KUNA tetesi ambazo inawezekana zikawa siyo nzuri kwa mashabiki wa Klabu ya Yanga, hiyo ni kuhusu suala la vipimo vya wachezaji ndani ya klabu hiyo.
Taarifa ambazo Championi Ijumaa imezipata kutoka ndani ya Yanga zinadai kuwa kumekuwa na tabia ya baadhi ya wasimamizi kufanya hujuma ya kuongeza ‘cha juu’ katika suala la matibabu ya wagonjwa ili kuweza kupata chochote kitu pindi wanapokwenda kufanya vipimo vya nje.
Taarifa hizo zimeibuka wakati huu ambapo wachezaji wawili wa kikosi cha kwanza cha Yanga, Yacouba na Said Ntibazonkiza ‘Saido’ wamekuwa nje ya uwanja kutokana na kuwa majeruhi huku timu yao ikiwa inapata matokeo ya sare mfululizo.
“Hili suala la majeraha ya wachezaji wakati mwingine kuna watu wanafanya vitu tofauti kupitia wagonjwa, kuna vipimo vingine wanakwenda kupimwa vikiwa havina ulazima ilimradi kupata njia ya kutengeneza fedha katika hospitali nyingine.“
Masuala mengine yanakuwa yanaendelea na uongozi haujui, hivyo ni suala linalohitaji umakini wa hali ya juu, mtu haumwi au wanajua kabisa anasumbuliwa na kitu fulani wao wanaenda kumfanyia vipimo tofauti kabisa na anavyoumwa ilimradi tu wapate cha juu,”alisema mtoa taarifa huyo.
Aidha, gazeti hili lilimtafuta Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Fredrick Mwakalebela kuzungumzia juu ya suala hilo ambapo alisema kuwa hana taarifa na suala hilo kwa kuwa ndiyo kwanza analisikia.
Stori:Khadija Mngwai,Dar es Salaam
GPL
APP YETU MPYA: Sasa unaweza kusoma kwa urahisi kupitia APP yetu. Download hapa kwa KUBOFYA HAPA
0 Comments