wakiwa makini watalimaliza.
APP YETU MPYA: Sasa unaweza kusoma kwa urahisi kupitia APP yetu. Download hapa kwa KUBOFYA HAPA
0 Comments