Zanzibar. Tume ya Utangazaji Zanzibar imekifungia kituo cha televisheni cha Tifu kwa muda wa siku saba baada ya kudaiwa kurusha vipindi vinavyokwenda kinyume na uombolezaji wa msiba wa Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad.
Katibu Mtendaji wa tume hiyo, Omar Said akitoa taarifa hiyo alisema kwamba tume hiyo imelazimika kuchukua uamuzi huo baada ya kubaini kwamba kituo hicho katika kurusha wa vipindi vyake katika kipindi hiki, kinakwenda kinyume na muongozo uliotolewa na Serikali kupitia Tume hiyo.
Alisema kufuatia taarifa iliyotolewa na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi hapo jana juu ya msiba wa Makamu wa kwanza wa Rais, Maalim Seif , tume hiyo ilitoa muongozo wa urushaji wa matangazo na vipindi kwa kipindi hiki cha muda wa siku saba za maombolezo kwa vituo vya televisheni, redio na mitandao ya kijamii.
Alisema katika muongozo huo wamevitaka vituo vyote kubadilisha ratiba zao za urushaji wa matangazo na vipindi, na kuandaa vipindi maalum vya maombolezo katika muda huu wa siku saba, huku wakiweka wazi kwamba hawatakuwa tayari kuona kuna kituo kinakwenda kinyume na muongozo huo.
Alisema licha ya hatua hiyo ya kutoa mwongozo kwa vituo hivyo, lakini kituo cha Tifu kimeonekana kwenda kinyume na muongozo huo, hivyo ililazimika kuchukuliwa hatua hiyo, ili kutoa fundisho juu ya kufuata muongozo wa serikali katika urushaji na uandaaji wa vipindi.
“Kwa kweli hatukutaka kuchukua maamuzi haya kwa chombo hiki, lakini kutokana na kukiuka maadili ya muongozo uliotolewa, imelazimika kuchukua uamuzi huo, ifahamike kwamba maamuzi haya yamekuja kufuatia majadiliano na vyombo vingine mbalimbali vya Serikali, juu ya kitendo hicho, na ikaamuliwa kwa pamoja kichukuliwe hatua za kinidhamu,”alisema.
Said aliviomba vyombo vya habari kufuata kikamilifu muongozo uliotolewa na Serikali kupitia Tume ya Utangazaji juu ya urushaji wa vipindi na utangazaji katika kipindi hiki cha msiba wa Maalim Seif aliyefariki jana wakati akipatiwa matibabu jijini Dar es Salaam.
APP YETU MPYA: Sasa unaweza kusoma kwa urahisi kupitia APP yetu. Download hapa kwa KUBOFYA HAPA
0 Comments