**************************************
NA MWANDISHI WETU, DAR
DIWANI wa Kata ya Kivukoni, Sharik Coughle (CCM), amewasilisha maombi katika kikao cha Baraza la Madiwani la Halmashauri Manispa ya Ilala, kumuomba Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania , Dk. John Pombe Magufuli, kumkabidhi baadhi ya majengo yaliyokuwa yakitumika na ofisi mbalimbali kabla ya kuhamia Dodoma.
Diwani huyo aliomba Rais Dk. Magufuli amkabidhi majengo hayo ambayo yako wazi ili yatumike kwa shughuli mbalimbali za kijamii.
Alisema Kata yake ya Kivukoni ina shule moja tu ya msingi ambayo ni Bunge lakini haina shule ya sekondari ya kata, haina zahanati wala kituo cha afya, ofisi ya kata pamoja na huduma zingine za msingi.
Alibainisha kuwa hali hiyo ni kutokana na kata hiyo kuwa kati kati ya Jiji la Dar es Salaam, hivyo kuto kuwa na eneo la wazi la kujenga majengo ya huduma hizo.
“Kwa kipindi kirefu baada ya Rais Dk. Magufuli kuhamishia makao makuu Dodoma, majengo mengi yako wazi katikati ya jiji. Yanaendelea kuchakaa.
Ninamuomba Rais. Dk. Magufuli, kupitia Baraza hili atukabidhi badhi ya majengo ili tuyatumie kwa kuanzisha vituo vya afya, shule ya sekondari na msingi na huduma zingine muhimu kwa wananchi wa Kata ya Kivukoni,”alieleza Choughle.
Diwani huyo alisema, Kata ya Kivukoni ambayo ndani yake ipo Ikulu ya Magogoni, haina maeneo ya wazi ambayo yanaweza kutumika kwa ujenzi wa huduma muhimu kama hizo hivyo ni vema majengo yaliyopo ambayo yako wazi yakatumika.
“Manispaa ya Ilala inatenga fedha nyingi kujenga shule mpya na hata kuongeza madarasa, hospitali na vituo vya afya, kama itampendeza Rais basi tunaomba majengo haya yaliyo wazi yatumike kwa huduma hiyo ili kupunguza hata gharama za ujenzi,”alisema Choughle.
Alibainisha kuwa anaamini Rais Dk. Magufuli ni msikivu na anaweza kulitathimini ombi hilo kwani majengo mengi ya serikali ambayo awali yalikuwa yakitumika kwa shughuli mbalimbali jijini Dar es Salaaam yamebaki kama magofu.
“Naiomba Manispaa ya Ilala kupitia baraza hili tukufu iliwasilishe hili kwa Rais Dk. Magufuli ili tupate majengo hayo.
Kivukoni tunahitaji shule, vyuo vya ufundi, zahanati, vituo vya afya,hospitali, ofisi ya mtendaji na huduma nyingine. Tunaweza kupewa jengo moja kwa shughuli za kiutendaji na jengo lingine kwaajili a shule au zahanati,”alieleza Shoughle.
Alisema Shule ya Msingi Bunge ambayo ni tegemeo, imefurika wanafunzi na miundo mbinu yake imechaka hivyo kuna umuhimu wa kata hiyo kuwa na shule nyingine ya msingi atakayo punguza msongamano katika Shule ya Msingi Bunge.
“Bunge ya sasa siyo ile ya zamani. Imechakaa na watoto ni wengi. Inapoteza hadhi yake ya ubora. Kama tutapata jengo la kuanzisha shule nyingine ya msingi basi Bunge itapumua,”alisema Choughle.
Diwani wa Kata ya Kinyerezi, Leah Mngitu, aliunga mkono hoja hiyo na kuliomba baraza kutilia uzito kwani huduma za wananchi ni muhimu.
“Hili ni wazo zuri na tunaomba liingizwe kwenye umbukumbu za kikao,”alisema Leah.
Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala, Omari Kumbilamoto, alisema tayari Diwani Choughle alishaliwasilisha ombi hilo katika ofisi yake na linaendelea kufanyiwa kazi.
APP YETU MPYA: Sasa unaweza kusoma kwa urahisi kupitia APP yetu. Download hapa kwa KUBOFYA HAPA
0 Comments