JPM AKITAKA KIWANDA CHA MPUNGA KUITANGAZA TANZANIA | ZamotoHabari.

Na Immaculate Makilika- MAELEZO

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli  amekitaka kiwanda cha mpunga kinachozalisha bidhaa za  Korie kuwa na bidhaa zenye jina la kitanzania ili zisaidie kuitangaza nchi kimataifa.

Rais Magufuli ameyasema hayo leo mkoani Morogoro wakati akifungua kiwanda cha Kukoboa Mpunga cha Murzar Wilmar Mill, kilichopo Kihonda  mkoani  Morogoro.

“Natoa rai kwa muwekezaji kutengeneza bidhaa zenye jina linalohusu nchi yetu kwa sababu Tanzania tumekuwa tukizalisha vitu vingi lakini hatutangazi nchi yetu. Siwazuii kuendelea na jina la Korie lakini kuwe na jina jingine linalotangaza nchi”, alisema Rais Magufuli.

Aidha, Rais Magufuli alisema kuwa bila kuwa na viwanda hakuna uchumi, viwanda ndio sehemu pekee inayotengeneza ajira za watanzania, na kuwa alipoingia madarakani aliamua kuhakikisha kuwa katika kipindi cha miaka mitano Serikali inajenga jumla ya viwanda 8,477, sambamba kufikia azma yake ya kutengeneza ajira milioni 8.

“Natoa wito kwa wizara zote zinazohusika na uwekezaji zishirikiane katika kuhamasisha ujenzi wa viwanda na kuleta wawekezaji wa kutosha, watanzania kuwekeza hakuhitaji fedha nyingi, tuzitumie taasisi zetu za fedha katika kuanzisha viwanda”, alisisitiza Rais Magufuli.

Vilevile Rais Magufuli alimpongeza  mwekezaji wa kiwanda hicho kwa kutoa ajira za moja kwa moja 75,000 na ajira  nyingine zisizo za moja kwa moja kwa wakulima,  na kuongeza   kuwa  Tanzania ni mahali pazuri kwa ajili ya kuwekeza  na  kuwa huu ni mwelekeo muafaka wa kuingia uchumi wa kati.

Naye, Afisa Tawala wa Kiwanda hicho, Martha David alisema kuwa kiwanda hicho  kilichojengwa kwa gharama ya dola milioni 21, kina uwezo wa kukoboa mpunga tani 288 kwa siku, na  bidhaa zake  zinazozalishwa zinauzwa nchini pamoja  na nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.

“Katika mwaka wa mazao 2020, kampuni ilipokea zaidi ya tani 65,000 za mpunga kutoka mikoa mbalimbali, pia tumetengeneza ajira za moja kwa moja kwa wananchi 75,000 na zisizo  rasmi 250”, alisema  Martha.





APP YETU MPYA: Sasa unaweza kusoma kwa urahisi kupitia APP yetu. Download hapa kwa KUBOFYA HAPA

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini