Bodi ya Ushauri ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania imeridhishwa na uendelezwaji wa viwanja vya ndege vya Lake Manyara na Arusha, mara baada ya kufanya ziara katika viwanja hivyo hapo jana Mkoani Arusha na Manyara.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Dr. Masatu Chiguma mara baada ya kutembelea viwanja hivyo vya ndege ikiongozwa na Menejimenti ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) na uongozi wa viwanja hivyo vya ndege.
“Tumeridhishwa sana na maendeleo yaliyofanyika katika viwanja hivi, ukiangalia viwanja hivi vimekaa kitalii na ni sehemu muhimu sana kwa TAA kuweza kujiongezea mapato. Kuna fursa nyingi za kibiashara katika viwanja vya ndege, ambazo ni vivutio kwa abiria vinavyowawezesha kupata mahitaji yao muhimu kabla na baada ya safari zao. Pia tumeridhishwa zaidi na miradi ambayo imekwishakamilika katika Kiwanja cha Ndege cha Arusha ambacho ni muhimu sana katika kuchangia pato la Taifa linalotokana na Sekta ya Utalii” alisema Dr. Masatu.
Awali akitoa taarifa ya Kiwanja cha Lake Manyara, Meneja wa Kiwanja hicho Bw, Hamza Biyonenge alisema, “Kiwanja cha Lake Manyara ambacho kipo katika daraja la pili B kina barabara ya kuruka na kutua kwa ndege yenye urefu wa mita 1220 na upana wa mita 23 yenye hali ya changarawe na ni kiwanja ambacho kipo katika mpango wa uendelezaji viwanja iliyo chini ya ‘Development Corridor Transport Project’ (DCTP) ambayo inafadhiliwa na Serikali na Benki ya Dunia. Ambapo uthamini umeshafanyika na kuthibitishwa na mthamini Mkuu wa Serikali Septemba, 2020 na kukabidhiwa kwa Wakala wa Barabara (TANROADS) ili kulipa fidia kwa wahanga 187 ambao wataathiriwa na mradi huu.
Katika hatua za kuongeza mapato ya kiwanja na kuongeza miruko ya ndege katika kiwanja hicho TAA imefanikiwa kumpata mwekezaji wa mafuta ya ndege (JET–A1), ambaye anatarajiwa kuanza kutoa huduma ya kujaza mafuta hivi karibuni. Uwekezaji huo utaongeza mapato ya kiwanja na kuongeza miruko ya ndege katika kiwanja hicho.
Naye Meneja wa Kiwanja cha Ndege cha Arusha Mhandisi Elipid Tesha akitoa taarifa kwa Bodi hiyo alisema Kiwanja cha Ndege cha Arusha kimeweza kukamilisha miradi mbalimbali katika miaka ya fedha ya 2019/2020- 2020/2021, ambapo umefanyika ujenzi na upanuzi wa barabara ya kuruka na kutua kwa ndege kutoka mita 1640 mpaka mita 1840, matengenezo ya njia za kupita ndege kwa mita 500, ujenzi wa eneo la kugeuzia ndege , ujenzi wa maegesho mapya ya ndege ujenzi wa barabara wezeshi yenye urefu wa kilomita 1.5, usimikaji wa mfumo mpya wa maegesho ya magari, maboresho ya jengo la abiria, ujenzi wa eneo la maegesho ya magari kwa hatua ya kwanza na ya pili.
“Miradi yote hii imewezeshwa na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania na itaongeza uwezo wa Kiwanja katika kutoa huduma bora kwa wadau wake, maboresho ya mapato, kuwezesha uwezo wa Kiwanja katika maegesho ya ndege, ulinzi na usalama wa ndege, kuongeza uhai na utunzaji wa miundombinu ya kiwanja na ongezeko la abiria. Na miradi hii imewezesha ndege aina ya bombardier Q 400-8 kuweza kutua katika kiwanja hicho kwa mara ya kwanza Januari 19, 2021” alisema Mhandisi Tesha katika taarifa yake.
Ziara hiyo ni Muendelezo wa ziara za Bodi ya Ushauri ya TAA, ziara ya kwanza ilifanyika Agosti, 2020 katika Kiwanja cha Ndege cha Dodoma, Kiwanja kidogo cha Kongwa na kutembelea eneo ambalo linatarajiwa kujengwa Kiwanja cha ndege cha Kimataifa cha Msalato.
Mjumbe wa Bodi ya Ushauri ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania Mhandisi Daniel Kihunsi (kwanza kulia) akihoji jambo kwa Meneja wa Kiwanja cha ndege cha Arusha Mhandisi Elipid Tesha(kwanza kushoto) mara baada ya kufanya ziara katika kiwanja cha ndege cha Arusha.
APP YETU MPYA: Sasa unaweza kusoma kwa urahisi kupitia APP yetu. Download hapa kwa KUBOFYA HAPA
0 Comments