PROF OLE GABRIEL ATEMBELEA KIWANDA CHA KUZALISHA CHANJO, ATAKA WAZALISHE CHANJO ZENYE UBORA | ZamotoHabari.

MRATIBU na Mkurugenzi wa Operesheni, Kiwanda cha Kutengeneza Chanjo cha Hester, Tina Towo Sokoine amesema kuwa lengo la kiwanda hicho ni kutumia Wataalam wa ndani lakini uhaba wa Wataalam wa masuala ya sayansi wenye ujuzi hasa wa vitendo unaelekea   kukwamisha dhamira yao hiyo.

Towo aliyasema hayo alipokuwa akitoa taarifa ya utekelezaji wa kiwanda hicho kwa Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel alipotembelea kiwanda hicho kilichopo Wilayani Kibaha, Mkoani Pwani Februari 13, 2021.

Alisema kuwa kwa sasa wana wataalamu watatu tu kutoka nje ya nchi ambao wamewaajiri katika Kiwanda hicho lakini   kwa hali ilivyo wanaona watashindwa na labda wanaweza kuomba vibali vingine vya kuajiri wataalamu kutoka nje.

“Nia yetu ni kufanyakazi na Watanzania tu lakini bado vijana wengi tunaowafanyia usahili wanakosa ujuzi hasa wa vitendo, tunaiomba Serikali na Vyuo vinavyoandaa hawa Wataalam kuhakikisha wanajikita katika elimu ya vitendo na sio nadharia peke yake ili kukidhi mahitaji ya sasa na kulinda ajira za Watanzania,” alisema Towo

Kuhusu uzalishaji, Towo alisema kuwa wanatarajia kuzalisha chanjo ya kwanza mwezi wa nne mwaka huu, huku akiiomba Serikali kuona uwezekano wa taasisi zinazohusika na kusimamia uwekezaji kuunganishwa ziwe na lugha ya pamoja ili kumfanya muwekezaji aweze kupata huduma zote sehemu moja bila kuhangaika kama ilivyosasa.

Naye Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel aliutaka Uongozi wa Kiwanda hicho  kuhakikisha wanazalisha chanjo zenye ubora ili nchi iweze kuondokana na utegemezi wa chanjo na bidhaa nyingine za mifugo kutoka nchi za nje.

“Lengo la Wizara ni kuhakikisha kuwa nchi inaondokana na uagizaji wa chanjo kutoka nje, tunatamani kuwa na chanjo tunazoweza kudhibiti ubora wake na tuwe na uhakika nayo, hivyo uwepo wa kiwanda hiki kutatusaidia kuzalisha chanjo hapa hapa nchini ili kukidhi mahitaji ya Wafugaji wetu na Watanzania kwa ujumla,” alisema Prof. Ole Gabriel

Aliongeza kwa kusema kuwa Serikali inaweka mazingira mazuri ya uwekezaji ili mahitaji ya wafugaji na wananchi yawe yanashughulikiwa ndani ya  nchi.

Aidha, Prof. Ole Gabriel aliwaomba Wafugaji na Watanzania kuanza kujenga utamaduni wa kuthamini bidhaa za ndani na waondokane na ile dhana ya kwamba bidhaa bora ni ile inayotoka nje, wakithamini vya ndani wataongeza pato la Taifa na kukuza uchumi wa nchi.

Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel (kulia) akibadilishana mawazo na Mkuu wa Kiwanda cha Kutengeneza Chanjo cha Hester,  Dkt. Umapati Dasgupta (kushoto) muda mfupi baada ya kumaliza kutembelea kiwanda hicho kilichopo Wilayani Kibaha, Mkoani Pwani Februari 13, 2021.
Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Wataalam wa  Kitanzania wanaofanyakazi katika Kiwanda cha kutengeneza Chanjo cha Hester alipotembelea kiwanda hicho kilichopo Mkoani Pwani Februari 13, 2021. Wa kwanza kushoto ni Mratibu na Mkurugenzi wa Operesheni, Tina Towo Sokoine.
Mtaalam wa Kuendesha Mitambo katika Kiwanda cha Kutengeneza Chanjo cha Hester,  Geofrey Mahende (kulia) akitoa maelezo ya namna anavyofanyakazi yake kwa Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel (kushoto)alipotembelea kukagua kiwanda hicho kilichopo Wilayani Kibaha, Mkoani Pwani Februari 13, 2021.
 


APP YETU MPYA: Sasa unaweza kusoma kwa urahisi kupitia APP yetu. Download hapa kwa KUBOFYA HAPA

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini