OFISA MTENDAJI KATA AELEZA CHANGAMOTO ZA KATA YA IJUMBI WILAYANI MULEBA | ZamotoHabari.

 OFISA Mtendaji wa Kata ya Ijumbi iliyopo wilayani Muleba mkoani Kagera, Salehe Mruma amesema Kata hiyo inakabiliwa  na changamoto mbalimbali ikiwemo maji, umeme na  uhaba wa shule za Sekondari kwani iliyopo ni moja ina wanafunzi zaidi ya 1,000.

 Wakizungumza na waandishi wa habari kwa nyakati tofauti Mruma na Diwani wa kata hiyo, Wilbard Musirigi wamesema changamoto hizo zinarudisha nyuma maendeleo ya kata hiyo.

Salehe amesema kata hiyo  ina vijiji vitano, shule za msingi sita na sekondari moja ambayo kila mwaka idadi ya wanafunzi inaongezeka na kufanya mahitaji ya vyumba vya madarasa kuwa makubwa.

" Sasa hivi shule ya Sekondari Ijumbi ina jumla ya wanafunzi 1,070, mwaka huu wanafunzi walioingia kidato cha kwanza ni 342 ambao wanahitaji vyumba saba vya madarasa na tayari  tumeshajenga viwili," amesema Salehe na kuongeza;

"Kuna mahitaji ya Sekondari nyingine, kuna mahitaji ya madarasa na matundu ya vyoo ambayo yanahitajika kila mwaka,"amesema.

Pia amesema kwa sasa  vyumba vya madarasa vipo 21 na wanafunzi jumla 1,070 na kwamba mwaka huu wamefanikiwa kujenga madarasa mawili ambayo yamesimama bado kupigwa plasta.

"Kuna changamoto ya wanafunzi watoro na wengine wanapata mimba, mwaka huu nikimkamata kijana aliyempa mimba mwanafunzi wa darasa la sita nikamkabidhi kwenye vyombo vya sheria,"amesisitiza.

 Diwani wa kata hiyo,  Musirigi amesema wanakabiliwa pia na changamoto ya maji ambapo wananchi wanatembea umbali mrefu kufuata maji.

Amesema maji kwa wenye uwezo wananunua ndoo kuanzia Sh 300 hadi 400 na ambao hawana uwezo wanayafuata kilomita tatu mpaka nne kwenye makorongo.

Ofisa Mtendaji wa Kata ya Ijumbi iliyopo Muleba mkoani Bukoba, Saleh Mruma kulia, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kutaka kuanza kufanyia marekebisho majengo yaliojengwa na mdau wa maendeleo kijijini hapo, Prosper Rweyendera, baada ya kuwakabidhi kwa matumizi ya mbalimbali ikiwemo huduma za Afya, kushoto ni Diwani wa Kata hiyo,Wilbad Kakuru.



APP YETU MPYA: Sasa unaweza kusoma kwa urahisi kupitia APP yetu. Download hapa kwa KUBOFYA HAPA

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini